Saturday , 27 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Balozi Katanga atoa maagizo kwa viongozi
Habari Mchanganyiko

Balozi Katanga atoa maagizo kwa viongozi

Spread the love

 

KATIBU Mkuu Kiongozi wa Tanzania, Balozi Hussein Katanga amewataka viongozi wenye nafasi ya kufanya uamuzi wa masuala ya kisera na kiutendaji serikalini, kutumia mabadiliko ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ili kuwezesha kukuza uchumi kidigitali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Aidha, ameitaka wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari kuchukua jukumu la kuendelea kuwa wazazi kwa kukuza sekta ya mawasiliano baina ya Serikali, sekta binafsi na wananchi

Balozi Katanga alisema hayo jana Jumanne, tarehe 8 Machi 2022, visiwani Zanzibar alipofungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi wa Serikali ya Tanzania na Zanzibar kuhusu uchumi wa kidijitali.

Alisema viongozi wenye nafasi ya kufanya uamuzi wa masuala ya kisera na kiutendaji ndani ya Serikali kutumia fursa ya mafunzo hayo kujenga uelewa kuhusu mabadiliko haya ya Tehama “yanaliwezesha taifa letu kukuza uchumi ili kuhakikisha kuwa nchi inanufaika na maendeleo ya Tehama hivyo kujenga uchumi wa kidijitali.”

Kuhusu wizara ya habari, Balozi Katanga aliitaka kuchukua jukumu la kuendelea kuwa wazazi kwa kukuza sekta ya mawasiliano baina ya Serikali, sekta binafsi na wananchi na kubadilika kwa haraka kuendana na maendeleo ya sekta hiyo.

Alisema lengo ni kwenda sambamba na mabadiliko hayo na kwenda na wakati ili kuipeleka nchi yetu kwenye kiwango cha juu cha uchumi ili tufikie uchumi wa kidijitali ikiwemo kufungua fursa mpya.

Pia alise,a mabadiliko hayo yanawezesha kuongeza mapato ya kodi; mifumo ya kiutendaji; upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi; huduma za utalii na kuitangaza nchi kimataifa.

Aidha, kufanikisha ongezeko la huduma za intaneti na upatikanaji wa ajira ili mfumo huu mpya ulete mabadiliko kwenye nchi ikiwa ni pamoja na kuongeza wabobezi wenye ujuzi; kuendeleza na kupanua miundombinu ya kimkakati ya Tehama na anwani za makazi ikiwa ni pamoja na kutafuta masoko.

“Ni imani yangu kuwa mafunzo haya yataliwezesha taifa letu kunufaika na kwenda kasi na ukuaji wa Tehama duniani ikiwa ni pamoja na kuwa na mtandao wenye kasi kubwa; usalama wa mtandao na kupatikana kwa bidhaa na huduma ambapo maendeleo ya Tehama yameondoa mipaka ya upatikanaji na ufikishaji wa huduma kwenye maeneo mbalimbali,” alisema

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema mafunzo hayo yatafanyika kwa makundi mbalimbali ili viongozi wengine waweze kupata mafunzo hayo na kunufaika nayo kwa kuwa viongozi ndio wanaoshika usukani wa kuendesha nchi.

Alisema wakielewa tunaamini wataendesha vema taasisi za Serikali ili kuendana na ukuaji wa uchumi na uchumi wa kidijitali ili wananchi na taifa liweze kunufaika na maendeleo ya Tehama nchini kuelekea mapinduzi ya nne ya viwanda.

Nape alisema Tanzania imeamua kujikita kujenga uchumi wa kisasa wa kidijitali kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambapo mafunzo haya ni hatua ya kujenga msingi imara ili kuwa na Tanzania ya kisasa ili tuweze kujiunganisha na dunia.

Naye Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Jim Yonazi alisema ana amini baada ya mafunzo hayo Serikali itabadilisha kabisa namna ya utendaji kazi kwa kuongeza matumizi ya Tehama katika kukuza, kuendeleza na kuongeza matumizi ya uchumi wa kidijitali na Serikai itatumia fursa hii ya kidijitali kuhakikisha sekta mbalimbali zinatumia uchumi wa kidijitali ili kuwezesha muingiliano wa masuala ya Tehama.

“Ni muhimu kwa taasisi zetu kuweka mipango mizuri ili kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa zilizopo ili tuweze kuhakikisha kuwa usalama, faragha, ujuzi unapatikana ili wananchi na taifa waweze kunufaika na uchumi huu wa kidijitali,” alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk. Jabir Bakari alisema mafunzo haya yataiwezesha Serikali kutambua tuko wapi katika nyanja ya ukuaji wa uchumi; tunapotaka kwenda ili Tehama iweze kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Alisema mafunzo hayo yamejumuisha viongozi mbalimbali ambao ni watunga sera na wafanya maamuzi ili kuwa na uelewa wa pamoja wa namna bora ya kutumia Tehama katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali kwa kuangalia upya sera zilizopo nchini ili nchi yetu iweze kufika mbali na kwa tija zaidi.

Dk. Bakari alisema TCRA inaendelea kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuwawezesha wawekezaji kuwekeza nchini ili wananchi wapate huduma bora na za uhakika za mawasiliano ambapo Serikali inaandaa na kuboresha sera, sheria na kanuni.

Mafunzo hayo yamehudhuriwa na baadhi ya mawaziri; makatibu wakuu; wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali ya Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na yanatolewa na wataalam wabobezi wa ndani na nje ya Tanzania.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Wakili: Ukimpa zawadi mwenza marufuku kumpora hata mkiachana

Spread the love  WANANDOA na watu waliko kwenye mahusiano ya kimapenzi, wamekumbushwa...

Habari Mchanganyiko

Majaliwa: Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

Spread the love  WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino...

Habari Mchanganyiko

Exim Bank yatoa  vitanda kwa shule ya Jeshi la Polisi Moshi

Spread the love  BENKI ya Exim imekabidhii  seti ya vitanda kwa Shule...

Habari Mchanganyiko

NBC yakabidhi vitanda Shule ya Polisi Moshi

Spread the loveBenki ya NBC imekabidhi msaada wa vitanda 28 kwa Shule...

error: Content is protected !!