April 13, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Wizara ya elimu yazitaka shule zote kuunda kamati, bodi

Spread the love

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, imewaagiza wathibiti ubora wa shule kuhakikikisha shule zote za msingi na sekondari zinakuwa na kamati na bodi zinazofanya kazi kwa mujibu wa sheria za elimu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).

Agizo hilo limetolewa jana Ijumaa tarehe 10 Julaia 2020, mkoani Morogoro na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo wakati akifunga mafunzo ya kuwaingiza kazini watumishi wapya pamoja na wathibiti ubora wa shule ambao wamehamia makao makuu ya wizara.

Alisema kuwepo kwa bodi katika shule za sekondari na kamati kwa upande wa shule za msingi ni utekelezaji wa sheria ya elimu Sura Na.353 (RE 2002)

Dk. Akwilapo alisema zipo shule ambazo zimekuwa zikiendeshwa bila ya kamati au bodi jambo ambalo linalosababisha changamoto katika uendeshaji, akitolea mfano shule ya Right Way ambayo imejidhihirisha kutokuwa na bodi ya shule na kuleta usumbufu wakati wanafunzi wakijiandaa kufungua shule tarehe 29 Juni 2020.

“Hivi karibuni mmiliki wa Shule ya Right Way ya Mbezi Beach Dar es Salaam, ameonesha dharau kwa wazazi, kamati ya shule na hata mamlaka za nchi. Hatuwezi kuwadekeza wamiliki wa shule kama hawa,” alisema Dk. Akwilapo.

“Anasema hawezi kuitisha kikao cha wazazi na hana kamati ya shule, hii ni kinyume kabisa na taratibu na kanuni. Ni jukumu lenu wathibiti ubora wa shule kwenda kuwaelekeza wamiliki wa shule ili wajitambue na waelewe namna walivyo na jukumu kubwa katika kuelimisha jamii,” alisema Dk. Akwilapo.

Aidha, Dk. Akwilapo aliwataka wathibiti ubora wakuu wa kanda na wilaya kuchukua jukumu la kuhakikisha walimu wote wa shule binafsi wanafanyiwa uhakiki kama ilivyofanyika kwa watumishi wa sekta ya umma pamoja na kuhakikisha ratiba za masomo zinazingatiwa.

“Tumepata malalamiko mengi sana kuhusiana na ratiba za masomo, kuna shule zinaanza masomo alfajiri saa 12 sasa unajiuliza huyu mtoto anaamka saa ngapi ili afike muda huo na wengine wanabakizwa shuleni mpaka saa 12 jioni hii sio sawa wathibiti mkaangalie na hilo,” alisema Dk. Akwilapo.

Katika hatua nyingine, Dk. Akwilapo aliwataka wathibiti ubora wa shule waliopata mafunzo kuhakikisha wanafuata kanuni na taratibu katika utendaji pamoja na kutumia busara na hekima katika utoaji wa maamuzi.

“Busara na hekima ndio nyenzo kubwa kwenye utumishi wa umma. Ni kweli tuna sheria na kanuni lakini mwisho wa siku Kiongozi unatakiwa utoe hukumu kwa hekima na busara huku ukiangalia mazingira yaliyopo,” alisema Dk. Akwilapo.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo ya kuingia kazini ambaye pia ni Mthibiti ubora wa shule Kanda ya Dar es Salaam, Alodia Ndumbaro alisema, mafunzo waliyoyapata yatawasaidia kufanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa kwani uthibiti ubora ni jicho la jamii ambalo linapaswa kuona changamoto zilizopo kwenye maeneo ya kazi wanayosimamia na kusaidia kutafuta ufumbuzi hivyo kuboresha utendaji kazi.

error: Content is protected !!