Sunday , 5 May 2024
Home Habari Mchanganyiko Wananchi Rufiji wamwita Samia, wamtupia lawama Mchengerwa
Habari Mchanganyiko

Wananchi Rufiji wamwita Samia, wamtupia lawama Mchengerwa

Mohamed Mchengerwa
Spread the love

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameombwa afike wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani, kwa ajili ya kuwasilikiliza wananchi wenye changamoto sugu zinazodaiwa kutofanyiwa kazi na wasaidizi wake katika maeneo husika. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea).

Inadaiwa kuwa, baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo wamechukua jitihada mbalimbali za kutafuta msaada wa kutatuliwa changamoto zao, lakini si mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, wala Mkuu wa wilaya hiyo, Meja Jenerali, Edward Gowele, aliyeonesha nia ya kuwasaidia.

Kutokana na madai ya kukosa msaada, wawakilishi wa wananchi hao waliokuwa na malalamiko mbalimbali, wameamua kuomba msaada wa vyombo vya habari ili vipaze sauti juu ya kilio chao kwa ajili ya kumfikia mkuu wa nchi, Rais Samia ili aingilie kati wapate haki zao.

Yusuph Omari Mwela, amemuomba Rais Samia aingilie kati mgogoro uliopo kati yao na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ili walipwe fedha zao za fidia.

“Sisi tulikuwa na maeneo yetu tulipewa na mkuu wa wilaya wa enzi hizo, Majaliwa Kassim Majaliwa mnamo 2009 kwa ajili ya kulima, tulikaa miaka 12 baada ya hapo wakaja wanajeshi wakataka kuwapa maeneo wakati kukiwa na mazao yetu ya korosho. Sisi tulikubali tukakubaliana watulipe fidia lakini hadi leo hawajatulipa,” alidai Mwela.

Mwela alidai baada ya kuona hamna dalili za kulipwa fidia zao, waliamua kumtafuta mbunge wao, Mchengerwa bila mafanikio.

“Tumeomba msaada kwa mkuu wa wilaya tumekosa msaada, tumeenda kwa CCM tumekosa msaada, mbunge tumemtafuta kwa muda wa miezi minane hatujamuona hata kuja kufanya mikutano hamna wakati sisi wananchi tunahitaji kuonana naye kwa kuwa tuna matatizo makubwa ili atusaidie,” alisema Mwela.

Masoud Kambangwa, kutoka kikundi cha ujenzi cha Bravo Group, alisema malalamiko yao ni kukamilishiwa malipo ya kazi waliyofanya kujenga shule na vituo vya afya vya wilaya hiyo.

“Sisi ni mafundi ujenzi wa majengo mengi ya serikali, ikiwemo Shule ya Bibititi, Kituo cha Afya Ngorongo, Shule ya sekondari Ngorongo na nyingine mbalimbali lakini hela zetu hatujalipwa. Mbali na kikundi chetu, kuna vikundi vingine kama sita vinadai malipo tukienda kudai tunaambiwa mama Samia hajaleta hela,” alisema Kambangwa na kuongeza:

“Majengo tumeyakabidhi tangu Agosti 2021 na sheria inataka ukikabidhi jengo baada ya miezi mitatu ya uangalizi ulipwe hela yako lakini hatujalipwa hadi leo hii mwaka 2022 unafika ukingoni. Tunamuomba mama Samia atusaidie.”

“mimi malalamiko yangu nilitoa fedha halmashauri ili nipewe kibali cha kuvuna magogo, lakini bila sababu za msingi walinizuia na si hilo tu tuna malalamiko mengi na mama Samia alipokuwa anatokea lini vijana tulisimama barabarani na mabango ili kumfikishia ujumbe lakini baadhi walikamatwa ili wasitaje matatizo yao.”

“Mama tunakuomba uje Rufiji utusikilize mashamba yetu yamechukuliwa na JWTZ lakini tunaambiwa hela ziko kwako wao wanasema wamemaliza uthamini wanadai hela ziko kwako, mwaka huu umepita krosho hatujaokota watoto wanataka kwenda shule mambo magumu tunaomba utusaidie.”

Kutokana na malalamiko hayo, MwanaHALISI lilimtafuta kwa njia ya simu Mchengerwa ambaye ni Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, bila mafanikio na kufanikiwa kumpata Meja Jenerali  Gowele, ambaye alisema malalamiko yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kuhusu wanaodai malipo ya zabuni mbalimbali, Meja Gowele alisema wengi wamelipwa fedha zao na wale wachache waliobaki wanapaswa kufika ofisini kwake ili uhakiki ufanyike kwa ajili ya malipo.

“Hakuna mtu aliyekuja ofisini kwangu kupata msaada akafukuzwa, cha msingi kama wapo wafike ofisini tutawasaidia. Wakija tutakaa na maafisa manunuzi, maafisa ujenzi na mkurugenzi kuangalia namna ya kulipa, anayelipa ni mkurugenzi ila wanakuja kwangu nione mikataba yao ili niwasaidie walipwe,” alisema Meja Gowele.

Kwa wale wanaodai fidia ya maeneo yao yaliyochukuliwa na jeshi, Meja Gowele alisema halmashauri ya Rufiji imeshakamilisha taratibu za fidia na kwamba kwa sasa suala hilo linafanyiwa kazi hazina.

“Wewe unaelewa maana ya kufanyiwa uthamini, ni process lazima iende hazina mwisho waweze kupewa fedha. Malipo tayari yako hazina juzi nimetoka kuongea na mhusika anayeshughulikia kulipa amesema Rufiji watalipwa hivi karibuni kwa kuwa watu wa Kibiti wameshalipwa,”alisema Meja Gowele .

Akizungumzia madai ya wananchi hao kuzuiwa kuvuna korosho zao, Meja Gowele alisema“lazima wapishe jeshi liendelee kufanya kazi ndani ya eneo lile, haiwezekani jeshi lifanye mazoezi halafu watu wanaokota korosho si salama. Hao watalipwa jeshi haliwezi dhurumu mtu ingawa wao yale maeneo hawakukabidhiwa bali walipewa ruhusa ya kulima kwa muda.”

Meja Gowele alisema malalamiko ya Chingambe kunyimwa kibali cha kuvuna magogo licha ya kulipia tangu 2022, yalifanyiwa kazi na kwamba mwananchi huyo aliruhusiwa kuvuna.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Tanzania  yasisitiza kuwa Kituo Kikuu cha Uchimbaji Madini Afrika

Spread the loveTanzania imeendelea kusisitiza adhma yake ya kuwa kituo kikuu cha...

Habari MchanganyikoTangulizi

Kimbunga Hidaya chatikisa Mafia

Spread the loveWAKATI hali ya upepo mkali ikiendelea kushuhudiwa katika baadhi ya...

Habari MchanganyikoTangulizi

Usafiri baharini wasitishwa kukwepa athari za kimbunga Hidaya

Spread the loveUSAFIRI wa baharini umesimamishwa kwa muda ili kukwepa athari za...

Habari Mchanganyiko

RPC Dodoma akabidhiwa bunduki mbili za wahalifu

Spread the love  Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya...

error: Content is protected !!