Sunday , 28 April 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Balozi Seif Ali Idi ana hali gani?
Makala & Uchambuzi

Balozi Seif Ali Idi ana hali gani?

Balozi Seif Ali Iddi.
Spread the love

 

MNIJUZE wakazi wa Zanzibar, taswira halisi ya Balozi Seif Ali Idi, Makamu wa Pili Mstaafu visiwani humo ilivyo kwa sasa, je ni mwenye furaha? Anaandika Yusuph Katimba…(endelea).

Mie nipo zangu huku bara naendelea na majukumu yangu. Natamani kujua mwonekano wa Balozi Idi hasa baada ya kupata habari, kwamba wale aliosema ‘wananyea ndoo bara,’ sasa wamerejea nyumbani.

Anaonekanaje baada ya kubaini ukweli, kwamba viongozi wa Uamsho wameungana na familia zao, ndoo walizokuwa wakinyea wameziacha walikozikuta. Sasa wanatumia vyoo vya kuflashi kama yeye.

Nataka kujua hivyo hasa nikirejesha kumbukumbu zangu kuhusu kauli yake aliyoitoa Julai 2017 visiwani humo, huku akishangiliwa na waliomshangilia.

Nakumbuka, kwenye moja ya mkutano wa hadhara visiwani humo, akiwa amevalia sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Seif alitamka maneno yafuatayo.

“….wasisahau vyombo vya dola vipo, vitawashughulikia. Vyombo vya dola vipo, vitawashughulikia. Uamsho upo wapi sasa hivi?

“Uamsho kama wanaweza wajaribu tena, Dk. Salmin alisema, nikisikiliza hotuba zake kila subuhi anasema, dola haichezewi, wajaribu kuichezea dola, wenzao saa hizi wapo bara kule wananyea ndooni,” ni kauli ya Balozi Seif aliyoitoa 2017.

Bila shaka, busara na hekima ni maneno yenye herufi chache zilizobeba uzito wa maana isiyomithilika, maneno haya si mepesi katika kuyatumia kama nyenzo katika utawala isipokuwa kwa mwenye uono.

Ndani ya busara kuna matokeo ya mambo mengi ikiwa ni pamoja na werevu, maarifa, ujanja, ujuzi pia fikira, kwa muktadha huu, kiongozi yeyote anapaswa zaidi kuwa na busara katika kila kilichopo mbele yake.

Busara huwa dhahiri pale lugha itumikapo katika kuelezea, kunasihi au kuhimiza jambo fulani, pia huweza husaidia kujenga uelewano na uhusiano kati ya mtawala na mtawaliwa.

Kiongozi hupata sifa nzuri na kuheshimika anapotumia busara kwa kauli na vitendo vyake, kinyume na hivyo hujenga kumbukumbu mbaya ambayo hubebwa kwenye vifua vya anaowatawala.

Hili linaweza kuthibitishwa na ziara ya Dk. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar alipomtembea Balozi Seif nyumbani kwake katika Wilaya ya Kaskazini B, Unguja, Februari 2021.

Matokeo ya ziara hilo kwa Wazanizbari yalikuwa ni makombora kwa Balozi Idi huku wakimlaumu Dk. Mwinyi kwa kumtembelea, wengi walioniesha kukerwa huku wakimkumbusha ‘Uamsho bado wapo gerezani.’

Lujiulize, mbona Dk. Mwinyi alitembelea viongozi wengi lakini hakulaumiwa? lakini alipomtembelea Blozi Idi, Wazanzibari wakalipuka, ni kwa kuwa walirejea matamshi hasi ya Blozi Seif Idi.

Kwa muktadha huo, kauli yake aliyoitoa 2017 kuhusu Uamsho, inaweza kumtesa kwa muda mrefu kama ile aliyoitoa Nape Nnauye kuhusu ‘CCM itashinda hata kwa Bao la Mkono.’

