Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Vijana wanavyoandaliwa kuziba pengo la ujuzi sekta ya madini
Makala & Uchambuzi

Vijana wanavyoandaliwa kuziba pengo la ujuzi sekta ya madini

Spread the love

MOJAWAPO ya sekta ambazo katika miaka ya 2000 hazikuwa na vijana wenye ujuzi wa kutosha kutekeleza shughuli mbalimbali, ni ya uchimbaji wa madini.

Mathalani katika uchimbaji wa kina kifupi juu ya ardhi (open pit mining) ambayo kampuni nyingi zilizokuja kuwekeza nchini zilitumia aina hii ya uchimbaji, uliwaweka kando Watanzania wengi kujihusisha na shughuli hizo.

Hata hivyo, juhudi mbalimbali za wadau wa madini na Serikali zimefanikisha kuziba pengo hilo la uhaba wa wataalamu, lakini sasa kampuni nyingi zimehamia kwenye uchimbaji wa kina kirefu chini ya ardhi (Underground Mine).

Hii ina maana kuwa mbali na kuhitaji watalaamu hawa sasa wa uchimbaji wa aina hii ya pili, lakini kunahitajika viongozi watakaosimamia sekta hii kwa umadhubutu lakini pia kuwepo na watenda kazi wenye ujuzi wa kutosha ikilinganishwa na nchi mbalimbali ambako kunapatikana madini.

Mojawapo ya wadau walioshiriki hatua mbalimbali za kuwezesha ujuzi kwa vijana wa Kitanzania ni Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), ambayo inatajwa kuwa mdau mashuhuri katika tasnia ya madini nchini Tanzania. Kwa zaidi ya miongo miwili kampuni hii imekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia suala muhimu la uhaba wa ujuzi na ukuzaji vipaji ndani ya sekta hiyo.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, GGML haijazingatia tu ubora wa utendaji kazi bali pia kuwekeza katika nguvu kazi ya baadaye ya Tanzania.

Kwa kutambua umuhimu wa kuandaa wafanyakazi wa baadaye na kukuza vipaji vya vijana wa Kitanzania, GGML, kwa kushirikiana na wadau wengine, ilitoa mchango wa zaidi ya dola za Marekani milioni mbili mwaka 2009 katika kuandaa mitaala ya Programu ya Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya Uchimbaji Madini (IMTT) kwa vijana wa Kitanzania kupitia Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Moshi.

Mpango huu umezaa matunda kwa miaka mingi, ambapo zaidi ya vijana 1,400 walipata mafunzo ya uchimbaji wa kina kifupi juu ya ardhi (open pit mining), na hivyo kusaidia kupunguza uhaba wa ujuzi katika sekta hiyo.

Hata hivyo, dhamira ya GGML katika kukuza vipaji inazidi mafunzo ya ufundi stadi. Mnamo 2009, kampuni hiyo ilizindua mpango wa kuajiri wahitimu ili kutoa fursa za mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa vyuo vikuu wasio na ajira.

Programu hiyo ilikuwa na idadi ya wahitimu 12 kila mwaka hadi kufikia mwaka 2012 ilisitishwa kabla ya kuendelea tena mwaka 2017. Hata hivyo, katika kuwaongezea uthamani wahitimu wa programu hiyo ya mwaka mmoja, safari hii GGML imeongeza programu nyingine iliyopewa jina la African Business Unit Graduate Programu – ABU.

Baada ya programu ya awali kusitishwa kwa miaka mitano, kisha kuanza tena mwaka 2017, vijana waliofanikiwa kuingia kwenye mafunzo hayo tarajali, GGML iliwapa vijana wa Kitanzania uzoefu muhimu wa kufanya kazi katika nyanja mbalimbali ndani ya kampuni hiyo huku ikiwaruhusu kubobea zaidi katika fani zao. Kati ya 2017 na 2023 GGML ilichukua wahitimu 194 kwa programu yake ya mafunzo tarajali.

