WIZARA ya Katiba na Sheria imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka wa fedha wa 2024/25 ya kiasi cha Sh. 441.2 bilioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ombi hilo limewasilishwa bungeni jijini Dodoma, leo tarehe 29 Aprili 2024 na Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Pindi Chana, wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2024/25.
Balozi Chana amesema kiasi cha Sh. 112.4 bilioni zimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi, wakati Sh. 223.1 bilioni zikitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo na Sh. 105.6 bilioni zimepangwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo.
Balozi Chana amewasilisha vipaumbele zaidi ya 15 vinavyotarajiwa kutekelezwa na wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha, ikiwemo utungaji wa Sera ya Taifa ya Haki Jinai, kushughulikia masuala ya kikatiba ikiwemo utoaji elimu ya katiba na uraia kwa umma. Kusimamia mfumo wa haki na utoaji haki na kuimarisha miundombinu ya mahakama.
Vipaumbele vingine ni kuharakisha mashauri ya kawaida na kumaliza mashauri ya muda mrefu, uandishi wa sheria na kuimarisha marejeo na ufuatiliaji wa utekelezaji mikataba iliyosainiwa.
Leave a comment