Sunday , 19 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Mpina mwiba CCM, ahofia kuzibwa mdomo

Luhaga Mpina
Spread the love

WAKATI Chama cha Mapinduzi (CCM), kikijinasibu kuwa kinara wa demokrasia nchini, kimemuweka kwenye kitanzi mbunge wake wa Kisesa Luhaga Mpina kutokana na michango yake anayoitoa bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Tayari vikao vya kamati ya maadili ya CCM ngazi ya Wilaya na Mkoa vimejadili mwenendo wa mbunge huyo ndani na nje ya Bunge na kuna uwezekano mkubwa suala lake likafikishwa kwenye vikao vya juu kwa ajili ya uamuzi zaidi.

Mpina anatuhumiwa kuendesha siasa zinazokivuruga chama na kuibua hoja bungeni ambazo hajatumwa na wananchi waliomchagua na hawatembelei waliomchagua ili kujua kero zao na kushirikiana nao kutatua kero zinazowakabili.

Mbunge huyo, wiki iliyopita akiwa bungeni aliibua hoja ya kutaka iundwe tume huru ya uchunguzi juu ya kifo cha Rais John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu ya umeme wa moyo uliokuwa ukimsumbua.

Hata hivyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alimtaka Mpina aeleze ajenda iliyojificha nyuma yake badala ya kutoa hoja  zinazolenga kumhujumu Rais Samia na kuwadharau watendaji wa Serikali.

Hii ni mara ya pili kwa Mpina kubanwa. Mara ya kwanza ilikuwa Januari 25 mwaka huu alipohojiwa kwa madai haonekani jimboni, hafanyi mikutano ya wananchi, hasikilizi kero za wananchi na kazi yake kulumbana na wenzake huko na kukifanya chama kififie huku.

Katika mikutano ya Bunge, Mpina amekuwa mwiba kwa mawaziri bungeni ambapo miongoni mwa waliokumbana na hoja zake zinazoibua mijadala ni Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Hussein Bashe (Kilimo), Dk Mwigulu Nchemba (Fedha) na January Makamba aliyekuwa Nishati (sasa yupo Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa).

Safari hii hoja ya Mpina ilitokana na mahojiano aliyoyafanya Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Venance Mabeyo na chombo kimoja cha habari ambapo alisema baada ya kifo cha Magufuli kulikuwa na ugumu wa kutangaza mrithi wake na kuapishwa kwake.

Bashiru Ally

Kauli hiyo ya Mabeyo ilirejesha upya mjadala uliokuwapo kabla na baada ya kifo cha Magufuli ambapo baadhi ya watu walikuwa na wasiwasi kutokana na taarifa za ugonjwa na kulazwa kwakwe kutowekwa wazi kama inavyofanyika kwa viongozi wengine waliowahi kushikilia wadhifa huo.

Mahojiano hayo pia yalifufua tetesi zilizoenea wakati huo kuwa baadhi ya viongozi hawakutaka Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, aapishwe kushika wadhifa huo kama Katiba inavyoelekeza.

MwanaHALISI limedokezwa kuwa Mpina amekalia kuti kavu si tu kwa sababu ya hoja zake hizo bali pia kutoelewana na viongozi wa wilaya na mkoa ambao kila kukicha wanamlaumu kwa kutowajibika ipasavyo na kukipa chama wakati mgumu mbele ya wananchi.

Siku chache zilizopita Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu Shamsa Seif Mohamed alimtaka Mpina kuacha siasa za maji taka za kuhoji sababu za kifo cha Magufuli bali ashughulike na matatizo yanayowakabili wananchi.

Shamsa alisema kila binadamu ana siku yake ya kuzaliwa na kifo hivyo haoni sababu za Mpina kujificha kwenye hoja ya kifo cha Magufuli wakati wananchi wake wana shida mbalimbali na wanahitaji akawasemee bungeni.

“Sio sisi wala wananchi wake waliomtuma aende akazungumzie hoja hizo. Kwanza wananchi wanalalamika hawamuoni jimboni kila kukicha yeye kwenye mitandao na kutoa hoja wasizomtuma, aache siasa za maji taka,” alisema

Hata hivyo hatua ya CCM kumweka Mpina kwenye mbinyo inatajwa inaingilia uhuru wa wabunge kuchangia masuala mbalimbali ndani ya Bunge ambako wana kinga na hawapawi kuingiliwa na muhimili mwingine au mtu yoyote.

