Friday , 3 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mama aingukia Serikali akidai kutishiwa maisha kisa kupigania haki yake
Habari MchanganyikoTangulizi

Mama aingukia Serikali akidai kutishiwa maisha kisa kupigania haki yake

Bertha Mabula Kinungu
Spread the love

BERTHA Mabula Kinungu, mama mjasiriamali mkoani Shinyanga, ameiangukia Serikali akiiomba iingilie kati ili  alipwe fedha zake kiasi cha Sh. 295 milioni, anazodai amedhulumiliwa na Tumsime  Modest Tibaijuka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es salaam…(endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari  hivi karibuni, jijini Dar es Salaam, Kinungu amedai ameamua kuiangukia Serikali baada ya kupata vitisho vya uhai wake na hata kudai baadhi ya Polisi wanataka kumbambikia kesi ya ugaidi, ili kumnyamazisha asidai haki yake.

“Maisha yangu yako hatarini mnyarwanda (Tibaijuka) anatumia vyombo vya dola kupotosha na anatumia polisi wanikamate ili wanifungulie kesi ya ugaidi na kabla ya hapo alishapanga njama za kutaka kuniteka lakini Mungu alinisaidia nilinusurika. Vurugu zote hizo anazileta ili kuninyamazisha nisikate rufaa nikose haki yangu,” alidai Kinungu.

Kinungu alidai kuwa, baada ya kupokea vitisho hivyo aliliripoti kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, ambaye aliahidi kulifanyia kazi suala lake, lakini hakufanya hivyo.

Alidai kuwa, vitisho hivyo viliibuka katika harakati zake za kufuatilia mwenendo wa kesi ya madai No. 3/2023, aliyoifungua dhidi ya Tibaijuka, ili akate rufaa  kupinga hukumu iliyotolewa  kwa madai kuwa ilikuwa na dosari kisheria.

Kinungu anataka kupinga hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Mahimbali Machi 2024, akidai licha ya kuwasilisha mahakamani vilelezo vyote vya ushahidi vilivyothibitisha Tibaijuka hajamlipa fedha, bado jaji alitoa hukumu ya kwamba hana anachodai sababu alishalipwa.

Pia, anadai jaji alikula njama na Tibaijuka kwani alimrejeshea hati ya kiwanda kabla ya siku 60 zinazotakiwa kisheria, baada ya hukumu kutoka.

“Ili kubaini kama kuna njama, jaji alimpa hati ya kiwanda wakati kisheria inatakiwa hukumu inapotolewa ndani ya siku 60 asipewe kwani naweza kukata rufaa kupinga huo uamuzi, lakini alimpa na pia katika hukumu yake hakuzingatia ushahidi wote niliouleta badala yake alitumia maneno ya Tibaijuka ambayo yote yalikuwa uongo,” alidai Kinungu.

“Namuomba Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani anisaidie rufaa isikilizwe na itolewe uamuzi kwa haraka ili nipate haki yangu sababu Tibaijuka kwa sasa anataka kukiuza kiwanda kinyemela kwa mtu mwingine ili nikose haki yangu. Nakata rufaa sababu jaji hajanitendea haki katika mwenendo wa kesi tuliongea mengine na yeye katika uamuzi alitoa maelezo ambayo hayakuwahi kuwepo kama yaliyodai Tibaijuka alisaini mktaba kwa kutishiwa bastola na polisi,” alidai Kinungu.

Anadai kuwa, chanzo cha mgogoro huo ni  Tibaijuka kupitia kampuni yake ya Tunel Incorparation Limited,  kumuomba Mabula kupitia kampuni yake ya Focus For All Limited, washirikiane katika biashara ya utengenezaji vinywaji vikali, ambapo alimtaka ampe Sh. 300 milioni kisha fedha zake zitarudi kupitia faida itakayopatikana.

Anadai, kwa wakati huo fedha alikuwa hana hivyo akamshauri waende benki kukopa lakini walivyofika  Tibaijuka alinyimwa mkopo kwa sababu alikuwa hana vigezo.

