SERIKALI imeanza utekelezaji wa mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa kuanza kutoa mafunzo ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwa watu takribani 8,900 kwenye mikoa 10. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, leo tarehe 8 Aprili 2024, kupitia ukurasa wake wa Twitter, amesema watakaohitimu mafunzo hayo wataajiriwa serikalini. Amesema watu wenye ujuzi wa afya hawatahusika katika mpango huo.
“Afya ya jamii, nyumba kwa nyumba, kitongoji kwa kitongoji, mtaa kwa mtaa, hatumuachi mtu nyuma. Fursa kwa wananchi wenye umri kuanzia miaka 18 hadi 55, watakaochaguliwa tutawapa mafunzo maalum ya miezi sita (miezi mitatu darasani, miezi mitatu mafunzo) na Serikali itadhamini mafunzo haya,” ameandika Ummy na kuongeza:
“Baada ya mafunzo tunatoa ajira kwao ili waweze kufanya kazi katika vitongoji vyao na mitaani kwao. Lengo kumfikia kila mtanzania alieko mjini au kijijini na huduma bora za afya.”
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, mikoa 10 itakayonufaika katika awamu ya kwanza ya mpango huo ni Geita ambayo itapata wahudumu 920. Kagera (878), Kigoma (1,094), Lindi (1,724), Mbeya (836), Njombe (746), Pwani (480), Songwe (774), Tabora (966) na Tanga (482)
Taarifa ya TAMISEMI imebainisha kuwa, lengo la mpango huo ni kupata wahudumu wawili wa afya ngazi ya jamii, ambao ni mwanamke na mwanaume.
Leave a comment