Tuesday , 30 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?
Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Wakazi Kipunguni
Spread the love

WATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu, basi wafuatilie kuona ilivyofunga masikio yake kusikiliza malalamiko ya wananchi zaidi ya 1,800 wa maeneo ya Kipunguni, jijini Dar es Salaam, wanaodai fidia ya Sh. 147 bilioni baada ya maeneo yao kuchukuliwa kupisha upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Anaripoti Regina Mkonde… (endelea).

Serikali ilianza mchakato na utekelezaji wa mpango wa utwaaji maeneo hayo tangu mwaka 1997 baada ya kufanya tathmini kwa wananchi wa Kipawa, Kigilagila na Kipunguni.

Rekodi zinaonesha kwamba mwaka 2009 wakazi wa Kipawa na Kigilagila walilipwa stahiki zao kisha mwaka 2014 wakazi 59 kati ya 1,919  wa Kipunguni walilipwa. Kwa kuwa muda ulikuwa umepita sana, waliosalia walifanyiwa tathmini upya mwaka 2022 na kupewa matumaini ya kulipwa.

Kwa kuwa tangu maeneo yao yafanyiwe tathmini hawapaswi kuyaendeleza, wananchi hao walianzisha juhudi za kuonana na viongozi mbalimbali pamoja na kuwatumia wabunge wao ili waishinikize serikali lakini hawakufanikiwa.

Desemba 2023 walimwandikia barua Waziri wa Uchukuzi wakiomba aingilie kati walipwe fidia yao, lakini hawakufanikiwa. Halafu, Machi mwaka huu walimwandikia barua Waziri awezeshe wakutane na Rais Samia Suluhu Hassan ili wamjulishe kuhusu mgogoro wa malipo yao maana hawajui kinachosababisha mkwamo.

“Tunaomba kuonana na wewe ili kukujulisha madhila tunayopitia tangu tathmini ifanyike kwenye maeneo yetu kupisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha JNIA. Hii ni kwa sababu suala la hapa limekuwa sugu sana kwani limeanza tangu 1997,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Septemba 2023 wawakilishi wa wananchi hao walikwenda bungeni Dodoma kuzungumza na Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba kuhusu malipo yao. Katika mazungumzo hayo Dk. Mwigulu aliwaahidi watalipwa fedha zao mapema kwa kuwa zimeshatoka.

Miezi miwili baadaye, Novemba 2023, Mbunge wa Segerea, Bonna Kamoli (CCM), akiwa bungeni jijini Dodoma, alikumbusha utekelezaji wa ahadi hiyo. Katika majibu yake Dk. Mwigulu alisema kwamba zoezi hilo lilichelewa kwa ajili ya kupisha uhakiki baada ya kuona baadhi ya wasiostahili kulipwa kuwepo katika orodha ya wanaotakiwa kulipwa.

“Wananchi tulitaka tuwalipe Septemba kilichochelewesha siyo kwamba fedha za kuwalipa fidia zilikosekana, isipokuwa ulipofanyika uhakiki, ilibainika kuna miongoni mwao walishapewa maeneo mengine, lakini majina yalikuwepo kwenye fidia. Kwa maana hiyo, ingeweza kulipa fidia mara mbili, wengine wakawa hawajaridhika na fidia ilitakiwa ufanyike utaratibu baada ya kumaliza mzozo ndani ya mwezi mmoja tutaenda kulipa,” aliahidi Dk. Mwigulu akiwa bungeni Novemba 2023.

Tarehe 8 Aprili 2024, Naibu Spika, Mussa Azan Zungu, aliibua sakata hilo tena bungeni kwa kumhoji Dk. Mwigulu ni lini wananchi wa Kipunguni na wengine ambao wanadai fidia baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali, watalipwa haki zao.

“Kuna fidia ambayo inadaiwa, Kipunguni walipisha uwanja wa ndege wa Dar es Salaam. Hawa wananchi wanalalamika sana na tulishawahi kwenda pale lakini fidia yao bado haijalipwa, ni lini sasa watalipwa?” alihoji Zungu.

Kama ilivyo ada yake, Dk. Mwigulu alitoa majibu yaleyale ya 2023 kwamba italipwa baada ya uhakiki kufanyika ili kuondoa wasiostahili katika orodha ya wanaopaswa kulipwa.

“Kilichotokea ni kwamba ilikuja kugundulika kuna baadhi ya maeneo mbadala yalikuwepo na kuna baadhi walikuwa wanahitaji fidia zaidi, kilichofanyika tulipeleka timu kuweza kuainisha namba na jambo hilo limeshafanyika tunatafuta fedha ndani ya kipindi hiki cha mwaka wa fedha unaoendelea ili tuanze kufanya malipo na tutaanza na wale ambao madai yamehakikiwa na hayana vikwazo vyovyote,” alisema Dk. Mwigulu.

