Spika wa Bunge la Afrika Kusini, Nosiviwe Mapisa-Nqakula ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huku kukiwa na uchunguzi wa tuhuma za rushwa wakati akiwa waziri wa ulinzi. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Hayo yanajiri baada ya wiki iliyopita nyumba ya Spika huyo kuvamiwa na maofisa upelelezi, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa tuhuma hizo za rushwa.
Akitangaza kujiuzulu jana Jumatano, Mapisa-Nqakula alisema; “Kujiuzulu kwangu sio dalili au kukubali hatia kuhusiana na tuhuma zinazotolewa dhidi yangu.”
Kujiuzulu huko, ambako kunaanza kutekelezwa mara moja, pia kunaambatana naye kuacha kazi kama mbunge.
Mapisa-Nqakula alikuwa waziri wa ulinzi nchini humo kuanzia mwaka 2012 hadi 2021.
Shirika la utangazaji la serikali ya Afrika Kusini (SABC) liliripoti kwamba anatuhumiwa kupokea mamilioni ya pesa taslimu kama hongo kutoka kwa wakandarasi wa zamani wa kijeshi.
Mapisa-Nqakula alichukua likizo maalum baada ya uvamizi huo na juzi Jumanne, ombi lake kwa mahakama kuzuia mamlaka kumkamata, lilitupiliwa mbali.
Leave a comment