May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

69 mbaroni Dar kwa tuhuma za ujangili, wizi mtandao

Kamanda Polisi wa Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo

Spread the love

 

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewakamata watu 69 wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kukutwa na nyara za Serikali na wizi wa mtandao. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumatano, tarehe 9 Machi 2022 na Kamanda wa Jeshi la Polisi wa kanda hiyo, ACP Jumanne Muliro, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Kamanda Muliro amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kupitia operesheni maalumu ya kuzuia na kuwakamata wahalifu, iliyofanyika kuanzia tarehe 25 Februari hadi 9 Machi 2022.

Amesema, Jeshi la Polisi kushirikiana na Kikosi Kazi cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili, limewakamata watuhumiwa watatu, akiwemo Gabriel Mgana na Haffarman Yona, kwa tuhuma za kukamatwa na vipande 25 vya meno ya Tembo.

“Walikamatwa wakiwa na meno ya tembo 25 sawa na tembo 14 waliouawa. Vipande hivyo vyenye uzito wa Kg. 20 vilifichwa ndani ya nyumba ya mmoja wa watuhumiwa hao. Pia gari aina ya Toyota Wiills iliyodaiwa kutumika kusafirisha meno hayo hapa Dar es Salaam, imekamatwa,” amesema Kamanda Muliro.

Wakati huo huo, Kamanda Muliro amesema, Jeshi la polisi limemkamata Khatib Abdala, mkazi wa Banana Kitunda, jijini humo na wenzake watatu, kwa tuhuma za wizi kwa njia ya mtandao kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji hilo.

“Upekuzi wa kina ulifanyika katika nyumba za watuhumiwa hao na walikutwa na jumla ya kadi za simu 46 za kampuni tofauti tofauti, vizibao vinne vya uwakala, simu za mkononi 14 na vitambulisho vitatu vyenye majina yasiyo yao, wanavyotumia katika kazi za kusajili laini hatimaye kuwaibia wateja,” amesema Kamanda Muliro.

Katika matukio mengine, Kamanda Muliro amesema Polisi wamewakamata watu 17, kwa kosa la kupatikana na bhangi kiasi cha masunduku ya chuma mawili, nusu gunia na kete 1,305.

Pia, Kamanda Muliro amesema Polisi imewakamata watu wawili kwa tuhuma za kupatikana na mitambo minne ya kutengenezea pombe ya moshi ‘gongo, lita 780.

error: Content is protected !!