NCHI ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), leo tarehe 20 Disemba 2023, inafanya uchaguzi wake mkuu huku vigogo watatu, Rais anayemaliza muda wake ambaye pia ni mgombea wa Chama cha UDPS, Felix Tshisekedi, Moise Katumbi (Ensemble) na Martin Fayulu (ECiDe), wakichuana vikali. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Watu takribani milioni 44 wanatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo, ambapo vyama vya siasa 19 vimesimamisha wagombea wake kwenye kinyang’anyiro cha urais.
Mbali na uchaguzi wa rais, wananchi watachagua wabunge na wajumbe wa mabaraza ya wilaya.
Matokeo ya uchaguzi huo yataamua hatma ya mamlaka ya Rais Tshisekedi, aliyeingia madarakani tangu 2018, akichukua mikoba ya Joseph Kabila.
Katika kampeni zake, Rais Tshisekedi anawaomba wacongo wamchague kwa muhula wa pili ili aimarishe usalama wa nchi hiyo kwa kudhibiti makundi ya waasi ikiwemo M23, linalosumbua katika Jimbo la Kivu, lililoko Kaskazini mwa Congo.
Tume ya uchaguzi nchini humo imewaahidi waangalizi wa kimataifa kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, huku mamlaka zikisema mitandao haitafungwa wakati zoezi hilo likiendelea.
Leave a comment