Monday , 6 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Hivi kweli Ole Sendeka alishambuliwa kwa risasi?
Habari za Siasa

Hivi kweli Ole Sendeka alishambuliwa kwa risasi?

Spread the love

MIMI siamini kwamba yupo mtu mwenye nia ya kuua ambaye amepanga mashambulizi kwa kutumia bunduki anayeweza kumrushia risasi Christopher Ole Sendeka na akamkosa, haiwezekani, labda mtu huyo awe hajui kurusha risasi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Nasema hivi kwa sababu mwili mkubwa, mwili mnene na mwili wenye tumbo kuubwa kama wa Ole Sendeka huwezi kukosea shabaha. Yaani wewe unachotakiwa kufanya ni kuelekeza bunduki tu pale alipo Ole Sendeka na risasi inampata.

Kwa muuaji aliyeaminiwa na kutumwa kumuua kwa bunduki mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, halafu aende amlenge bunduki na akamkosa ni sawa na mwindaji kumlenga kiboko risasi na akamkosa. Limwili lote lile unakosaje?

Nasema haya kama mtu ninayefahamu matumizi ya bunduki na risasi. Mimi nilisomea ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Katoke ambacho kilitoa pia mafunzo ya kijeshi na pia nilikuwa Operesheni Kagera ambayo niliingia JKT kwa mujibu wa sheria huku vita ikirindima uganda na nikahusika kwa kiwango chake.

Baada ya Operesheni Kagera, mapema Julai 1979 huku muda wangu wa JKT haujaisha nilirushwa moja kwa moja hadi Nachingwea mkoani Lindi nilikoshiriki operesheni ya kusafirisha wapigania uhuru wa Zimbabwe ya Robert Mugabe kutoka Farm 17 kwenda Mtwara.

Pale Mtwara wapigania uhuru wale walichukuliwa usiku wa manane na madege makubwa sana ya Nigeria hadi Beira, Msumbiji na madege yale kutoka Beira hayakurudi tena Mtwara na hivyo ni sisi wachache sana tunaofahamu kama Nigeria ilihusikaje katika airlifting hiyo.

Maana yangu ni kwamba nilitoka katika matumizi ya bunduki katika Operesheni Kagera nikaenda Lindi na Mtwara ambako niliendelea kubeba bunduki begani masaa 24 katika kutekeleza majukumu hayo. Ninajua sana matumizi ya bunduki, milipuko na ulengaji shabaha hivyo Ole Sendeka hawezi kunidanganya.

Kwa hiyo Ole Sendeka anapokuja na hadithi zake za Alinacha kwamba waliomrushia risasi siyo wana CCM au kwamba warushaji risasi siyo mawakala wa serikali ajue kwamba sisi tuna vichwa vyenye bongo na hatukubeba  maboga mabegani.

Baada ya kupata habari kwamba mbunge wa Simanjiro mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka, amenusurika baada ya watu wasiojulikana kushambulia gari lake kwa risasi, tulitaraji mbunge huyo angetoa taarifa ya ukweli nini kilitokea.

Shambulio hilo, kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime, kwamba mbunge huyo alikuwa safarini katika kijiji cha Ngabolo wilayani Kiteto na kwamba lilitokea Machi 29, 2024 .

Msemaji wa Polisi DCP Misime alisema Machi 30 mwaka huu kwamba “Jeshi la Polisi limepokea taarifa hiyo, Ole Sendeka na dereva wake wote hawajapata madhara, uchunguzi umeanza mara tu baada ya kupokea taarifa.”

DCP Misime aliongeza kwamba “timu ya wataalamu wa matukio yaliyohusisha matumizi ya risasi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma imetumwa kwenda kushirikiana na timu ya Manyara kubaini wahusika na madhumuni yao au kusudio lao na kwamba baaada ya uchunguzi taarifa itatolewa.

Sikushangazwa na hilo la Polisi haraka haraka kutuma timu ya wataalamu wa mashambulio ya risasi kuchunguza tukio hilo ila nimeshangazwa sana na taarifa ya Ole Sendeka kwamba serikali ya CCM haihusiki na shambulio hilo dhidi yake.

Kwenye mitandao ya kijamii nimesoma kwamba “Mbunge wa Simanjio Christopher Ole Sendeka, amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, haihusiki na kushambuliwa kwake kwa risasi akiwa katika gari lake.

