Monday , 6 May 2024
Home Kitengo Maisha Afya Magonjwa yasiyoambukiza tishio, vyombo vya habari vyatakiwa kuelimisha umma
AfyaHabari Mchanganyiko

Magonjwa yasiyoambukiza tishio, vyombo vya habari vyatakiwa kuelimisha umma

Spread the love

VYOMBO vya habari vimetakiwa kuongeza jitihada katika elimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD’s) ili kukabiliana na janga hilo ambalo sasa likadiriwa kusababisha asilimia 27 ya vifo vyote nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Magonjwa hayo yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya moyo, mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari, magonjwa ya figo, ini kongosho, kuoza meno na magonjwa ya meno, mwaka 2016 yametajwa kusababisha vifo milioni 42 duniani sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi mkazi wa PharmAccess Dk. Heri Marwa alipozungumza na wahariri, waandishi wa habari na wana mitandao wanaopakia maudhui katika mitandao ya kijamii katika kikao kazi cha siku moja.

Kikao kazi hicho kinalenga kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya NCD’s ndani ya jamii, kimeandaliwa na PharmaAccess, Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza  (TANCDA), WHO na Wizara ya Afya.

Mkurugenzi mkazi wa PharmAccess Dk. Heri Marwa

Amesema magonjwa hayo yasiyoambukiza yameendelea kuongeza nchini na duniani hali inayoathiri jamii kwa kusababisha umaskini kwenye kaya na hata Taifa kutokana na nguvu kazi inayopotea pindi kunapotokea mgonjwa na vifo.

Ametoa mfano kuwa mashirika makubwa ya hisani yamewekeza fedha nyingi kwenye magonjwa yanayoambukiza kama vile Virusi Vya Ukimwi, lakini upande wa magonjwa yasiyoambukiza hakuna fedha za kutosha kukabiliana nayo hali inayozidisha uhatari hasa kwa nchi maskini.

Kutokana na hali hiyo, ametoa rai kwa vyombo vya habri kuongeza idadi ya vipindi, habari na makala zenye maudhui ya elimu ya kinga dhidi ya magonjwa hayo ambayo yamezidi kuwa tishio hivi sasa nchini.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa

Rai hiyo imeungwa mkono pia na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa ambaye amesema takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa mwaka 2012 zinaonesha asilimia 7 ya Watanzania wana ugonjwa wa figo, asilimia 9 kisukari na asilimia 29  wana shinikizo la damu hali inayodhihirisha namna magonjwa hayo yanaitesa jamii.

“Kati ya Watanzania watatu kuna mmoja ana ugonjwa usio wa kuambukiza, aidha kati ya vifo vitatu kuna kimoja ambacho kimesababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) unatumia 40% ya mapato yake kugharamia matibabu ya NCD’s.

“Yaani zaidi ya Sh. Bil. 137 kwa kipindi cha miaka mitatu zimetumika kutibu ni sawa na 18% ya fedha za NHIF.

“Tukiacha changamoto ya wengi kushindwa kugharamia matibabu, ni muhimu jamii kujikinga kwani ikiwa haitajikinga ni wazi NHIF itatumia gharama kubwa zaidi kuwatibu (miaka ijayo).

Msigwa amesisitiza “Tunahitaji tuongeze jitihada kwenye kuelimisha, kwa sasa Serikali inafanya mapitio ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 na imefikia hatua nzuri ngazi ya Makatibu Wakuu.

“Mkazo mkubwa ni kwenye kutoa elimu ya afya, lakini tunayo Sera ya 2007, Mkakati wa 5 wa Sera ya Afya, Mpango Mkakati wa Kudhibiti na Kupambana na NCD’s 2021/26 zote hizi ni jitihada za Serikali.

“Tunazoionesha na maana yake ni kwamba Serikali tupo tayari kushirikiana na wadau katika kutokomeza magonjwa haya,” amesisitiza.

Amehimiza wadau kushirikiana bega kwa bega na vyombo vya habari ikiwamo kuunda mpango kazi (Communication Strategy) ya uelimishaji jamii katika uelimishaji pamoja na kuweka ufadhili wa vipindi.

Naye, Dk. Omary Ubuguyu kutoka Wizara ya Afya amesema suala la kupambana na NCD’s ni mtambuka na muhimu wadau wote kushiriki ikiwamo jamii yenyewe.

“Mwaka 1960 wengi waliokufa walitokea nchi za magharibi na ilikuwa na vifo vingi zaidi, Finland ilikuwa na vifo vya juu kuliko nchi yoyote (duniani).

“Walisema ni mtambuka na si afya peke yake waliwekeza mkakati kwenye jamii kuelimisha, iliwasumbua pombe, nyama na mazao ya nyama kupita kiasi.

“Hawakuwa na ‘risk’ ya vitambi, walikuwa na colestol nyingi, waathiri walikuwa wanaume, walitafuta wanawake maarufu, wanahabari waliungana na kuelimisha, namna ya kuandaa chakula.

“Chakula kilianza kubadilika ‘culture’ zikabadilika, waliingia kwenye mazoezi, sasa wanafanya vizuri.

“Si madaktari tu watatutoa hapa tuliopo, tutapotea kama tutategemea madaktari na watu wengine wa afya watutoe (wote tuhusike katika mapambano),” amesisitiza.

Naye, Dk. Alphonsina Nanai anayeshughulikia magonjwa yasiyoambukiza WHO Tanzania amebainisha ifikapo 2030 dunia imedhamiria kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa hayo duniani.

“Mahitaji yanazidi kuwa makubwa, tatizo hili ni kubwa, takwimu za mwisho zinaonesha katika vifo mil. 41, vifo mil 31.4 ilikuwa kwa sababu ya NCD’s.

“Ukiangalia ni 74% ya magonjwa yote yalisababishwa na NCD’s mwaka 2008 vifo mil 17 walikuwa chini ya miaka 70 kwa sababu ya NCD’s.

Mwenyekiti wa chama cha wagonjwa wa kisukari na umoja wa maradhi yasiyoambukiza, Andrew Swai amesema asilimia “86 ya vifo vyote ilitoka nchi zinazoendelea (ikiwamo Tanzania) zaidi ya robo tatu ya vifo hivi na mzigo huu unatoka kwenye nchi hizo.

“Tunavyozidi kuendelea tunaona kuna magojwa kwa mfano shinikizo la damu na yanayohusisha mfumo wa damu ndiyo yanayosababisha vifo vingi zaidi kuliko mengine.

“Kuna saratani, presha, kisukari 80% unakuta ni haya na mengine unakuta ni mengi, WHO inapenda kupunguza kwa moja ya tatu 2030 na vifo chini ya miaka 70,” amesisitiza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Tanzania  yasisitiza kuwa Kituo Kikuu cha Uchimbaji Madini Afrika

Spread the loveTanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

error: Content is protected !!