Hatua za sasa

Sasa wananchi wamechoka ahadi za Dk. Mwigulu. Kwa kuwa walitumia taratibu za kiitifaki kumwandikia barua Rais Samia ili waonane naye lakini hawajafanikiwa, wanaomba akisoma gazeti la MwanaHALISI au akiambiwa na wasaidizi wake aingilie kati wapate haki yao.

“Tunamtaka Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba akae pembeni katika kushughulikia suala hili kwa kuwa hatuna imani naye. Tunamuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, aingilie kati ili tulipwe fedha zetu. Dk. Mwigulu amekuwa akitoa ahadi hewa na kutoa sababu ambazo hazina uhalisia,” alisema Katibu wa wananchi hao, Aseri Simon.

“Kwanza Dk. Mwigulu anasema walikwama sababu kuna mgogoro. Nilishamtaarifu mwaka jana Oktoba huku hakuna mgogoro wala hakuna kitu kama hicho ila anatumia kauli hiyo bungeni kupotosha Bunge na kuhadaa watu kwani hakuna mgogoro,” alisema Simon.

“Anachosema Dk. Mwigulu ni uongo tena sio wa dunia hii, ni uongo wa dunia nyingine. Hata kwenye kauli zake anababaika; mara aseme hela wanazo, mara wanatafuta. Tunachotaka Rais Samia apate habari hizi maana anadanganywa. Huku hakuna mgogoro, sababu tathmini imeshafanyika na huyo Dk. Mwigulu ametuma watu kuja kuhakiki mara mbili na walimaliza uhakiki Septemba 2023, ilibaki kitendo cha kulipwa,” alisema Simon.

Simon anamwomba Rais Samia aingilie kati ili yeye na wenzake zaidi ya 1,800 wanaodai fidia ya Sh. 147 bilioni, walipwe kwani wapo wenzao zaidi ya 30 wamefariki dunia wakisotea haki yao.

Mkazi mwingine Beatrice Kimanga, anasema, “Tunapitia adha kubwa, watu wamevunja nyumba zao wanalala nje na hii mvua inawanyeshea, wengine nyumba hazina wapangaji, usalama hakuna, kuvamiwa na wezi ni vitu vya kawaida baada ya nyumba kuvunjwa na kuna mapori. Hali iliyopo tunazuiwa hata kufanya vikao kujadili namna gani tunapata haki yetu, tukijaribu kukutana tunaletewa polisi.

“Tunahangaika na hakuna mahali ambako hatujaenda tumeanzia kwa mkuu wa wilaya hadi wizara ya fedha. Sisi tunachotaka tupewe fidia zetu tuondoke tuende mahali ambako salama. Hatuna imani na Dk. Mwigulu tunataka Rais Samia aseme neno atusaidie tupate haki yetu,” amesema Kimanga.

“Walipofanya tathmini upya 2022 walikuja mpaka watu wa benki ya NMB, wakatufungulia akaunti tukiamini tutaingiziwa hela, lakini sasa ni miaka miwili hatujaona hela. Mwigulu anajikanyaga tu,” alisema Pius Otaigo.

Naye Hussein Kabobo alisema, “Nimeathirika sana. Sisi wa upande wa mashariki tunapakana na pori la jeshi, tunakabiliwa na tishio la kiusalama, mwezi mmoja umepita tangu maiti tatu zitupwe kwenye maeneo ya makazi sababu ni pori. Pia wanatupa takataka sababu ya mapori ya maeneo ambayo watu wamevunja nyumba wakiamini watakuja kulipwa na serikali wakatafute makazi mengine.”

Wakazi wengine waliolalamikia ahadi hewa za serikali ni Method Hanta, Athanas Nyambari, Robert Shija ambaye alisema; “Waliovunja nyumba ni wengi, hebu fikiria unaaminishwa hela zinakuja karibuni halafu ndiyo maajabu hayo yanayotokea. Dk. Mwigulu labda ana ajenda na Rais, kama alisema mama ana hela akaahidi atalipa, leo kiko wapi?”

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

TMA yapongezwa kuimarisha ubora na usahihi wa taarifa za Hali ya Hewa

Spread the love  WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA),...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

7 wafa Ulanga, mbunge alia kutelekezwa na mawaziri, Tanroad

Spread the loveWatoto saba wamepoteza maisha na zaidi ya kaya 70 kukosa...

Habari Mchanganyiko

Bil 12.4 zimetumika ujenzi wa miradi wilaya ya Momba

Spread the love MKUU wa wilaya ya Momba mkoani Songwe Kennan Kihongosi...

AfyaHabari Mchanganyiko

Songwe katika mikakati ya elimu ya lishe kudhibiti udumavu

Spread the love  SERIKALI mkoani Songwe imejipanga kuendelea kutoa elimu ya lishe...

error: Content is protected !!