Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Miamka 60 ya Muungano: Tunakwama wapi?
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miamka 60 ya Muungano: Tunakwama wapi?

Spread the love

RAIS wa Jamhuri, Samia Suluhu Hasssan, Ijumaa iliyopita, aliongoza mamilioni ya wananchi kuadhimisha miaka 60 ya kuundwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anaandika Saed Kubenea… (endelea).

Sherehe za maadhimisho, zilifanyika uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam. Zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwamo marais wa mataifa jirani.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa 26 Aprili 1964, baada ya mataifa mawili huru – Jamhuri yaTanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar – kukubaliana kuanzisha dola mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mkataba wa Muungano, ulithibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi Zanzibar. Viongozi wa nchi hizo mbili, walikutana katika ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam, tarehe 27 Aprili 1964, kubadilishana Hati za Muungano.

Jina la kwanza la Muungano huu, lilikuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Lilianza kutumika tarehe 28 Oktoba 1964.

Rais Samia Suluhu Hassan

Aidha, Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ilibadilishwa jina kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 28 Oktoba 1964, kupitia Sheria Na. 61 ya mwaka 964.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Samia alisema, kuna kila sababu ya kujivunia muungano huu. Alisema, “…nchi hii, imetokana na maamuzi yetu wenyewe….”

Aliongeza, “…ninawashukuru kwa dhati waasisi wa Muungano huu, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, pamoja na viongozi waliofuata baada ya kutuleta pamoja na kujenga taifa huru, madhubuti na lenye matumaini.”

Alisema, zawadi pekee anayoweza kuwapa wananchi, ni kuendeleea kudumisha Muungano huu na kuenzi maono ya waasisi wake.

Swali ambalo wananchi wanajiuliza, ni kwamba ni kweli kuwa Muungano huu, bado ni madhubuti kama ambavyo rais ameeleza?

Ni kweli kwamba Jamhuri ya Muungano, ni taifa moja, kama rais anavyosema? Je, kwa nini serikali na chama kilicho madarakani, wameshindwa kutatua matatizo ya Muungano? Kuna nini? Tujadili:

Kwanza, mkataba wa Muungano uliotiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, tarehe 26 Aprili 1964, siyo unaotumika sasa.

Mgongano huu umeanzia kwenye Katiba ya Zanzibar, kwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Kwamba, mkataba unazitambua Katiba ya Jamhuri ya Muungano (1977), Katiba ya Tanganyika (1962) Amri za Katiba (Decrees) za Zanzibar na Katiba ya Zanzibar (1984), kuwa msingi wa “Hati ya Makubaliano ya Muungano.

Katiba ya Muungano, inaitambua Zanzibar, kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini Zanzibar inakataa utambuzi huo.

Ibara ya kwanza ya Katiba hiyo inasema, “Tanzania ni nchi moja na ni Jamhuri ya Muungano.”

Ibara ya 2 (1) ya Katiba ya Muungano inaongeza: “Eneo la Jamhuri ya Muungano, ni eneo lote la Tanzania Bara na eneo lote la Tanzania Zanzibar, na ni pamoja na sehemu yake ya bahari ambayo Tanzania inapakana nayo.”

Bali Ibara ya Kwanza ya Katiba ya Zanzibar, inaeleza kuwa “Zanzibar ni Nchi ambayo eneo la mipaka yake, ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na Visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Hayati Rais John Magufuli

Nayo Ibara ya 2 ya Katiba hiyo inasema, “Zanzibar ni miongoni mwa Nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Maneno “Zanzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” yanathibitisha kuwa Zanzibar bado ni Nchi kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano. Ni kwa sababu, Katiba ya Zanzibar, haisemi zilizounda. Inasisitiza “zinazounda.”

Ibara ya 2A ya Katiba ya Zanzibar, inakwenda mbali zaidi. Inasema, “Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali, Rais aweza kuigawa Zanzibar katika Mikoa, Wilaya na maeneo mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.”

Maneno haya, hayamo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Badala yake, mamlaka ya kugawa nchi katika wilaya na mikoa, yamebakishwa mikononi mwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haya yameelezwa vizuri katika Ibara ya 2 ya Katiba hiyo, kupitia kinachoitwa, “utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.”

Kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano aweza kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge.

Ibara ya 26 (1) ya Katiba ya Zanzibar, inamtaja Rais wa visiwani hivyo, “kuwa Mkuu wa Nchi ya Zanzibar.”

Rais wa Zanzibar, “atakuwa Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Idara Maalum ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na atakuwa na uwezo wa kufanya chochote kile anachohisi, kwa maslahi ya Taifa, kinafaa.” Rejea Ibara ya 123 ya Katiba ya Zanzibar.

Hii maana yake ni kwamba Rais wa Jamhuri, siyo Amiri Jeshi Mkuu wa Zanzibar. Amiri Jeshi Mkuu, ni rais wa Zanzibar.

Ibara ya 6 (1) ya Katiba ya Zanzibar, inatambua kuwapo kwa raia wa Zanzibar. Inasema, kutakuwa na Mzanzibari ambaye upatikanaji wake, upoteaji wake na urudishwaji wake, atakuwa kama alivyoainishwa katika Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inatambua kuwapo kwa raia wa Tanzania na kwamba suala la uraia, ni miongoni mwa mambo yaliyokubaliwa katika mkataba wa Muungano.

Suala la uraia, lilitajwa katika mambo 11 ya Muungano, yaliyotajwa kwenye Katiba ya muda ya Jamhuri ya Muungano (1965), kwamba yatakuwa chini ya usimamizi wa Serikali ya Muungano.