Februari 2024, GGML ilizindua mpango wa wahitimu wa Kitengo cha Biashara cha Kiafrika (ABU). Wahitimu 10 kundi la mafunzo tarajali kwa mwaka 2023/24, ambao walionyesha uwezo wa kufanya kazi kwa bidii na hamu ya kujifunza katika muda wao wa mafunzo, walichaguliwa kuendelea programu mpya ya ABU.

Meneja Mwandamizi wa Rasilimali Watu kutoka GGML, Charles Masubi, anafafanua kuwa program hiyo ya ABU inalenga kuandaa viongozi na wabobezi wa  baadae katika sekta ya madini.

“Programu ya ABU inawapa wahitimu kutoka vyuo mbalimbali fursa ya kujifunza wa kina zaidi kuliko mafunzo tarajali ambayo hupatiwa kwa muda wa mwaka mmoja.

“Washiriki kupitia mafunzo hayo yanayolenga kuimarisha ujuzi wao, maarifa na uwezo wao wa uongozi chini ya ushauri wa wataalamu waliobobea, watajengewa uzoefu huo kwa kupitia migodi ya AngloGold Ashanti ambayo ipo katika nchi za Guinea na Ghana” anasema.

Masubi anasisitiza kuwa wahitimu wanaofanya vizuri katika programu hiyo sio tu kwamba wanahusishwa na mipango kama hiyo katika migodi mingine ya Afrika chini ya AngloGold Ashanti lakini pia wanapewa mafunzo ya ujuzi wa hali ya juu unaoendana na fani zao.

Mbinu hii inalenga kuwapa washiriki ujuzi unaohitajika ili kustawi katika tasnia shindani huku ikikuza utamaduni wa kuendelea kujifunza na kukua.

Anasema Programu ya Wahitimu – ABU unasimama kama ushuhuda wa dhamira ya GGML ya kukuza vipaji na kuwawezesha watu kupaa hadi kwenye majukumu ya uongozi ndani ya kampuni  hiyo na kwingineko. Kwa kuandaa hazina ya baada ya vijana wenye ujuzi stahiki, GGML haiwekezaji tu katika nguvu kazi yake bali pia inachangia maendeleo ya sekta ya madini ya Tanzania kwa ujumla.

Baadhi ya wahitimu wa mafunzo tarajali mwaka jana ambao wameendelea na Programu ya ABU mwaka huu, ni   Evelyne Julius, na Mkunde Frank ambao wanathibitisha kwamba mbinu na ubunifu unaotumiwa GGML katika kuandaa kizazi kipya cha viongozi kwenye sekta ya madini, imeendelea kuibua ari kwa vijana kusomea masomo ya sayansi yale yenye muelekeo wa sekta ya madini.

Evelyne Julius ambaye ni mhandisi wa masuala ya umeme naye anasema “nimejifunza vitu vingi. Uwepo wangu GGML ni fursa ya kipekee kwa sababu nitaweza kutekeleza miradi mbalimbali kwa ujasiri na ujuzi nilioupata,” alisema.

Mkunde Frank ambaye ni mteknolojia wa masuala ya jiolojia, naye anasema nafasi aliyoipata ya kuendelea kufanya kazi ndani ya GGML kupitia progamu ya ABU, imeendelea kumjengea kujiamini na kunoa zaidi ujuzi wake.

“Mathalani kwenye kitengo cha geolojia tumepata fursa ya kipekee, kila mfanyakazi anapewa uthamani bila kujali mkubwa au mdogo. Lakini hata ukishuka kwenye machimbo chini ya ardhi kila mfanyakazi anazingatia mafunzo aliyopewa kwa vitendo hasa katika kutekeleza kipaumbele cha kwanza ambacho ni usalama,” anasema.

Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Ujuzi kutoka Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Albert Rukeisa anasema hitihada hizo za GGML kwa zaidi ya miaka 15 zimekuwa chachu kwa waajiri wengine kuendelea kutoa nafasi kwa vijana kujifunza na kuongeza wataalam wa madini katika sekta hiyo. Makala imeandaliwa na Gabriel Mushi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Je, miji ya Uingereza inafilisika?

Spread the loveMNAMO 1890, mwandishi mmoja wa habari Mmarekani aitwaye Julian Ralph...

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

error: Content is protected !!