Friday , 24 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?
Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia ni Mzanzibari: Shida Iko Wapi?

Spread the love

TAIFA linakabiliwa na upungufu wa fikra sahihi. Upungufu huu unaonekana wazi kwa viongozi wetu lakini kwa kuwa viongozi wetu ni kioo cha wananchi, hili tatizo laweza kuwa kubwa zaidi katika taifa zima.

Ukiona ufinyu wa fikra za baadhi ya viongozi inabidi ujiulize kama huyu ndiye alionekana ni bora, je waliobaki katika mchujo wa kumpata huyu, wana hali gani.

Katika ngazi ya baraza la mawaziri na wateule wengine wanaoteuliwa na mamlaka ya juu zaidi, bado hali inatia shaka. Mtu unajiuliza, hivi waziri huyu ndiye aliyeonekana anafaa kati ya wote? Kama maswali haya hayana maana basi uteuzi unaofanywa na rais ni kwa manufaa na mapenzi ya rais na si kwa manufaa ya wananchi.

Maneno ya Profesa PLO Lumumba yanapata uhalali hapa kwamba wenye maono hawana nafasi na wenye nafasi hawana maono.Ukiona hali hii ujue kuna kosa la kiufundi linatokea.

Viongozi wetu wanatenda kwanza na kufikiri baadaye. Vitendo vinatangulia mbele na nadharia inafuata nyuma badala ya nadharia kuongoza vitendo. Kwa hiyo, anaweza kuua kisha akatengeneza nadharia ya kuua, kuliko kwanza kutengeneza nadharia itakamuongoza kuua.

Ndiyo maana haishangazi kuona baadhi ya teuzi kama ule wa kumteua mtu kama Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda na kumkabidhi kipande cha ardhi na kumtangaza kuwa ndiye rais wa mkoa. Sifa pekee aliyo nayo Makonda ni kutenda bila kufikiria madhara na hilo linampa uhalali mbele ya mteuzi wake.

Wiki hii kumeibuka mjadala mkali kuhusu matamshi aliyoyatamka Tundu Lisu katika mkutano wa hadhara huko mkoani Manyara. Bila kunukuu moja kwa moja alichosema Lisu, lakini kilichoibua hisia ni kumwita Rais Samia kuwa ni Mzanzibari anayedaiwa kuuza raslimali za Watanganyika.

Kinachoonekana kukera watu si tuhuma za kuuza bandari na ardhi bali Tundu Lisu kumwita Rais Samia kuwa ni Mzanzibari. Kumwita mtu anayetoka Zanzibar kuwa Mzanzibari kuna ubaya gani? Kwani Uzanzibari ni kabila?

Imetamkwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuwa endapo rais atatokea upande mmoja wa Muungano (Zanzibar au Tanganyika), basi Makamu wake atatoka upande wa pili. Kwa maana nyingine, hatuwezi kuwa na rais na makamu kutoka upande mmoja.

Na ili kuwatofautisha hawa, sharti ni mmoja atambulike kama Mzanzibari na mwingine Mtanganyika (siyo Mtanzania kwa sababu hata Mzanzibari ni Mtanzania). Hili hata Rais Samia analijua na analipenda. Yeye ni Mzanzibari kamili. Si tusi, si kejeli wala kashfa kwake.

Aidha, sehemu ya pili ya Katiba ya Zanzibar, Ibara ya 6 (1) inasema, “Kutakuwa na Mzanzibari ambaye upatikanaji wake, upoteaji wake ma urudishwaji wake atakuwa kama alivyoainishwa katika Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi.”

Ibara ya 6 (2) inasema, “Kila Mzanzibari, kwa misingi ya Katiba hii, ataweza kufaidi haki na fursa zote anazostahiki Mzanzibari, na atapaswa kutekeleza wajibu, na jukumu na dhamana za Mzanzibari kama ilivyo kwenye Katiba hii au kwenye Sheria iliyotungwa na Barzaza la Wawakilishi.”

