Tuesday , 30 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Makonda kung’oka tena
Habari za SiasaTangulizi

Makonda kung’oka tena

Paul Makonda
Spread the love

UWEZEKANO wa Paul Makonda, kuendelea na wadhifa wake wa mkuu wa mkoa wa Arusha, ni mdogo mno, Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa kutoka vyanzo vya ndani ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), zinaeleza kuwa kuna uwezekano mdogo wa Makonda kudumu kwenye nafasi yake, kutokana na “matendo na kauli” alizozitoa mkoani Arusha.

“Kitendo cha kufanya maandalizi ya kujipokea, kauli alizozitoa dhidi ya viongozi na watendaji wengine wa serikali, zimewachukiza baadhi ya viongozi waandamizi serikalini na hivyo, kujiweka katika wakati mgumu wa kuendelea na wadhifa huo,” ameeleza kiongozi mmoja serikali kwa sharti la kutotajwa jina.

Aliongeza: “Huyu bwana ni kama sikio la kufa. Mtu mwenye kujitambua hauwezi kusema maneno yale. Kwamba, rais Samia amemtoa mtoto wake wa pekee kwenda Arusha na kwamba haogopi na hana alichojifunza kwa kuondolewa kwenye wadhifa wa Katibu Mwenezi CCM.”

Alisema: “Hii maana yake ni kwamba Makonda amemtumia salamu Rais Samia na kumwambia yuko tayari kuwa mkuu wa mkoa wa siku moja na kwamba hakuna alilojifunza hata baada ya kupokwa uenezi. Huwezi kumtunishia msuli aliyekuteua kisha ukabaki salama.”

Matendo, kauli na hulka ya Makonda ya kukabiliana na viongozi wa serikali, CCM, watumishi wa umma na wengine, ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha kuondolewa katika wadhifa wa katibu mwenezi na kutupwa mkoani Arusha.

Baadhi ya wadadisi wanatafsiri uteuzi wake mkoani Arusha, kuwa ni kitanzi kwa mwanasiasa huyo asiyechagua maneno ya kusema.

Kabla ya kuondolewa CCM, Makonda alijaribu mara kadhaa, lakini bila mafanikio, kumuingiza Rais Samia katika mambo yasiyofaa yaliyotendwa na mtangulizi wake, Rais John Magufuli.

Akizungumza wakati wa kupokea ndege mpya iliyonunuliwa na serikali, wiki mbili zilizopita, Makonda alidai kuwa Rais Samia na Magufuli,  ni ‘pacha,’ na kwamba yeyote anayetaka kuwatenganisha ni mnafiki.

Kauli hiyo ambayo alikuwa akiirejea mara kwa mara inatajwa kuwa miongoni mwa yaliyochangia kuondolewa kwake, kwa kuwa utawala wa sasa ulishachora ramani na kuweka njia ya kufukia makosa yaliyotendwa na utawala wa Magufuli.

Baada ya Rais Samia, kuingia madarakani, tarehe 19 Machi 2021, alianza kuhubiri siasa za maridhiano, kujenga nchi, kuvumiliana na kufanya mageuzi, mambo ambayo Magufuli hakuyapa kipaumbele.

Katika miaka mitano ya utawala wake, Magufuli alilaumiwa kuminya haki za binadamu, wakiwamo washindani wake wa kisiasa, kupora mali na fedha za watu na kukandamiza demokrasia.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, licha ya watu kadhaa kumkanya juu ya namna anavyoendesha siasa zake na minendo yake, Makonda haonekani kubadilika.

Akishirikiana na baadhi ya marafiki zake, Jumatatu iliyopita, alitumia mamilioni ya shilingi, kulipa waandishi wa habari na wapambe wake wengine, ili kuandaa mapokezi yake.

Wachambuzi wanasema, lengo la kufanya hayo, ni kutaka kuamianisha umma kuwa yeye ni kiongozi imara, kuliko waliomtangulia.

Akiapisha viongozi aliowateua, tarehe 4 Aprili, Rais Samia Suluhu Hassan, alimmwagia sifa Makonda huku akieleza kuwa ana imani naye na atatimiza matamanio yake mkoani humo.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa na utawala wa sheria wanasema, mtu akifanya vizuri huongezewa majukumu. Haijawahi kutokea mtu anayefanya vizuri, kupunguziwa makujumu.

Kitendo cha kumuondoa Makonda kwenye wadhifa wake wa awali, ni njia ya kuonesha kuwa kuna mambo hayakuwa sawa.

Akipokelewa kwa mbwembwe jijini Arusha, Makonda alijinasibu kuwa Rais Samia kawapendelea wananchi wa mkoa huo kwa kumtoa yeye ambaye ni mwanaye wa pekee, kumpeleka mkoani mwao.

