Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa SMZ yasalimu amri, yashusha viwango vya malipo Bandari ya Malindi
Habari za SiasaTangulizi

SMZ yasalimu amri, yashusha viwango vya malipo Bandari ya Malindi

Bandari Kuu ya Malindi Zanzibar
Spread the love

 

SERIKALI imerudisha viwango vya malipo ya uingizaji mizigo kupitia Bandari Kuu ya Malindi, mjini hapa, baada ya “kishindo kikubwa” cha malalamiko ya wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kuanzia juzi Septemba 18. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Mbele ya waandishi wa habari leo, walikuwepo Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Joseph Meza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Nahat Mohamed waliotoa tamko la kubadilisha utaratibu mpya wa malipo ya gharama za utoaji na upakiaji mizigo kwenye Bandari hii ambayo inahudumia kiasi cha tani 45,000 kwa mwezi.

Wakuu hao wa Shirika la Bandari wamesema viwango vilivyoanza kutumika siku ya kwanza ya kuingia kwa mwekezaji wa kushughulikia eneo la mizigo kwenye Bandari ya Malindi si vipya kwani vilipitishwa kisheria mwaka 2018 lakini iliamuliwa kutovitumia na “kuendelea na viwango vya mazoea.”

Mkurugenzi Nahat amesema kilichotokea ni mwekezaji aliyeingia mkataba na Serikali kuanza kazi kwa kufuata nyaraka na “sio mazoea” yaliyosababisha huduma kutolewa kwa viwango vya kabla ya marekebisho ya mwaka 2018.

“Viwango si vipya. Kwa kweli viliwekwa kwa mujibu wa kanuni ya uendeshaji wa Bandari, lakini wenzetu walipoingia wao walifuata nyaraka na sio mazoea yetu,” alisema na kuongeza:

“Sasa Serikali imeamua kuendelea na viwango vyetu mpaka hapo mbele tutakapofanya tathmini.” Hata hivyo si yeye Nahat wala Mwenyekiti wa Bodi aliyethubutu kutaja kwa uhakika ni lini hiyo tathmini itafanywa.

Wakati uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar “ukijenga ukuta” kwa kusalimu amri, malalamiko ya wadau wakiwemo mawakala wa uingizaji na utoaji mizigo yameibuka kwa kasi huku eneo la makontena nao wakidai hawajashirkishwa kwa lolote katika mabadiliko ya viwango vya tozo bandarini.

Juzi wafanyabiashara wa eneo la majahazi, walilalamika kuanza usumbufu kwa kutozwa viwango vya juu kwa zaidi ya asilimia 200 hatua iliyozorotesha utoaji wa mizigo hususan bidhaa za chakula kutoka Tanzania Bara.

Lakini wakati serikali ikijirudi, Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali ifute mkataba wa kuingiza mwekezaji kwa kuwa ushirikiano huo haukufanywa kisheria.

Kupitia kwa Katibu wake wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma, Salim Bimani, chama hicho kimesema kinashuku harufu ya rushwa kutawala usiri wa namna mkataba huo na kampuni ya African Global Logistics (AGL) ulivyofikiwa huku ikiaminika wadau hawakushirikishwa.

“Tunaona ni wazi kwamba hofu zilizokuwa zimetanda miongoni mwa watu juu ya nia ovu ya ukodishwaji wa Bandari sasa zinathibitika kuwa na uhalisia. Ukodishwaji wa Bandari ya Malindi kwa kampuni ya AGL kutoka Ufaransa haukuwa na nia njema bali kitendo cha kifisadi cha watu wachache kujilimbikizia mali kupitia mgongo wa Wazanzibari walio wanyonge na kufisidi mali zao,” imesema taarifa yake.

ACT Wazalendo imetaka yatolewe maelezo ya: 1. Ni kwanini ubinafsishaji ulifanywa kwa siri. 2. Ni lini tenda ilitangazwa, kampuni zipi ziliomba, utaratibu na vigezo vipi vilitumika mpaka kufikia AGL kukabidhiwa uendeshaji.

Zaidi chama hicho kinahoji mwekezaji atawekeza nini wakati Serikali ya Zanzibar mwaka juzi ilitumia Dola milioni 6 kugharamia ufungaji mifumo ya kidijitali ya udhibiti na ulipaji wa tozo, huku ikitumia Sh. 16.5 Bilioni kununua zana na mitambo kwa ajili ya upakuaji na upakiaji mizigo.

“Tunalichukulia tendo hili la kupandisha gharama za uendeshaji Bandari ya Malindi ni tendo baya, ovu na ambalo linakwenda kuongeza gharama za maisha na kuwaongezea umaskini wananchi,” alisema Bimani.

Serikali imesema imeingiza Wafaransa AGL kwa mkataba wa miaka mitano kushughulikia usimamizi wa huduma kwa uingizaji na utoaji wa mizigo na litakusanya mapato ambayo asilimia 30 ndio mgao wake na 70 inakuwa ya AGL na kutarajiwa kuongezeka ufanisi, nidhamu na mapato.

Imeelezwa kuwa AGL katika utekelezaji wa mkataba, imesajili hapa nchini kampuni ya Zanzibar Multipurpose Terminal kushirikiana nayo, kampuni ambayo ACT Wazalendo inalalamika kuwapo shaka kuwa inamilikiwa na wakubwa.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Wanaotaka kujifunza ZEC kwao kukoje?

Spread the loveMKURUGENZI wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Biteko, Nape wanadanganya?

Spread the loveKWA mila na desturi zetu za Kiafrika mkubwa huwa hakosei,...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miamka 60 ya Muungano: Tunakwama wapi?

Spread the loveRAIS wa Jamhuri, Samia Suluhu Hasssan, Ijumaa iliyopita, aliongoza mamilioni...

ElimuHabari za Siasa

Serikali kuongeza wanufaika mikopo ya elimu ya juu

Spread the loveSERIKALI imesema itaongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu...

error: Content is protected !!