Monday , 6 May 2024
Home Habari Mchanganyiko “Jamii ielimishwe faida za uhifadhi”
Habari Mchanganyiko

“Jamii ielimishwe faida za uhifadhi”

Spread the love

WIZARA ya Maliasili na Utalii imesema ili kukabiliana na migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni vema kwa wadau wote kushiriki kutoa elimu kwa jamii juu faida za uhifadhi, mazingira na viumbehai waliopo. Anaripoti Selemani Msuya … (endelea).

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Maliasili na Utalii, John Mapepele wakati akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), waliokuwa wanashiriki mafunzo juu ya Miradi wa Kupunguza Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori.

Mradi huo ambao unatekelezwa katika vijiji 30 vilivyopo wilayani Liwale mkoani Lindi, Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma unafadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mapepele alisema hakuna njia mbadala ya kumaliza migongano ya binadamu na wanyamapori tofauti na wadau kushiri kutoa elimu, huku akiwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa kuandika habari zenye mtazamo chanya ili jamii iweze kubadilika kwa haraka.

Mkuu wa Kitengo amesema lengo la mradi huo ni kuwajengea uelewa jamii inayoishi karibu na maeneo ya hifadhi, ili wawe na uwezo wa kudhibiti na kutatua changamoto baina yao na wanyamapori, huku wakiamini kuwa wanawajibu wa kuishi nao kwa upendo.

“Migongano baina ya binadamu na wanyamapori ipo na haiwezi kuisha kwa haraka, kinachotakiwa ni sisi serikali, wadau wa uhifadhi kama JET, GIZ na waandishi wa habari kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii inayoishi karibu na hifadhi, shoroba, mapori ya akiba na tengefu kuwa wanapaswa kuishi na wanyamapori kwa upendo, kutokana na ukweli kuwa asilimia kubwa binadamu ndio wameingia kwenye maeneo ya wanyamapori,” amesema.

Mapepele amesema matumaini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuwa kupitia mradi huo migangano baina binadamu na wanyamapori itapungua kama sio kuisha kabisa.

Mkuu huyo amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 21 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni, hivyo hakuna namna ya kuacha migongano hiyo kuendelea, bali ni wadau wote kushiriki kutoa elimu kwa jamii, hali ambayo itachangia ongezeko la mapato.

Amesema sekta hiyo imekuwa na mchango mkubwa kwa jamii hasa vijana na makundi mengine hivyo elimu ikiendelea kutolewa ni wazi faida zitaongezeka kama ajira na uhifadhi.

Mapelele amesema uhai wa viumbehai vyote  unategemea mazingira bora na rafiki, hivyo ili kuwepo na uendelevu ni jukumu la waandishi kuandika bahari za uchechemuzi kuhusu eneo hilo lenye fursa nyingi za kiuchumi.

Mkuu huyo amesema wizara yao inatumia mbinu mbalimbali kutangaza utalii nje na ndani ya nchi, hivyo haitapendeza juhudi hizo zipotee bila kuleta faida kwa jamii.

“Wananchi au jamii inayoishi karibu na hifadhi na misitu wanapaswa kufaidika na rasilimali zilizopo ila kwa utaratibu wa kisheria, lakini hilo watalijua iwapo nyie wandishi mtaamua kuliandika kwa kina na ufasaha,” amesema.

Amesema Tanzanian inasifika kwa kuwa na wanayama wengi hali ambayo inavutia watalii, hivyo serikali itahakikisha fursa hiyo inakuwa endelevu, huku wanadamu nao wakipata haki zao.

Amesema kwa sasa sekta hiyo imezidi kupaa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia mwenyewe moja kwa moja kuitangaza, hivyo iwapo kutakuwa na migongano baina ya wanadamu na wanyamapori faida haitakuwepo.

Mshauri kutoka Shirika la GIZ, Anna Kimambo amesema wameamua kushirikiana na serikali kutoa elimu kwenye maeneo yenye migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na uendelevu.

Amesema changamoto kwenye vijiji 30 vya mradi ni kubwa ila kwa ushirikiano ambao serikali na wadau wengine wakiwemo waandishi wa habari ni imani yao hali itakuwa nzuri na binadamu na wanyamapori wataishi pamoja kwenye hifadhi na shoroba.

“Tunaamini elimu ikitolewa kwa ushirikiano wa wadau wote, ikiwemo waandishi wa habari kuandika habari za ukweli na uhakika, hali itakuwa nzuri, kuna wakati unasikia habari mpaka unakosa amani, lakini msingi wake ni kukosekana taarifa sahihi, ila kupitia JET na nyie tunatarajia kuona na kusoma taarifa zenye tija kwa sekta hii,” amesema.

Kimambo amesema GIZ inatekeleza mradi huu wa mwaka mmoja kwa kutambua faida zilizopo kwenye uhifadhi, hivyo ni matumaini yake kila mdau atashiriki kuhakikisha mafanikio chanya yanapatikana.

Mshauri huyo amewaomba waandishi wa habari kuzingatia misingi ya uandishi ili taarifa zao ziweze kuleta matokeo chanya kwa haraka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa JET, John Chikomo amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika masuala ya uhifadhi, mazingira na shoroba.

Amesema wamechagua waandishi wachache na wameanza kwa kuwapatia mafunzo kuhusu eneo hilo na baadae wataenda kutembelea vijiji 30 kwa makundi ili waweze kuona hali ilivyo kuhusu migongano ya binadamu na wanyamapori.

“Tumewachagua nyie kwa kuzingatia mambo mengi, lakini pia hatutasita kumuacha mtu ambaye haendani na kasi yetu, JET tunataka mabadiliko chanya kwenye sekta ya utalii na maliasili, ili iweze kuchangia pato kubwa zaidi kwa nchi,” amesema.

Naye Mkufunzi na Mwandishi Mkongwe, Pili Mtambalike amewataka waandishi wa habari kuandika habari ambazo zitaleta mabadiliko chanya kwa jamii husika.

“Mnatakiwa muandike habari zenye tija na zinazofuata misingi ya uandishi wa habari, eneo hili ni muhimu sana iwapo litaripotiwa kwa kufuata misingi ya uandishi,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Tanzania  yasisitiza kuwa Kituo Kikuu cha Uchimbaji Madini Afrika

Spread the loveTanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

error: Content is protected !!