Wakati hali ikionekana kumwia ngumu Mpina, juzi Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Amos Makalla aliwaambia wahariri jijini Dodoma kuwa chama chake kitaendelea kuwa kinara wa demokrasia na kutoa uhuru wa watu kujielezea pamoja na uhuru wa habari.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Mehrab Jabira ameliambia MwanaHALISI kuwa wanachofanya CCM ni kuwatisha wabunge wao hasa wanaoonekana wakali kwenye hoja zinazotoa wakati mgumu kwa Serikali na viongozi wake.

“Sioni sababu ya CCM kukaa vikao vya kumjadili Mpina, kama hafai si hatoweza kupita kwenye mchujo wa wanaotaka ubunge utakaofanyika mwakani? Hii si afya kwa demokrasia,” alisema

“Hivi mara ngapi CCM inafuatilia hoja zinazotolewa na wabunge wake bungeni ndizo wanazotumwa na wananchi? Huyu Mpina wakati akipima urefu wa samaki na kuchoma nyavu za kuvulia Samaki si walimshangilia? Sasa wavumilie mwiba wao,” alisema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Hafsa Shamori mwanafunzi wa chuo kimoja jijini Dodoma, aliliambia MwanaHALISI kuwa CCM wanapaswa kuonesha mfano wa kuvumiliana kwa vitendo kama wanavyohubiri kila siku badala ya kumshughulikia Mpina

“Kuna tatizo gani kwa mbunge mmoja kati ya 300 kuwa na hoja au mawazo tofauti na wenzake? Rais Samia anahubiri maridhiano na kuruhusu mijadala ya wazi, sasa huyu Mpina ana athari gani katika siasa za Taifa?”

Alisema hoja ya kutaka uchunguzi wa kifo cha Magufuli si mpya wala si ajabu kutoka na matamko ya watu mbalimbali akiwemo Mkuu wa majeshi mstaafu, Venance Mabeyo.

“Mabeyo alituambia wakati Magufuli anakufa kulikuwa na wakuu wa usalama watatu, hapa kuna maswali kwa nini mkewe hakuwepo? Kwa nini walianza kutaarifiwa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Bashiru Ali na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa waliokuwa Dodoma wakati Makamu wa Rais alikuwapo Tanga na akachelewa kufika Dar es Salaam kuliko wenzake?”

Alisema njia nzuri ya kuua hoja ni kuipatia majibu sahihi badala ya kutumia nguvu kuizima au kukabiliana na mtoa hoja kama wanavyofanya kwa Mpina

Naye mwanaharakati wa kutetea uhuru wa Bunge na kujieleza, Joyce Magayane alisema ni vema viongozi na watendaji wa vyama vya siasa wakaacha kuwatisha makada wao wenye mitazamo tofauti kama alivyofanya Mpina.

“Haya mambo tunayaona si kwa CCM pekee bali hata kwenye vyama vya upinzani, yaani wabunge wenye kukosoa au kuhoji mambo fulani, badala ya kupatiwa majibu sahihi wanapewa vitisho. Hii haisaidii sana kwa kuwa jamii inabaki kuwa na kiu ya kutaka majibu, hoja ijibiwe kwa hoja si nguvu, matusi au kebehi,” alisema

MwanaHALISI liliwasiliana na Mpina kutaka kujua msimamo wake juu ya kinachoendelea ndani na nje ya Bunge ambapo hakuwa tayari kuzielezea zaidi ya kudai kuwa anafanya kazi kulingana na taratibu zilizopo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

CCM yamteua Pele kuwa mgombea ubunge Kwahani

Spread the loveKamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Ujenzi kituo cha kupoza umeme Chalinze wafikia asilimia 93.7

Spread the loveKamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza...

Habari MchanganyikoHabari za SiasaTangulizi

Wakili Mwabukusi anusurika kufungiwa, asema hatarudi nyuma

Spread the loveWAKILI Boniface Mwabukusi amesema kuwa hatorudi nyuma kuwatetea Watanzania na...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

RC Chongolo atangaza ‘vita’ kwa wanaovusha wageni kinyemela

Spread the loveKATIKA kulinda usalama wa nchi kupitia mpaka wa Songwe, Mkuu...

error: Content is protected !!