Katika mapokezi hayo, kuliandaliwa magari zaidi ya 20 mengi yao yakiwa yanayobeba watalii, huku waandishi wa habari wasiopungua 25 wakiripoti shughuli hiyo.

Makabidhiano ya ofisi kati yake na John Mongella, aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, yalitumia takriban saa moja na dakika 30. Yalirushwa moja kwa moja na televisheni za mtandaoni kwa malipo ambayo hayakuweza kufahamika kiasi chake mara moja.

Mmoja wa wakazi wa Arusha aliyejitambulisha kwa jina la Zubeda Ismail, aliliambia MwanaHALISI kuwa mapokezi ya Makonda, yametumia fedha nyingi na ambazo hazifahamiki chanzo chake.

Mkazi huyo wa Njiro alisema: “Huu ni ufisadi. Fedha hizi zingeweza kuboresha huduma za kijamii, ikiwamo kusaidia walioathirika na mafuriko. Kama fedha zimetolewa na watu binafsi, tujiulize watanufaikaje? Atawezaje kuzirudisha?”

Ameongeza: “Ninaona hapa kuwa aliyemteua atakuwa na mzigo mkubwa wa kumlinda na kumtetea atakapokuwa akifanya ndivyo sivyo. Kama alimuona mzuri na alikichangamsha chama kwanini amemuondoa wakati huu wanapoelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa na uchaguzi mkuu?”

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Makonda alionya viongozi na watendaji wengine wa serikali, kuwa hatakuwa na huruma nao.

Alisema, amechelewa kufika Arusha kwa kuwa kuna mambo mengi ya kufanya, hivyo wajiandae kuwajibika kwa kuwa hatakuwa kama mtangulizi wake, aliyekuwa akiangalia maumbile ya watu, kabla ya kuchukua hatua.

Akampa Kamishna wa Ardhi mkoani humo, miezi mitatu, kumaliza migogoro ya ardhi, vinginevyo achague kuacha kazi au kuhamishwa.

“…sitaki kusikia migogoro ya ardhi hapa. Una miezi mitatu ya kuchagua kufanya kazi au uombe uhamisho. Mimi hapa tayari nina viwanja, sitaki mjipendekeze kwa kunitafutia viwanja,” alieleza.

Baadhi ya watu wametafsiri kauli hiyo kuwa yaweza kumuingiza kwenye mgogoro na watendaji wengine wasiokuwa kwenye mamlaka yake.

Hulka ya Makonda kuingilia utendaji wa taasisi nyingine, ulimgharimu alipokuwa mkuu wa wilaya ya Kinondoni, kufuatia kutaka kuwafukuza kazi baadhi ya watumishi wa idara ya ardhi na ujenzi, akiwatuhumu kwa rushwa.

Hata hivyo, Baraza la madiwani la Manispaa ya Kinondoni, liligoma kutekeleza matakwa yake, kwa maelezo kuwa mchakato mzima wa kinidhamu, uligubikwa na ukiukwaji wa taratibu na uonevu.

“Huyu kijana afundishwe vizuri uongozi. Vinginevyo huko tunakoelekea tutashuhudia mambo ya ajabu na hatari kama ilivyokuwa hapa Dar,” ameeleza mbunge mmoja wa Dar es Salaam, kwa sharti la kutotajwa jina lake.

Chanzo kimoja cha gazeti hili, kimedokeza kuwa miongoni mwa vitu ambavyo Makonda alitamba navyo kuvifanya mkoani Arusha, ni kushughulika na upinzani, hususani Godbless Lema, aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini (Chadema).

Akizungumza kwenye Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliyoketi wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wakati alipopewa nafasi ya kuaga, Makonda alisema kwa muda mfupi aliokaa kwenye nafasi ya mwenezi, ametembea nchi mzima na sasa kazi anayokwenda kuifanya Arusha, ni kushugulika na Lema.

Jijini Arusha, Lema anayejitambulisha kama ‘nabii’ na nguli wa siasa za jiji hilo linaloongozwa na mbunge wa CCM, Mrisho Gambo aliyeingia madarakani mwaka 2020.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Mavunde aomba bilioni 231.9 bajeti wizara ya madini

Spread the loveWAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde leo Jumanne amewasilisha hotuba ya...

Habari za SiasaTangulizi

Lissu amjibu Fatma Karume kuhusu Rais Samia

Spread the love  MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)...

Habari za SiasaTangulizi

Dk. Slaa: Watanzania iungeni mkono Chadema uchaguzi 2025

Spread the loveMWANASIASA mkongwe nchini Tanzania, Dk. Wilbroad Slaa, amewataka watanzania wakiunge...

Habari za SiasaTangulizi

Samia ataja miradi ambayo Tanzania inashirikiana na IDA

Spread the loveRais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan leo Jumatatu amehutubia...

error: Content is protected !!