Mwandishi mmoja aliwahi kubainisha, busara na hekima hazipatikani kama nguo za kununuliwa dukani. Ni dhana adhimu zilizomo ndani ya silika ya mwanadamu.

Huchomoza pale mtu atumiapo akili na fahamu zake kwa uadilifu katika kuunganisha tabia za watu kufanya mema na kuacha mabaya.

Dhana hizo pia hupimwa na hutolewa maana na tafsiri na watu mbalimbali wanaopokea lugha inayozungumzwa na mtu au kiongozi yeyote aliyekusudia ujumbe wake kuwafikia walengwa. Mapokezi yake huwa chanya au hasi.

Kauli ya Balozi Idi ndani na nje ya visiwa vya Zanzibar inazama kwenye tafsiri halisi ya kiongozi huyo wakati akihutubia wananchi wake kuhusu Uamsho.

Dunia ilivyoumbwa na Muumba, kila jambo lina ukomo, iwe uhai ama kifo, mapenzi, madaraka na hata ujinga. Muhimu katika yote hayo ni subira kufikia wakati.

Upo msemo kwamba, ‘weka akiba ya maneno,’ tungo hii ni maarufu ambayo hutumika kuonya ama kutoa tahadhari. Walio na busara hutumia tungo hii kulinda ndimi zao. Daima hufanikiwa.

Uongozi wenye busara hutawaliwa na kuchunga ndimi, maisha yale leo si ya kesho, hivi ndivyo wazazi wetu wamekuwa wakituusia.

Tanzania imeshuhudia tukio zito, tukio lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na raia wa nchi hii bila kujali dini zao. Ni kuonekana kwa viongozi wa Uamsho kuwa huru.

Baragumu hili lilikuwa likipulizwa na kada zote, watetezi wa haki za binadamu, waandishi na wapenda haki wamekuwa wakishikamana kuhakikihsa Uamsho wanatendewa haki kikatiba.

Kutokana na umuhimu wake, Josephat Gwajima, Mbunge wa Kawe, Dar es Salaam ambaye pia Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amekuwa kielelezo kizuri cha Wakristo kutetea haki kwa masheikh wa Uamsho. Alifanya hivyo ndani ya bunge.

Wengi walisimama katika katika kutendewa haki na si upendeleo, ndio maana hata wasio Wasilam walisimama imara kutaka hatua za kisheria zichukuliwe.

Juhudi hizo zililenga kuzuia mazoea ya kuvunja sheria, hata mataifa yanayotaabika leo, msingi wake ulikuwa kuimarika tabia ya kupuuza katiba zao, mwisho wa siku ilijengwa mazoea na kuwa tabia mpya.

Nimalize kwa kauli ya waliotutangulia kuishi kwamba, ni bora kujikwaa kidole kuliko kujikwaa ulimu, kuna maisha baada ya madaraka.

1 Comment

  • SASA WANAWEWESEKA SEIF ALI IDI NA BABU ALI SABABU YA UOVU WALIOWATENDEA WA ZANZIBAR INCHI WAMEINAJIS NA SASA KUNA KAZI KUBWA YA KUMUOMBA ALLAH AITAKATISHE.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaMakala & Uchambuzi

Kanda ya Ziwa yaonyesha NMB inavyosaidia afya ya mama na mtoto

Spread the loveMafanikio inayozidi kupata Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

‘Mwanapekee’ wa Rais Samia: Atabadili nini Arusha?

Spread the loveMAPEMA wiki hii, baadhi ya viongozi walioapishwa na Rais Samia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

Kipunguni waihoji serikali, ziko wapi fedha za fidia?

Spread the loveWATU wanaodai kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu,...

Habari za SiasaMakala & UchambuziTangulizi

Askofu Bagonza: Tusichonganishwe; tusichokozane na tusikufuru

Spread the loveJOTO la chaguzi linapanda kila siku hapa nchini. Upo umuhimu...

error: Content is protected !!