Mengine yaliyokubaliwa, ni mambo ya nje, ulinzi, polisi, mambo yanayohusu hali ya hatari, uhamiaji, mikopo na biashara ya nchi za nje na utumishi katika serikali ya Muungano.

Ibara ya 6 (2) ya Katiba ya Zanzibar, inasisitiza kuwa kila Mzanzibari, kwa misingi ya Katiba hii, ataweza kufaidi haki na fursa zote anazostahiki Mzanzibari.

Atapaswa kutekeleza wajibu, majukumu na dhamana za Mzanzibari kama ilivyo kwenye Katiba hii au kwenye Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.

Katiba ya Zanzibar, haimtaji kokote raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inasisitiza kuwapo Mzanzibari, haki zake na wajibu wake kwa taifa lake.

Katika mazingira haya, hakuna anayeweza kusema kuwa Tanzania ni nchi moja na akaaminika. Hakuna anayeweza kusema, tunaye mkuu wa nchi mmoja. Hakuna na hatakuwapo.

Kinachonekana hapa ni kwamba kumekuwapo na nchi mbili – Zanzibar na Tanganyika, tangu mwaka 1964; moja ya nchi hizo, bado ina utaifa wake na nyingine inatumia koti la Muungano.

Pili, muundo wa sasa wa Muungano, unazitambua Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, kama vyombo vya utendaji.

Serikali ya Muungano inashughulikia mambo yote ya Muungano na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara.

Nayo Serikali ya Zanzibar, inashughulikia mambo yote yasiyo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar.

Ibara ya 52 (1) ya Katiba ya Muungano inasema, Waziri Mkuu atakuwa na madaraka ya juu ya udhibiti, usimamiaji,utekelezaji wa siku hadi siku wa kazi na shughuli za serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Nayo Ibara ya 52 (3) inampa Waziri Mkuu madaraka ya kutekeleza au kusababisha kutekelezwa kwa jambo lolote ambalo rais ataagiza litekelezwe.

Lakini waziri mkuu anayetajwa na Katiba ya Muungano na ambaye ndiye mkuu wa shughuli za serikali ya Muungano bungeni, hana mamlaka Zanzibar. Hawezi kuagiza utekelezaji wa lolote.

Waziri mkuu ambaye anaweza kuwajibishwa na Bunge la Muungano, linalobeba hadi wabunge kutoka Zanzibar, wakiwamo wanaotoka Baraza la Wawakilishi (BLW), kwa mambo yaliyoamriwa au kutekelezwa na serikali ya Muungano, hana majukumu yoyote Visiwani.

Hivyo basi, hakuna ubishi kuwa muundo wa sasa wa Muungano, pamoja na Katiba zote mbili – Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano –  vimeshindwa kuimarisha muungano huu.

Badala yake, muundo huu wa muungano wa serikali mbili, unaong’ng’anizwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa maslahi yao binafsi, umeongeza jeraha badala ya tiba.

Kwa mfano, kupitia muungano huu, Zanzibar imekuwa ikidai kwa miaka mingi, kudhoofishwa kiuchumi na Tanganyika.

Serikali ya Zanzibar, hairuhusiwi kujiunga na mashirika ya kimataifa; kukopa ama kufunga mikataba ya ushirikiano, bila idhini ya Ikulu ya Magogoni.

Aidha, baadhi ya wananchi Visiwani, wakiwamo viongozi wakuu wa serikali na chama kilichoko Ikulu -CCM, wamekuwa wakituhumu serikali ya Muungano, kukwamisha kuundwa kwa Kamati ya fedha ya pamoja, kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa Muungano.

Wanadai serikali ya Muungano, imeongeza baadhi ya mambo na imewalaghai Wazanzibari katika baadhi ya maeneo.

Kwamba, Zanzibar ililazimishwa kujiondoka kutoka Jumuiya ya Kiislamu (OIC), ili kuruhusu Jamhuri ya Muungano kujiunga na jumuiya hiyo, na hivyo Zanzibar ingenufaika kupitia mlango wa Muungano. Lakini sasa ni takribani miaka 22 tangu Zanzibar kujiondoa, lakini serikali ya Muungano, haijatekeleza ahadi yake na hakuna dalili kama itatekeleza.

Benjamin Mkapa

Njia pekee inayoweza kutuondoa katika mkwamo huu, ni kuwapo muundo wa serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano – kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Francis Nyalali, Tume ya Jaji Robert Kisenga, Tume ya Jaji Joseph Warioba na kama ambavyo wananchi waliowengi wanavyotaka.

Nje ya hapo, hakuna namna ambayo Muungano huu unaweza kuishi bila manung’uniko na kudumu. Itawalazimu wanaong’ang’aniza muudo wa sasa, kujiandaa kushuhudia Muungano ukivunjika. Yawezekana ikawa sasa au baada ya wao kuondoka ulimwenguni.

Ni vigumu kuwa na wakuu wa nchi wawili, mmoja yuko Zanzibar na mwingine yuko Dodoma, kisha mkabaki salama. Tunayo fursa ya kurekebisha kasoro hizo sasa.

Hii ni kwa sababu, tumebahatika kuwa na rais anayetoka Zanzibar, hivyo kuwa rahisi kushughulikia matatizo ya Visiwani kwa kusaidia Tanganyika kuwa serikali, hata kama serikali hiyo, haitakuwa na mamlaka makubwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!