“Akizungumza kwenye mji mdogo wa Orkesumet jana Jumatatu (Aprili Mosi) Ole Sendeka amesema anaiunga mkono serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivyo haihusiki na jaribio la kutaka kupoteza maisha yake.”

Ole Sendeka aliongeza kwamba “siwezi kusema CCM imenishambulia kwa risasi, nina imani nayo. Hivyo serikali hii haiwezi kunishambulia kisha niiunge mkono.”

Kutokana na maelezo haya ya Ole Sendeka na DCP Misime, tumejifunza mambo mengi; kubwa moja likiwa kwamba wapo wataalamu wa matukio ya kutumia silaha za moto pale Makao Makuu ya Polisi ambao sasa wanachunguza tukio la Ole Sendeka.

Pili, kwamba watalamu wa matukio ya silaha za moto hufanya uchunguzi wa matukio ya kutumia silaha za moto pale tu mwanachama wa CCM au kiongozi wa CCM au kiongozi wa serikali ya CCM au mfanyakazi wa serikali ya CCM anaposhambuliwa.

Tatu, kwamba mtu mwingine hivihivi kama vile mwanachama wa chama cha upinzani, kiongozi wa chama cha upinzani au mfanyakazi katika ofisi za chama cha upinzani akishambuliwa kwa silaha za moto timu ya matukio ya silaha za moto kutoka Makao Makuu ya Polisi hailazimiki kuchunguza.

Wenzangu wameniambia kwamba hii ndiyo sababu tukio la kushambuliwa kwa risasi kwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Antipas Lissu, mchana wa saa saba kwenye eneo la makazi ya viongozi mjini Dodoma mwaka 2017 halijachunguzwa hadi leo.

Jambo la nne tulilojifunza kutokana na maelezo ya Ole Sendeka na DCP Misime ni kwamba CCM na hasa Ole Sndeka wanawajua washambuliaji wanaotumia silaha za moto na wanaweza kufahamu ni wapi wamehusika na wapi hawakuhusika.

Ole Sendeka anaposema kuwa serikali ya awamu ya sita ya Samia Suluhu haikuhusika na shambulizi dhidi yake ni kwamba anawajua ni akina nani wamehusika kumshambulia na kwamba washambuliaji hao si waajiriwa au watu waliotumwa na Serikali ya Samia.

Jambo la tano tunalojifunza kutokana na maelezo ya DCP Misime na Ole Sendeka ni kwamba washambuliaji hawakutaka kumdhuru Ole Sendeka ndiyo maana pamoja na ukubwa wa mwili na tumbo lake walipiga risasi tano na zote zikamkosa yeye na dereva wake.

Mimi siamini kama washambuliaji wale hawakuwa na shabaha, bali naamini kwamba katika tukio lile washambuliaji waliajiriwa na Ole Sendeka ili kurusha risasi hapa na pale jirani ya gari yake na yeye apate kiki ya kisiasa kama kiongozi Mmasai anayetetea maslahi ya Wamasai wa Loliondo anayetishiwa kuuawa ili apate umaarufu na asipate shida katika kampeni za Uchaguzi Mkuu ujao 2025.

Na kwa sababu anawafahamu watu aliowaajiri wamrushie risasi lakini wasimdhuru ndiyo maana anadiriki kusema kwamba serikali ya CCM inayotuhumiwa kumiliki watu wasiojulikana haihusiki na tukio la kushambuliwa kwake kwa risasi siku ya Machi 29, 2024.

DCP Misime ameahidi kwamba timu ya wataalamu wa matukio ya matumizi ya silaha za moto iliyotumwa Manyara wilayani Kiteto ikimaliza uchunguzi wake taarifa itatolewa lakini mimi nafahamu taarifa hiyo haitatolewa hadi tunakwenda kwenye Uchaguzi mkuu 2025. Kidumu Chama Cha Mapinduzi.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

BiasharaHabari za Siasa

Bunge laitaka Serikali kudhibiti ufisadi miradi ya mkakati

Spread the loveKAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, imeitaka Serikali kuimarisha...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Wizara ya Uchukuzi yaomba kuongezewa bajeti na Bunge

Spread the loveWIZARA ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti yake kwa mwaka...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Serikali kutafuta mwekezaji mwingine Bandari ya Dar es Salaam

Spread the loveSERIKALI inaendelea kutafuta mwekezaji mwingine atakayeendesha gati namba nane hadi...

error: Content is protected !!