JESHI la Israel, limerejesha mashambulizi katika ukanda wa Gaza, baada ya kundi la wanamgambo wa kiislamu la Hamas, kudaiwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, pamoja na kuwaacha huru mateka wote wa taifa hilo. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Kwa mujibu wa mtandao wa BBC Swahili, mashambulizi hayo ya Israel yameanza baada ya wanamgambo wa Hamas kuwafyatulia risasi wanajeshi wake, pamoja na kurusha roketi angani.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amedai Hamas haijawaacha huur mateka wanawake kama walivokubaliana, badala yake wameanzisha mashambulizi asubuhi ya leo Ijumaa.
Jeshi la Israel na Hamas, walikubali kusitisha mapigano kwa muda, ili kutoa nafasi ya mateka wa pande zote mbili, kuachwa huru.
Hadi sasa Jeshi la Israel linasambaza vipeperushi vya onyo kwa wapalestina waishio kusini mwa Gaza, ikiwataka waondoke katika eneo hilo mara moja, kwa kuwa eneo hilo ni hatari kwa ajili ya mapigano.
Mtandao wa Aljazeera umeripoti kuwa, tangu Israel ianzishe mashambulizi hayo, watu zaidi ya 15 wamefariki dunia.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, amelaani mapigano kuanza upya, huku akitaka mpango wa kuyasitisha kwa muda ujadiliwe upya na pande zote mbili.
Leave a comment