SERIKALI imesema itaongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu, wenye sifa na uhitaji, kutoka 223,201 waliopata kwenye mwaka wa fedha wa 2023/24, hadi kufikia 252,243 watakaopewa 2024/25. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo, leo Jumanne bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo hiyo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB).
“Wizara itaendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Sh. 198 bilioni kutoka sekta ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi. Aidha, itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi,” amesema Prof. Mkenda.
Kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu kwa 2024/25, Prof. Mkenda amesema wizara yake imepanga kutumia Sh. 1.96 trilioni, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na bajeti ya Sh. 1.67 trilioni, iliyopitishwa na Bunge 2023/24.
Prof. Mkenda amesema, Sh. 1.32 trilioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na Sh. 637 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kaiwada ya wizara.
Waziri huyo wa elimu ametaja vipaumbele vya wizara yake kwa 2024/25, ikiwemo kuboresha elimu ya msingi, sekondari, vyuo vikuu na vya mafunzo ya ufundi stadi.
Prof. Mkenda amesema katika bajeti hiyo wizara yake itaongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya ufundi na ufundi stadi, kwa kuwezesha ujenzi wa shule mpya 100 za sekondari za ufundi, ambapo 26 zitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2025. Pia, itaendelea na ujenzi wa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi 65.
“Wizara itaanzisha mafunzo ya ualimu katika vyuo vitatu vya VETA, Moshi, Dar es Salaam na Kagera, kwa lengo la kuongeza idadi ya walimu wenye sifa na ujuzi wa kufundisha vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi,” amesema Prof. Mkenda.
Katika hatua nyingine, Prof. Mkenda amesema mikopo ya elimu itatolewa kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipaumbele na zenye uhaba wa watalaamu nchini ikiwamo fani za sayansi na ufundi.
Leave a comment