Baada ya kushindwa kukopa, Tibaijuka alimtaka Kinungu achukue hati yake ya kiwanda kisha achukue mkopo kwa kuwa yeye anakopesheka, kwa makubaliano kwamba akimaliza kulipa mkopo atamrejeshea hati yake.

Kinungu anadai alikubali ombi hilo mwezi Novemba 2021 na kwenda kukopa mkopo katika Benki ya NMB kiasi cha Sh. 300 milioni huku riba ikiwa Sh. 60 milioni. Anadai Tibaijuka aliishia kulipa Sh. 65 milioni,  kisha aliingia mitini na kushindwa kumalizia Sh. 295 milioni, ambazo anamdai hadi sasa.

“Tulivyochukua mikopo alitakiwa kulipa Sh 45 milioni kila baada ya miezi mitatu, lakini hakupeleka mwisho wa siku alinipa kiwanja chake  akitaka nikiuze mimi nikalipa sh. 45 milioni na baadae yeye akalipa 20, hivyo zilibaki 295, aliahidi kulipa hizo hela benki lakini hakulipa,” amedai Kinungu.

Mabula anadai, kutokana na Tibaijuka kugoma kumaliza kurejesha mkopo huo licha ya fedha kuzichukua, imepelekea lile deni libaki mikononi mwake na mali zake kuwa hatarini kutaifishwa kwa kuwa  NMB inamtambua  yeye mdaiwa.

Kwa mujibu wa mkataba wa makubaliano kati ya Kinungu na Tibaijuka, ambayo mwandishi ameuona, ulimtamka kuweka fedha hiyo katika akaunti namba 30610019953 kwenye benki ya NMB, ya kampuni ya Kinungu ya Focus For All Limited, lakini hakufanya hivyo.

Inadaiwa kuwa, masharti ya mkataba huo yalielekeza mali zilizomo kiwandani humo zitakuwa chini ya Kinungu hadi pale Tibaijuka atakapomaliza kulipa deni, lakini taarifa zilizopo zinadai baada ya mfanyabiashara huyo kupewa kinyemela hati ya kiwanja na mahakama, anapanga njama za kukiuza kwa mtu mwingine ili kukwepesha haki kutendeka.

Alipotafutwa na waandishi wa habari ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, Kamanda Magomi alikana kulifahamu suala hilo na kumtaka mhusika afike ofisini kwake akaripoti ili lifanyiwe kazi.

Kamanda huyo wa Polisi amekana kumfahamu Kinungu, licha ya mhusika kudai alishawahi kuzungumza naye kwa njia ya simu.

“Mimi hizi taarifa sina na bahati nzuri huwa nina tabia ya kukagua vitabu hivyo hizo taarifa sina. Kwanza hata simjui, wala simjui. Yeye kwa mujibu wa taarifa zenu anasema alikuja kwangu? Au nimesahau kama binadamu sikumbuki, unajua kufanya kazi kwenye simu kama binadamu unaweza kusahau lakini mtu akija kuripoti ofisini huwezi kusahau,” alisema Kamanda Magomi.

Alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu madai ya kula njama na polisi ili amfungulie kesi ya ugaidi kwa lengo la kumnyamazisha, Tibaijuka alikana kuhusika katika tukio hilo.

“Huyo mama namfahamu, nilikuwa nashtakiana naye mahakamani na hukumu ilitoka nimeshinda. Sasa hizo taarifa za kuwatuma polisi wamfungulie kesi ya ugaidi hayo siyajui mimi ila ninachofahamu ilikuwepo kesi na ikaamriwa na mahakama haya mambo ya kumtishia maisha siyafahamu,” alidai Tibaijuka.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

BiasharaHabari Mchanganyiko

NMB yang’ara maonesho OSHA

Spread the loveBenki ya NMB imebeba tuzo ya kampuni bora kwenye sekta...

Habari MchanganyikoKimataifa

Ruto amteua Kahariri kuwa mkuu wa majeshi

Spread the loveRAIS wa Kenya, William Ruto, amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri,...

error: Content is protected !!