Sunday , 19 May 2024
Home Kitengo Michezo TFF, Amrouche ngoma nzito
Michezo

TFF, Amrouche ngoma nzito

Adel Amrouche
Spread the love

VIPENGELE vya mkataba wa kazi aliotia saini Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars,’ Adel Amrouche vimeliweka katika wakati mgumu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuachana naye. Anaripoti Erasto Masalu… (endelea).

Amrouche, raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Algeria, aliyesaini mkataba wa miaka mitatu kuinoa kikosi cha Taifa Stars, yupo nje ya uwanja baada ya kufungiwa michezo nane na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) ikiwa pamoja na kufungiwa kwa muda usiojulikana na TFF kutokana na kauli yake ya kuishutumu Morocco katika fainali ya AFCON zilizopita.

TFF ilimsimamisha Amrouche mara tu baada ya kufungiwa na Caf lakini haikuweka wazi kifungo chake ni cha muda gani huku Serikali ikiendelea kumlipa mshahara wake kama ilivyokuwa katika makubaliano ya mkataba wao.

Taarifa zilizopatikana kutoka ndani ya shirikisho hilo, zinasema kuwa walikuwa tayari kuvunja mkataba huo lakini kama wakifanya hivyo watatakiwa kumlipa kocha huyo mamilioni ya fedha kama fidia ya kuvunja mkataba wake.

“Kama nilivyokwambia hakuna anayehitaji kuendelea na Amrouche (Adel), TFF walikuwa tayari kuvunja mkataba lakini wakashtuliwa na kiongozi mmoja kuwa kufanya hivyo watatakiwa kumlipa fedha nyingi sana, hivyo wakaachana na mpango huo,” alisema afisa mmoja wa TFF.

“Mpango wa sasa ni kukaa naye chini (Adel Amrouche) ili kukubaliana pande zote mbili namna ya kuweza kuachana kwa faida ya kila upande.”

Mwezi uliopita MwanaHALISI lilipomhoji Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau juu ya  hatma ya Amrouche, majibu yake yalikuwa, “Maswali yote muulizeni Ndimbo (Clifford Mario – afisa habari wa TFF), atawapa ufafanuzi.”

Ndimbo alipoulizwa alijibu, “Suala la Amrouche, TFF itakutana na kocha baada ya kumalizika michezo ya kalenda ya FIFA inayofanyika Azerbaijan ili kujadili mustakbali wake.”

TFF haikupanga tarehe ya kukutana na Amrouche lakini mashindano ya Fifa Series yalimalizika na timu hiyo iliyokuwa chini ya Hemed Morocco aliyekuwa kocha msaidizi tangu kocha huyo kusimamishwa na Caf katika fainali za AFCON ilikwisha kurejea.

Juzi Jumanne MwanaHALISI liliamua kumtafuta tena Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau lakini hakupatikana na simu ya Ndimbo ilikuwa ‘bize’. Baadaye alipatikana Mkurugenzi wa Michezo, Ally Mayai, lakini alipopokea alijibu kwa sauti ya chini: “niko kwenye kikao.”

Kwa kuwa kocha huyo analipwa na serikali, MwanaHALISI lilifanya juhudi za kumpigia simu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro lakini hakupokea.

Baada ya kumkosa Waziri Ndumbaro, MwanaHALISI lilimtafuta naibu wake, Hamis Mwinjuma, ambaye alipokea simu lakini alipoulizwa kuhusu hatma ya Amrouche na kwamba serikali itaendelea hadi lini kumlipa mshahara bila kufanya kazi, alisema yupo katikati ya kikao hivyo atafutwe baadaye.

Hasira za CAF

Kibarua cha Amrouche kilitatizika tangu wakati wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Januari mwaka huu nchini Ivory Coast. Mwishoni mwa Januari, MwanaHALISI lilijulishwa kwamba hatima ya kocha huyo ilikuwa inasubiri kikao cha TFF baada ya kumalizika kwa fainali hizo.

“Hamna mtu anayemtaka ndani ya TFF. Safari yake ishaiva yule, haponi yule, alikuwa anatafutiwa sababu na sasa imepatikana,” alisema afisa mmoja wa shirikisho. Alikuwa anajibu swali “hivi suala la kocha limekaaje, anaweza kuwa na maisha marefu kutokana na sakata hili?”

Kuvunjika kwa ndoa hiyo kulitokana na matukio kadhaa ya kocha huyo kuelekea katika fainali hizo za Afcon na zaidi ni shutuma zake dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (FRMF).

Amrouche, wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya mchezo wao dhidi ya Morocco aliwashutumu FRMF kuwa wanaishinikiza CAF kuwapangia ratiba zinazowabeba ikiwa ni pamoja na kuwapangia muda mzuri wa wao kucheza mechi.

Haraka Rais wa TFF, Wallace Karia alijitokeza na kujibu kuwa huo si msimamo wa shirikisho la soka nchini bali ni maoni binafsi ya kocha. Hata hivyo, kauli hiyo haikuokoa hasira za CAF.

Kwanza, CAF ilimpa kocha huyo adhabu ya kutokusimamia Stars katika mechi nane. Pili, TFF ilitozwa faini ya dola za Kimarekani 10,000 sawa na Sh. 25 milioni. Kutokana na TFF kuadhibiwa, nalo liliamua kumsimamisha kwa muda usiojulikana.

Kwa kuwa Stars bado ilikuwa inakabiliwa na mechi mbili dhidi ya Zambia na dhidi ya DR Congo, TFF ilimkaimisha ukocha mkuu, Ahmed Morocco aliyekuwa msaidizi wa Amrouche, na pili likamteua, kocha wa timu ya wanawake ya Simba, Juma Mgunda na kumsafirisha hadi Ivory Coast kuwa msaidizi wa Morocco. Amrouche alirejeshwa Dar es Salaam kusubiri hatima yake.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Michezo

Uingereza, Hispania, Italia na Ufaransa kinawaka leo

Spread the loveLIGI mbalimbali barani ulaya kuendelea leo na michezokadhaa mikali itakwenda...

Michezo

Leo mkwanja upo Meridianbet, usipishane nao

Spread the love  Siku ya leo ni nzuri sana kwa wewe mtumiaji...

Michezo

Anza wikendi yako na Meridianbet, upige mkwanja wa maana

Spread the love Siku ya leo ni nzuri sana kwa wewe mtumiaji...

Habari MchanganyikoMichezo

Arafat atoka bima na kurejea kwenye benki

Spread the loveRais wa Zanzibar Hussein Mwinyi amemteua Arafat Ally Haji kuwa...

error: Content is protected !!