RAIS wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa leo ameondoka kutoka visiwa vya Maldives alikowasili jana baada ya kuikimbia nchi yake kufuatia shinikizo la maandamano ya umma yanayomtaka kujiuzulu kutokana na mzozo mkubwa wa kiuchumi. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Afisa mmoja wa serikali ya Maldives aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema, Rajapaksa aliondoka katika visiwa hivyo kwa kutumia ndege ya shirika la Saudi Arabia inayoelekea Singapore, ambako anatarajiwa kuishi kwa muda.
Rajapaksa (73) na mkewe waliikimbia Sri Lanka jana Jumatano wakitumia ndege ya jeshi wakati waandamanaji wakiendelea kuyamakata majengo ya serikali kumlazimisha kujiuzulu wakimtwika dhima ya kuwa chanzo cha hali mbaya ya kiuchumi inayoikabili nchi hiyo.
Hata hivyo, inaarifiwa hadi sasa kiongozi huyo hajawasilisha barua yake ya kujiuzulu licha ya kutoa ahadi ya kufanya hivyo jana na badala yake amemteua waziri mkuu, Ranil Wickremesinghe kuwa rais wa muda.
Uteuzi wake, ulitangazwa na Spika wa Bunge, chini ya Kifungu cha 37.1 cha katiba ya Sri Lanka.
Kwa mujibu wa Katiba ya Sri Lanka, nafasi ya rais ikiwa wazi, waziri mkuu ataapishwa na kukaimu kwa muda mpaka atakapochaguliwa rais kutoka miongoni mwa wabunge.
Uchaguzi huo unapaswa kufanyika ndani ya siku 30 baada ya Rais kujiuzulu. Spika wa Bunge alisema, uchaguzi unaweza kufanyika 20 Julai 2022.
Mapema jana, afisa wa uhamiaji alisema rais na mke wake, pamoja na walinzi wawili, waliondoka nchini humo kwa ndege ya jeshi, ambayo ilitua katika mji mkuu wa Maldives, Male.
Utorokaji huo wa mapema wa rais unafuatia maandamano makubwa katika taifa hilo, ambalo limekuwa likikabiliana na mzozo mbaya wa kiuchumi, yaliyofikia kilele kwa uvamizi wa makaazi rasmi ya rais na waziri mkuu siku ya Jumamosi
Leave a comment