Monday , 6 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Mfuko wa SELF ngazi ya ‘kubadilisha maisha’
Habari Mchanganyiko

Mfuko wa SELF ngazi ya ‘kubadilisha maisha’

Afisa Muendeshaji wa Mfuko, Mudith Cheyo
Spread the love

 

MFUKO wa Self unaoendeshwa na Serikali, unakusudia kupanua wigo wa utoaji ukilenga kutimiza idadi ya matawi 20 nchi nzima, hatua inayotokana na mafanikio ya mfano ya kutoa Sh. 314 Bilioni za mikopo mpaka sasa kwa wananchi wenye mahitaji. Anaripoti Jabir Idrissa, Dar es Salaam … (endelea).

Mbele ya Wahariri wakiwemo wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), uongozi wa SELF umejieleza kwa sauti kuu ukionesha maendeleo makubwa waliyoyafikia tangu mwaka 2015 mfuko ulipokabidhiwa majukumu yaliyokuwa yakifanywa na mradi uliokuwa chini ya ofisi ya Makamo wa Rais, ukiwa na dhima ya kubadilisha maisha ya watu kwa kutoa huduma ya sekta ndogo ya fedha kwa masharti nafuu.

Moja ya hatua za kimaendeleo ambazo Mfuko wa SELF umefikia, ni kuwezesha kutungwa sheria mahsusi mwaka 2018 ya kuongoza na kusimamia sekta ndogo ya fedha nchini kupitia utaratibu wa kuzipatia fedha za mikopo taasisi za kifedha kwa ajili ya kuwafikia wananchi wanaojishughulisha na uzalishaji mali pamoja na mwananchi mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na Kurugenzi ya Biashara ya SELF, wanatoa mikopo midogo kwa watu binafsi ikitangulia na kazi ya kutoa elimu ya usimamizi wa fedha hasahasa kwa asasi zinazokopesha wajasiriamali wenye miradi midogo na ya kati (SME) ya kuzalisha bidhaa pamoja na vyama msingi vya ushirika (SACCOS).

Huduma za mfuko kwa sasa ambazo zinatolewa kupitia matawi yake 12 yalioko mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Arusha, Mtwara, Tanga, Zanzibar, Dodoma, Iringa, Songwe, Mbeya, Rukwa, Geita na Mwanza zimefikia zaidi ya watu 310,000 – asilimia 53 wakiwa ni wanawake.

Kutokana na mikopo waliyoitoa, zaidi ya ajira 37,000 zimezalishwa wakati asasi za Star Natural Product Ltd ya Dar es Salaam inayotengeneza mafuta ya kupikia kutokana na michikichi; na Bright Future Academy ilioko Zanzibar inayoendesha shule baada ya kujenga madarasa 32, zinaongoza kwa ufanisi. Star imekopeshwa zaidi ya Sh. 100 milioni na Bright Future kupata mkopo wa zaidi ya Sh. 300 milioni.

Taarifa inaonesha kuwa ifikapo mwaka 2026, mfuko utakuwa umeongeza matawi manane kutimiza idadi ya matawi 20 nchi nzima na kufanikiwa kutia faida kutokana na fedha za serikali na kupeleka mchango wake kila mwaka kwenye mfuko mkuu wa mapato wa serikali.

Akizungumza kwenye majumuisho ya mkutano juzi, Afisa Muendeshaji wa Mfuko, Mudith Cheyo alisema pamoja na hatua mbalimbali za kuimarisha huduma wanazotoa, jitihada kubwa zinafanywa ili kuhakikisha mfuko unaendelea kuwa endelevu ukishughulika na kuelimisha wakopaji namna bora ya kusimamia matumizi ya mikopo wanayopata.

Cheyo anasema njia mojawapo ni kusaidia asasi kopeshaji kutunga sera za ukopeshaji na ukaguzi huku wakitilia mkazo udhibiti wa fedha kutozipeleka nje ya makusudio.

Amesema mafanikio mengine wanayojivunia ni kushirikiana na mashirika mengine katika kuongeza huduma kama za bima na kuweka dhamana kwa wakopeshaji kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Bodi ya Kahawa nchini ambayo hutoa vifaa badala ya fedha taslim kwa asasi kopeshaji.

Mfuko wa SELF pia hauko nyuma katika kutumia maendeleo ya teknolojia yanayozidi kukua ili kuimarisha mifumo ya kuhudumia wanaohitaji huduma wanazotoa kwani nao wanazingatia mkazo wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuendesha mageuzi ya kiuchumi chini ya mifumo ya kidigitali.

Written by
Jabir Idrissa

+255 774 226248

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Tanzania  yasisitiza kuwa Kituo Kikuu cha Uchimbaji Madini Afrika

Spread the loveTanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

error: Content is protected !!