May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Wanahabari wampongeza Rais Samia

Samia Suluhu Hassani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Spread the love

KLABU ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza(MPC), imempongeza Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuvifungulia vyombo vya habari vilivyoungwa kwa sababu mbalimbali .Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza…(endelea).

Pongezi hizo zimetolewa leo Jumanne tarehe 6 Aprili 2021 na Mwenyekiti wa MPC,  Edwin Soko, muda mfupi baada ya Rais Samia  kuagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  kuvifungulia vyombo vya habari vilifungwa.

Akizungumza katika hafla ya kuapishwa viongozi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Samia  aliiagiza wizara hiyo kusimamia vyombo hivyo pasina kuvibana, huku akitoa wito kwa tasnia hiyo itekeleze majukumu yake kwa kufuata sheria na kanuni.

Soko amesema kuwa, uamuzi huo unalenga kuruhusu vyombo hivyo kufanya kazi zake kwa uhuru.

“MPC inapongeza kwa dhati maamuzi ya Rais Samia, kwani ni maamuzi yanayolenga kuruhusu vyombo vya habari kufanya kazi zake kwenye mazingira rafiki bila vikwazo.

Kitendo kilichofanywa na Rais ni  cha hekima na busara kwa tasnia ya habari hapa nchini, amesikia kilio cha vyombo vya habari kwa muda mrefu” amesema Soko.

Mwenyekiti huyo wa MPC  amesema, vyombo vya habari vikiwa huru vinafanya kazi zake kwenye mawanda mapana ya kuleta maendeleo,  kupitia fikra pevu za misingi ya uandishi wa habari.

“MPC inaamini kuwa, vyombo vya habari sio adui wa Serikali bali ni rafiki wa Serikali kwenye kuhakikisha vinafanya kazi zake kwa weledi na kuibua kasoro mbalimbali zinazoathiri utendaji wake. Ili hatua stahiki zichukulie pamoja na kasoro hizo zifanyiwe kazi na kuleta mabadiliko chanya nchini,” amesema Soko.

Wakati huo huo, Soko ameiomba Serikali ya Rais Samia ifanyie marekebisho kanuni za sheria mbalimbali zinazoongoza taaluma ya habari nchini, ambazo ni vikwazo katika uendeshaji wa tasnia hiyo.

“Hata hivyo MPC inatoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya sheria mbalimbali  zinazo ongoza taaluma ya habari nchini, ikiwemo Sheria ya Huduma ya vyombo vya habari 2016.

Kama ilivyoamriwa na Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki pamoja na sheria nyingine na kanuni zenye ukakasi,” ameomba Soko.

Aidha, Soko ametoa rai kwa Waandishi habari nchini kufanya kazi zao katika misingi ya taaluma ili kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Taifa.

Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyofungwa ni Magazeti ya MwanaHALISI, Mawio na Mseto, yanayochapishwa na Kampuni ya HaliHalisi Publishers. Na Gazeti la Tanzania Daima.

error: Content is protected !!