Friday , 17 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Chadema kumshtaki Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the love

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya madai Rais Samia Suluhu Hassan, endapo hatashusha mabango yenye picha yake na baadhi ya viongozi wa Chadema, yaliyobandikwa katika baadhi ya makao makuu ya mikoa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo Alhamisi, kwenye viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu amedai Rais Samia amekuwa akinufaika kisiasa kupitia mabango hayo kwa kuwaaminisha watanzania kwamba hana shida na chama chake, ilihali shida ipo.

“Kwenye kamati kuu ijayo moja ya ajenda tutaiwekea msimamo haya mabango, tukawaambie msipoyashusha tunakushtaki. Rais huwa hashtakiwi kwenye jinai kwenye madai saizi yetu. Tutaenda kumtolea maamuzi kamati kuu ayaondoe haya mabango kwa sababu hatujamruhusu yeye kufanya matangazo ya picha zetu namna hiyo na kufaidika kuisiasa,” amesema Lissu.

Kigogo huyo wa Chadema amedai wana tatizo na Rais Samia ndio maana wanafanya maandamano ya amani yasiyo na kikomo hadi pale madai yao yatakapofanyiwa kazi.

“Samia amepiga picha na viongozi wa Chadema mwaka jana kwenye sherehe za siku ya wanawake duniani, sijui tutaelezana tu na tutaambizana tu sijui ilikuwaje tukamualika lakini tulimualika sababu kulikuwa na kipindi kinaitwa maridhiano, hakuja mwenyewe. Sasa matokeo ya hiyo mialiko hilo bango liko hapo,” amesema Lissu.

Lissu amesema “Mabango ya mama na Chadema lengo lake kuonesha kwamba mama na Chadema hatuna tatizo, haki ya Mungu nawaapieni kama sisi hatuna tatizo na mama tumehongwa.”

Mwanasiasa huyo amesema kuwa, lengo la picha hiyo kubandikwa katika baadhi ya makao makuu ya mikoa nchini ni kuonesha kwamba Chadema na Rais Samia hawana tatizo na kwamba kila watakachosema viongozi wa chama hicho kwa wananchi kuhusu dosari za uongozi wake zipuuzwe.

“Haiwezekani kama hatuna matatizo kwa nini tunaandamana kama mambo ni mazuri. Mabango lengo kuwaonyesheni kwamba kuna namna hamuwezi mkakaa vizuri vile halafu mnalalamika, hivyo lengo kuwafanya nyie mtie shaka msimamo wa Chadema tutakachosema mkitilie shaka, tutakachowaambia msiamini ndiyo maana ya yale mabango,” amesema Lissu.

Lissu amesema Chadema wanaandamana kwa kuwa Rais Samia ameshindwa kutekeleza ahadi yake ya kutimiza maridhiano kwa kufanikisha upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi, katiba mpya na mifumo mizuri ya demokrasia.

Picha iliyoko kwenye mabango yanayolalamikiwa na Chadema ni yale ambayo yana picha ambayo Rais Samia amepiga na baadhi ya viongozi wa chama hicho aliposhiriki maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyoandaliwa na Chadema na kufanyika mkoani Iringa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Udhibiti wa serikali wakera asasi za kiraia

Spread the loveBaadhi ya wadau wa demokrasia na viongozi wa asasi za...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Nape aomba bajeti ‘kiduchu’ kwa mwaka 2024/25

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Seneta: Wanasiasa hawasaidii mchakato wa Katiba mpya

Spread the loveSeneta wa jimbo la Busia, nchini Kenya, Okiya Okoiti Andrew...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

ACT-Wazalendo yasusia uchaguzi wa ubunge Zanzibar

Spread the loveCHAMA cha ACT-Wazalendo, kimegoma kushiriki uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo...

error: Content is protected !!