WATANI wa jadi Simba na Yanga wameanza vema kuipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kuibuka na ushindi mnono ugenini katika raundi ya awali ya Ligi ya mabingwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Yanga waliokuwa katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam ambao umetumiwa na Klabu ya Zalan kutoka Sudan Kusini kama uwanja wao wa nyumbani, wameibuka na ushindi wa mabao 4 kwa nunge.
Mabao ya Yanga yamewekwa nyavuni na kiungo wao Feisall Salumu ‘Feitoto’ na mshambuliaji wao matata, Fiston Mayele aliyeondoka na mpira baada ya kupiga hattrick.
Aliyefungua karamu ya mabao alikuwa Mayele dakika ya 47, Feitoto dakika ya 54 kisha Mayele akamalizia misumari dakika ya 84 na 87.
Licha ya Yanga kupata ushindi huo, Zalan waliokolewa na golikipa wao baada ya kuokoa mashuti nane yaliyolenga lango katika kipindi cha kwanza na kuwafanya Yanga waende kujiuliza vyumbani katika dakika hizo 45 kabla ya kurejea na moto mkali.
Kwa upande wa Simba SC. ambao walikuwa ugenini nchini Malawi kupepetana na Nyasa Big Bullet, nao waliwatungua wenyeji hao bao 2-0.
Mabao ya Simba yamewekwa kambani na Moses Phiri dakika ya 29 na John Bocco dakika 84 na kuwafanya wekundu hao wa Msimba kurejea na matumaini tele nyumbani.
Kwa matoke hayo, timu hizo zimejiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye raundi ya kwanza katika Ligi hiyo ya Mabingwa Afrika baada ya kurejea wikiendi ijayo.
Leave a comment