August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mrema ataka Tume Huru, “Katiba mpya sio mwarobaini”

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Chama cha (TLP), Augustine Mrema amesema ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki ni lazima kuwepo tume huru ya uchaguzi, huku akisisitiza kuwa Katiba mpya sio mwarobaini wa matatizo nchini. Anaripoti Seleman Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Kauli hiyo ya Mrema kutaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi inaungana na wadau wengine kama Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, CAG mstaafu Profesa Mussa Assad, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, Chama cha ACT-Wazalendo, asasi za kiraia na wengine ambao wamefika mbele ya Kikosi Kazi hicho chenye ajenda tisa.

Katika Kikosi Kazi hicho zipo ajenda za Tume Huru, Katiba mpya, demokrasia na nyingine ambazo zote zinalenga kuboresha mazingira ya ufanyaji siasa na demokrasia nchini.

Akizungumza baada ya kutoa maoni na mapendekezo yake mbele ya Kikosi Kazi cha Rais cha Kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, Mrema amesema suala la Tume Huru halipingi kwa sasa kwani ndio hitaji la Watanzania.

Amesema kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kuhusu tume huru ya uchaguzi, hivyo ni vema kikosi kazi hiki kikatumika kuwavusha hapo.

“Ni muhimu kuwepo na tume huru ya uchaguzi, ili tuweze kuandaa chaguzi huru kuanzia sasa. Lakini pia chaguzi za Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji,”alisema.

Mwenyekiti huyo amesema iwapo tume huru itapatikana na wananchi wakachagua wawakilishi wao kwa uhuru na haki wataona kama kuna umuhimu wa kwenda kwenye Katiba mpya.

Mrema amesema suala la Katiba sio jipya na kwamba “tunatakiwa kuendelea pale ambapo mchakato iliishia.”

“Suala la Katiba kwangu mimi naona ni jambo la baadae na nimeshauri kama mchakato wake unafanyika tuanzie pale ambao tuliishia, tuendelee na sio kuanza moja kwa sababu ilishapendekezwa,” mesema.

Amesema Katiba mpya sio mwarobaini wa kila kitu na kwamba wanasiasa na viongozi wasiaminishe wananchi kwamba Katiba mpya ni ufumbuzi wa matatizo yote.

Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Vunjo amesema mfano wa kuwa Katiba sio mwarobaini wa kila kitu ni nchi ya Kenya ambayo haijatulia pamoja na kuwa na Katiba mpya.

Amesema pia nchi ya Marekani ambayo inasifiwa kwa demokrasia bado wakati wa uchaguzi wanalalamika kuibiana kura.

“Nadhani mwaka jana mmeona Marekani Donald Trump akilalamika kuwa ameibiwa kura, hivyo Katiba sio mwarobaini wa kila kitu,”amesema.

Mwenyekiti huyo ametoa raia kwa Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa lile ambalo anaanzisha na sio kumkatisha tamaa.

“Tuache kusemasema hovyo kwani Marais kama Samia hawapatikani hovyo, tumuunge mkono aweze kupeleka nchi kwenye neema.

Mrema amefika mbele ya Kikosi Kazi kwa kuletwa na mkewe ambaye alikuwa anamuendesha na gari aina ya Harrier.

error: Content is protected !!