Tuesday , 7 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sakata la kujiondoa SUK: ACT-Wazalendo yamhoji maswali 8 Rais Mwinyi
Habari za Siasa

Sakata la kujiondoa SUK: ACT-Wazalendo yamhoji maswali 8 Rais Mwinyi

Spread the love

CHAMA cha ACT-Wazalendo, kimemhoji maswali nane Rais Dk. Hussein Mwinyi, kikimtaka atoke hadharani ayajibu, kuhusu madai yao ya kutaka kujiondoa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Maswali hayo yameulizwa leo Ijumaa na Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa Radhu, baada ya hivi karibuni baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), visiwani humo kudai mambo yanayowafanya watishie kujiondoa SUK, hayako kwa mujibu wa sheria na msimamo huo ni kinyume cha katiba.

Miongoni mwa maswali ambayo ACT-Wazalendo imemtaka Rais Mwinyi ajibu ni kuhusu ahadi alizotoa kwa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Hayati Maalim Seif Sharif Hamad, kabla hajakubali ombi la kuunda ushirikiano serikalini ili kutibu majeraha yaliyojitokeza katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Moja, baada ya kuapishwa kuwa Rais, Dk. Mwinyi hakutuma ujumbe akutane na Maalim Seif wazungumze? Nakusudia Novemba 2020 baada ya yote yaliyotokea na kuapishwa kuwa Rais je hakutuma ujumbe kuomba wakutane wazungumze?” amesema Jussa.

Maswali mengine ambayo chama hicho kimemtaka Rais Mwinyi ayajibu ni je, hawakukubaliana na Maalim Seif kuhusu hoja zake tatu na kumwandikia kwa maandishi ili azitekeleze. Lingine, hakumuahidi Maalim Seif kwamba hoja hizo amezikubali na kuomba washirikiane kuzitekeleza pamoja kupitia SUK.

“Nne je, yeye mwenyewe Rais Mwinyi hakutuambia sisi viongozi wa ACT tulipokwenda kumuona na kumkumbusha utekelezaji wa hoja tatu hizo baada ya kifo cha Maalim Seif na kwamba tumpe muda mpaka apewe umakamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar sababu sekretarieti ya CCM iliyokuwepo ilikuwa haimsaidii na wala haimuungi mkono?” amesema Jussa.

Akiendelea kuuliza maswali hayo, Jussa alihoji “tano je anaweza kutoka hadharani na kusema kwamba yeye sio aliyeleta salamu kupitia makamu wa kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman kuomba radhi baada ya uteuzi wa mkurugenzi wa uchaguzi na kuahidi kumuondoa? Sita, tunataka atuambie ni katiba ipi na sheria ipi inayosema kura zisihesabiwe na atangazwe mshindi bila kuzihesabu?”

Jussa amesema, swali la saba ni katiba ipi iliyompa mamlaka ya kuiamrisha mahakama kuondosha kesi zilizofunguliwa na ACT-Wazalendo kuhusu uchaguzi wa 2020 kwa hoja kwamba walizungumza na Maalim Seif wakati si kweli na swali la mwisho kama kuna wanachama wa CCM waliopata madhara ikiwemo kupoteza maisha kupitia vurugu za uchaguzi huo, kwa nini wasioneshe orodha yao kama chama chake kilivyofanya.

Jussa amesema ACT-Wazalendo kinataka kujiondoa SUK kikidai Rais Mwinyi amevunja uaminifu katika kutekeleza hoja tatu alizokubaliana na Maalim Seif kabla ya kukubali kujenga umoja wa kitaifa na kushiriki serikalini.

Hoja hizo tatu ambazo wanachama wa ACT-Wazalendo walimtaka Maalim Seif awasilishe kwa Rais Mwinyi kwa ajili ya utekelezaji na kwamba kiongozi huyo wa Zanzibar hajazifanyia kazi ni, uundwaji wa tume huru ya kimahakama ya kiuchunguzi kwa ajili ya kuchunguza  matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyotokea katika uchaguzi wa 2020.

Lengo la uundwaji wa tume hiyo ni kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika nayo na kuwalipa fidia waathirika.

Hoja nyingine ni Serikali yake kufanya maboresho ya mfumo mzima wa uchaguzi visiwani humo, ikiwemo kuiboresha Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), sheria za uchaguzi na zinazosimamia vyombo vinavyotekeleza zoezi hilo ikiwemo mahakama, polisi na idara nyingine za serikali.

Hoja ya mwisho ni uanzishwaji wa tume ya kudumu ya maridhiano na umoja wa kitaifa itakayosaidia kazi ya kujenga na kuimarisha maridhiano na umoja wa kitaifa kuanzia ngazi ya taifa hadi chini kwa wananchi.

Jussa amesema ACT-Wazalendo kinamtaka Rais Mwinyi athibitishe nia yake njema kuhusu utekelezaji wa hoja hizo alizokubaliana na Maalim Seif.

“Maalim Seif alimwambia tumeona wewe ni mtu tunayeweza kufanya naye kazi, tunayeweza kusikilizana na kukupa nafasi uthibitishe nia yako njema ambayo imetufanya sisi tutangulize nchi kwanza licha ya madhila yote yaliyojitokeza. Tunamuomba Rais Mwinyi ajiulize kathibitisha hiyo nia yake njema?” amesema Jussa.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Wanaotaka kujifunza ZEC kwao kukoje?

Spread the loveMKURUGENZI wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Thabit Idarous...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Biteko, Nape wanadanganya?

Spread the loveKWA mila na desturi zetu za Kiafrika mkubwa huwa hakosei,...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miamka 60 ya Muungano: Tunakwama wapi?

Spread the loveRAIS wa Jamhuri, Samia Suluhu Hasssan, Ijumaa iliyopita, aliongoza mamilioni...

ElimuHabari za Siasa

Serikali kuongeza wanufaika mikopo ya elimu ya juu

Spread the loveSERIKALI imesema itaongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu...

error: Content is protected !!