Tuesday , 7 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Aliyeondolewa kesi ya ugaidi adaiwa kutekwa kweupe
Habari MchanganyikoTangulizi

Aliyeondolewa kesi ya ugaidi adaiwa kutekwa kweupe

Spread the love

WAKATI masikio ya Watanzania yakiwa yamepumzika kusikia taarifa za kutekwa au kuuawa raia na watu wasiojulikana, matukio hayo yanaanza kurejea taratibu.

Tukio la kutekwa na kupelekwa kusikojulikana Rashid Mitambo aliyeachwa Machi mwaka huu kwenye kesi ya ugaidi limesababisha hali hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu… (endelea).

Mitambo alikamatwa kwa tuhuma za ugaidi mwaka 2016 na kesi yake kuondolewa mwaka huu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuamua kutoendelea nayo.

Mke wa Mitambo aitwaye Mwajuma Raisi akizungumza na wanahabari Dar es Salaam juzi, alisema mumewe alifuatwa Agosti 17 mwaka huu, na watu wasiozidi sita akiwa Tandika kwenye shughuli zake za ushonaji, wakamtia pingu na kumwingiza kwenye gari.

Mke wa Rashid Mitambo

Mwajuma alisema kwa mujibu wa mashuhuda, ambao ni wamiliki wa maduka ya karibu na shughuli yake, waliona gari Toyota IST namba T748DHF likitumika kumchukua mumewe.

Alisema alipopata taarifa hizo, alikwenda kituo cha Polisi Chang’ombe, ambako mumewe alitakiwa kuripoti tarehe 15 ya kila mwezi kwa miaka miwili tangu alipoachwa.

Alisema alipofika kituoni hapo, askari walimwambia hayupo, akaenda kituo cha Buguruni ambako pia hakuonekana.

“Juzi Ijumaa, nikaenda kituo kikuu cha Polisi Dar es Salaam, pale nikaambiwa niende Oysterbay huko kote sikumkuta na wala polisi hawakunipa maelezo ya matumaini,” alieleza huku machozi yakimlenga.

Alieleza hofu yake, kuwa pengine hayuko hai, kwani zipo taarifa za watu watatu kuokotwa kwenye viroba wakiwa wameuawa.

“Nina shaka na uhai wa mume wangu, juzi nilisikia taarifa kwenye vyombo vya habari, kuwa wameokotwa maiti watatu na sijapata taarifa yoyote mpaka sasa,” alizungumza huku akifuta machozi.

Latifa Mitambo, mtoto wa Rashidi Mitambo alisema baba yake ametoweka na wamekwenda takribani vituo vyote vya Polisi kumwulizia lakini bila kumpata.

“Kama wangekuwa na shida naye, wadhamini wake wangejua baba tunadhani hayuko kwenye mikono salama,” alilalamika Latifa.

Alisema yeye ni mtoto wa tatu katika familia ya Mitambo, na tangu mwaka 2016 ndugu zake hawajafaidi malezi ya baba yao baada ya kukamatwa na kutuhumiwa ugaidi.

Alisema hawajawahi kusikia baba yao akiwa na ugomvi na mtu yeyote mtaani au kupigana. “Baba yangu kusema kweli ni mwenye mwenendo wa wazi kwenye jamii.”

Gazeti hili lilimpigia simu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kuhusu suala hilo, akasema Jeshi lake linalifanyia uchunguzi.

“Jambo hilo nalisikia kwako, lakini jukumu la Jeshi la Polisi ni kufanya uchunguzi, tutalifanyia uchunguzi suala hilo,” aliahidi Kamanda Muliro.

Matukio ya watu wasiojulikana kyuteka na kushambulkia watu walijitokeza sana katika Serikali ya awamu ya tano na kuzusha hofu miongoni mwa watu, huku Jeshi la Polisi likiahidi kuchunguza na kuchukua hatua.

Hata hivyo, uchunguzi huo haujafanikiwa kuwabaini watu hao na hivyo hakuna aliyekamatwa na kufikishwa mahakamani kuhusu mashambulizi dhidi ya Makamu wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu.

Lakini pia, kuhusu kupotea kwa aliyekuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ben Saanane na aliyekuwa mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited, Azory Gwanda.

Ni katika awamu hiyo pia ndipo miili ya watu wasiojulikana ilipogundulika ikiwa ndani ya mifuko ya sandarusi ikielea mtoni na baharini.

Hata hivyo pia miezi ya mwanzoni mwa mwaka huu, vijana watano waakzi wa Dar es Salaam walitoweka na mpaka leo haijulikano waliko, na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillius Wambura ameahidi kulishughulikia kwa kuwasiliana na wazazi wao.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Samia aagiza huduma za dharura maeneo yaliyoathiriwa na kimbunga Hidaya

Spread the love   RAIS wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Samia...

Habari Mchanganyiko

Mahakama yatoa uamuzi zuio dhidi ya Club House

Spread the loveMAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu jijini Dar es Salaam,...

Habari Mchanganyiko

GGML, OSHA yawanoa bodaboda 200 Arusha

Spread the loveZAIDI ya madereva bodaboda 200 wa jiji la Arusha wamepatiwa...

Habari za SiasaTangulizi

Jacob, Malisa wapandishwa kizimbani kwa mashtaka ya uongo mitandaoni

Spread the loveMKURUGENZI wa Shirika la Haki, Godlisten Malisa na mwanachama wa...

error: Content is protected !!