Saturday , 27 April 2024
Home Kitengo Maisha Afya Serikali yatoa taadhari ya ugonjwa wa manjano
Afya

Serikali yatoa taadhari ya ugonjwa wa manjano

Ummy Mwalimu
Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania imetoa taadhari kwa kwa wananchi dhidi ya ugonjwa wa homa ya manjano ambao umeonekana kutokea katika nchi ya jirani ya Kenya.

Pamoja na tahadhari hiyo, pia imeweka utaratibu wa kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini na kutoka nje ya nchi wanapatia chanjo ya kinga dhidi ya homa ya manjano. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo tarehe 9 Machi, 2022 Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wizara ina utaratibu wa kufuatilia taarifa za magonjwa ya milipuko yakiwemo yale yanayozuilika kwa chanjo kama Surua, Rubella, Polio na Homa ya Manjano ili kudhibiti magonjwa hayo hapa nchini.

Amesema tarehe 3 Machi, 2022 Wizara ya Afya ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyopo hapa nchini, ikielezea kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Kenya katika Kaunti ya Isiolo umbali wa takribani Kilomita 285 (Kaskazini mwa Nairobi).

Ummy amesema taarifa hiyo ilieleza kuwa, mgonjwa wa kwanza mwenye dalili za ugonjwa huo alipatikana tarehe 12 Januari 2022 na hadi kufikia tarehe 3 Machi 2022, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 15 na vifo vitatu vilivyotokana na ugonjwa huu.

Aidha, kati ya sampuli sita zilizopimwa katika maabara ya Kenya (KEMRI), sampuli tatu zilithibitika kuwa va virusi vya homa ya manjano kwa kutumia vipimo vya serology na PCR.

Vilevile, kumekuwa na tetesi za kuwa na wagonjwa wenye dalili za homa ya manjano katika nchi za Uganda, Sudan ya Kusini na Chad.

Waziri Ummy amesema Tanzania taarifa za kipindi cha miezi mitatu iliyopita katika mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa yaliyopewa kipaumbele wa (IDSR) zinaonesha kuwa hapakuwepo na taarifa zinazoashiria kuwepo kwa ugonjwa wa Homa ya Manjano.

Vile vile katika kipindi hiki, mfumo wa taarifa wa ufuatiliaji wa tetesi za magonjwa haujaashiria kuwepo kwa dalili za ugonjwa huo hapa nchini.

“Hata hivyo, ninatoa tahadhari kwa wananchi ili kuchukua hatua na kuhakikisha ugonjwa huu hauingii nchini kwetu.

“Ugonjwa wa homa ya manjano husababishwa na virusi ambavyo huenezwa na mbu aina ya Aedes, kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na vilevile kati ya mtu na mtu.

“Watu wanaofanya kazi kwenye misitu huambukizwa kwa kung’atwa na mbu ambao hupata vimelea vya ugonjwa huo kutoka kwa wanyama wa porini kama Nyani nk.

Vilevile ugonjwa huo huambukizwa kati ya mtu na mtu pindi mtu mwenye virusi hivyo anapoumwa na mbu na hatimaye kueneza kwa mtu mwingine.

“Dalili za ugonjwa wa homa ya manjano ni pamoja na homa, kuumwa na kichwa, maumivu ya misuli pamoja na mgongo, mwili kutetemeka, kupoteza hamu ya kula, kusikia kichefuchefu na kutapika, mwili kuwa na manjano, kutokwa na damu sehemu za wazi kama mdomoni, puani, machoni na tumboni na wakati mwingine damu huonekana kwenye matapishi na kinyesi na ugonjwa unapokuwa mkali figo hushindwa kufanya kazi.

“Kipindi cha kuonekana kwa dalili za ugonjwa huu ni kati ya siku 3 hadi 6 baada ya kuambukizwa.

“Ugonjwa wa Homa ya Manjano hauna tiba mahsusi bali mgonjwa anayezidiwa uhitaji huduma ya karibu, ambapo mgonjwa anatibiwa kutokana na dalili zinazojitokeza,” amesema.

Amesema mara nyingi matibabu yanahusisha utoaji wa dawa za kushusha homa na kupunguza maumivu au kuongezewa maji mwilini kwa kunywa au kwa kuwekewa dripu.

Amesema baada ya kupata taarifa za ugonjwa huo katika nchi ya Kenya, Serikali kupitia Wizara Afya inaendelea kuchukua hatua zote stahiki ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa watu wenye dalili za ugonjwa katika vituo vya afya vya bandari, viwanja vya ndege na mipakani.

Kwa wasafiri watokao nje ya nchi na kuhakikisha kuwa wasafiri watokao nchi zenye hatari ya ugonjwa huo wanakuwa na uthibitisho wa chanjo ya homa ya manjano kabla ya kuruhusiwa kuingia nchini.

Aidha, amesema wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu wasafiri wote wanaoingia nchini hususani kutoka nchi zilizo katika hatari ya maambukizi ya homa ya manjano.

“Kuhakikisha kuwa chanjo za kutosha za ugonjwa wa Homa ya manjano zinakuwepo hapa nchini.

“Kusimamia na kuhimiza usafi wa mazingira ili kudhibiti mazalia ya mbu. Kuendelea kutoa elimu ya Afya kwa wananchi kuhusu ugonjwa huu” ameeleza Ummy.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Afya

Mloganzila yajipanga kupandikizaji wa ini

Spread the love  HOSPITALI ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imesema kutokana na uwekezaji uliofanywa...

AfyaHabari za Siasa

Serikali yasaka watumishi afya ngazi ya jamii 8,900

Spread the loveSERIKALI imeanza utekelezaji wa mpango jumuishi wa wahudumu wa afya...

AfyaHabari za SiasaTangulizi

Bima ya afya kwa wote kuanza Aprili, wajane kicheko

Spread the loveSHERIA ya Bima ya Afya kwa Wote, inatarajiwa kuanza kutumika...

AfyaHabari Mchanganyiko

Marekani kuipa Tanzania bilioni 980 kudhibiti VVU, UKIMWI

Spread the loveSERIKALI ya Tanzania inatarajiwa kupewa msaada wa fedha kiasi cha...

error: Content is protected !!