October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Watoto milioni 14.6 wapatiwa chanjo ya polio

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Spread the love

 

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema jumla ya watoto 14,690,597 wametiwa huduma ya chanjo ya polio ya matone sawa na asilimia 118.6 ya malengo waliyojiwekea katika utoaji wa chanjo hiyo.

Amesema awamu ya tatu ya kampeni hiyo ya utoaji chanjo iliyoanza tarehe 1 Septemba hadi 4 Septemba, 2022 chini ya uratibu wa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI ililenga kuwapatia chanjo kwa watoto 12,386,854 wa Tanzania Bara. Anaripoti Juliana Assenga, UDSM …. (endelea).

Taarifa iliyotolewa leo tarehe 14 Septemba, 2022 na Waziri huyo wa Afya amesema ufanisi wa utoaji chanjo ya polio umeonekana kutofautiana kati ya mkoa mmoja hadi mkoa mwingine kwa asilimia kama ifuatavyo;

Kwa ngazi za mikoa takwimu zimeonesha kwa kiasi gani mikoa hiyo imeweza kuvuka lengo ambapo mkoa wa Kilimanjaro umevuka lengo kwa 166.96%, Katavi 129.25%, Dar es Salaam 124%, Geita 122.66%, Lindi 118.60%, Rukwa 117.56%, Morogoro 117.53% na Mbeya 116%.

Aidha, Waziri Ummy amewashukuru na kuwapongeza wakuu wa mikoa, Mkatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu wa Afya, Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Vyombo vya Habari na Wananchi kwa kufanikisha vema utekelezaji wa kampeni hii ya awamu ya tatu.

Pia ametoa wito kwa viongozi wa ngazi mbalimbali, wadau wa maendeleo, wataalamu wa afya, wazazi na walezi kutoa ushirikiano kwa kampeni ya awamu ya 4 na ya mwisho zilizopangwa kutolewa mwezi novemba 2022 kutokana na mlipuko wa ugonjwa huu.

Ummy amewataka kutunza rekodi ya Tanzania na nchi zisizokuwa na ugonjwa wa polio na kuwa wanayo sababu ya kuwalinda watoto na nchi kwa ujumla dhidi ya gonjwa hilo la polio na kuwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo ya polio.

Waziri Ummy amesema ugonjwa wa polio unazuilika hivyo amewasihi wazazi na walezi kuwapeleka watoto katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma hiyo ili kupatiwa huduma hiyo ya chanjo ya polio.

error: Content is protected !!