October 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkutano mkuu CCM: Profesa Lipumba asema furaha kwa Watanzania inawezekana

Spread the love

PROFESA Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amemuomba Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ahakikishe mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, unaendeshwa kwa haki na usawa, ili kuwapa fursa wananchi ya kuwachagua viongozi wanaowataka. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma…(endelea).

Prof. Lipumba ametoa ombi hilo leo Jumamosi tarehe 11 Julai 2020, wakati akitoa salamu za vyama  vya siasa vya upinzani, kwenye Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), unaofanyika jijini Dodoma.

Mbele ya wajumbe wa mkutano huo, Prof. Lipumba amekiomba chama hicho tawala kuhakikisha kampeni za uchaguzi huo zinafanywa kistarabu, pamoja na kushindana na kwa hoja.

“Ombi letu kwa mgombea mtarajiwa wa CCM wa Urais wa Tanzania na mwenyekiti wa CCM na chama kwa ujumla, tunaingia katika uwanja wa siasa wa kufanya kampeni za kutafuta chama gani cha kitakachoongoza nchi,” amesema Prof. Lipumba.

Prof. Lipumba amesema, “Tufanye kampeni za kistarabu tushindane kwa hoja, tuwape fursa Watanzania wachague kiongozi wanayemtaka.”

Aidha, Prof. Lipumba amewapongeza CCM kwa kufanya mkutano huo wa kuthibitisha wagombea wao wa Urais wa Tanzania na Zanzibar.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM wanatarajia kuthibitisha majina ya wagombea wake wa Urais wa Tanzania na Zanzibar.

Jana tarehe 10 Julai 2020, Rais Magufuli alichaguliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (CCM), kugombea Urais wa Tanzania, huku Dk. Hussein Mwinyi, akichaguliwa kuwa Mgombea wa Urais wa Zanzibar.

“Napenda kuwapongeza kwa mkutano huu muhimu wa kuchagua mgombe wa urais, nawatakia mkutano mwema na sisi tunakuja na ajenda ya furaha kwa Watanzania inawezekana,” amesema Prof. Lipumba.

Augustine Mrema, Mwenyekiti wa Chama cha TLP akizungumza katika mkutano huo, ameendelea kusisitiza kwamba chama chake kitamuunga mkono Rais Magufuli katika uchaguzi huo.

“Katika kikao cha Halmashauri Kuu ya TLP ikasema hatuna mbadala wa Dk. Magufuli, tukasema Dk. Magufuli anatosha, sisi hatukutaka kuweka mgombea urais tulichotaka tutafanya kampeni nchi nzima kuhakikisha unachaguliwa,” amesema Mrema.

Aidha, Mrema amekiomba chama cha CCM kihakikishe TLP kinakuwa na wagombea katika kata na majimbo yote.

“Ombi langu kwenu nimeona kwenye mikoa mengine majimbo mengi mnaweka wagombea 30, wanahangaika ili achague mmoja, naomba fursa iliyopatikana , tujipange kuhakikisha kuanzia kata zote tuna mgombea wa TLP na CCM, kwenye majimbo yote,” amesema Mrema.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI Online kwa habari zaidi

error: Content is protected !!