Ndiyo, Watanzania hawakuzoea kuona wala kusikia mkuu wa nchi anakosolewa hadharani. Kwa hiyo kumkosoa, kumkejeri, kumbagaza ni utamaduni mpya ambao watu wengi wanapata shida kuukubali.

Lakini wakati huo huo, Watanzania wamezoea kuona kiongozi wa umma akijali mali za umma, akikazana kuongeza raslimali na si kuuza, akitetea wazawa kuliko wageni. Katika habari ya raslimali, Watanzania wangetamani anayetafuta masoko na raslimali nje kuliko kwenda kutafuta wanunuzi wa raslimali zetu za asili.

Kwa hiyo maneno aliyoyasema Tundu Lisu kwa kumwita rais Samia kuwa ni Mzanzibari ni ya kweli na yenye kumpa heshima na haki yake. Rejea Sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi Sheria Na. 2 ya mwaka 2002 kwenye kifungu cha 5.

Ninachoona kuwa kinaleta shida katika matamshi haya kimejificha katika maeneo matatu.

Eneo la kwanza ni ukweli kuwa Rais Samia ni wa pili kutoka Zanzibar kuongoza Jamhuri. Kwa kuwa na rais wa muungano atokaye Zanzibari ni jambo ambalo halijazoeleka. Wangekuwepo wengi waliomtangulia au zingekuwepo zamu, matamshi haya yangekuwa ya kawaida.

Eneo la pili mazoea ya watu wa Zanzibar kupenda kujitambulisha kama Wazanzibari kuliko Watanzania. Ndugu zetu hao wanasisitiza wao ni Wazanzibari kwanza kabla ya kuwa Watanzania. Msisitizo huo unajenga taswira ya kujitenga na Watanganyika. Inapotokea Mtanganyika kuwaita ni Wazanzibari, badala ya kufurahi wanachukia. Wanataka wajiite, ila wasiitwe Wazanzibari.

Eneo la tatu ni kukosekana kwa hoja yenye nguvu kujibu hoja za wanaohoji Muungano, uuzwaji wa bandari na ardhi za upande wa Tanganyika. Chama tawala kimelemaa kwa muda mrefu kwa kujibu hoja wakitumia majeshi na raslimali za serikali.

Haishangazi kuona maneno ya Lissu yakijibiwa ndani ya Bunge kwa kulitaka Bunge kumtenga Lissu na chama chake. Inapofika hatua ya unaoitwa ubaguzi kujibiwa kwa kutumia ubaguzi, fikra pevu na muhimu zinakuwa zimeisha.

Ni sahihi kumuuliza Mheshimiwa sana Nape Nnauye ikiwa Rais Samia si Mzanzibari ni nani? Na kama si Mzanzibari basi katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imevunjwa tayari maana Makamu wa Rais Dk. Philip Isidory Mpango ni Mtanganyika wa Kigoma.

Na kama Rais Samia ni Mzanzibari, na ni kweli, tatizo liko wapi kwa Lissu kumwita ni Mzanzibari? Tangu lini mtu kuwa Mzanzibari limekuwa tusi?

Ikumbukwe majuzi ulizuka mjadala kutokana na kauli ya Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali Venance Mabeyo, kwamba wakati wa kifo cha Rais John Magufuli, wapo watu waliomwendea mmoja wa marais wastaafu kupendekeza kwamba, kwa kuwa rais aliyekufa alikuwa wa Bara (Tanganyika) na makamu wake ni Mzanzibari, basi mtu wa kushika nafasi ya marehemu awe wa kutoka Bara na makamu (Samia wakati huo) abakie kuwa ni makamu.

Siwezi kushangaa ikiwa siku moja tutaambiwa kuwa mawaziri wanaoona Lissu amekosea ndio hao hao waliotaka Rais Samia abakie kuwa Makamu kwa kuwa ni Mzanzibari. Kutoa povu bila hoja ni dalili mbaya na hatia moyoni. Wanauunga mkono Muungano kwa midomo yao lakini mioyoni hawautaki. Makala hii imeandaliwa na Kondo Tutindaga.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Biteko awataka makatibu mahsusi kujiendeleza, kuwa kielelezi cha huduma bora

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyookoa walemavu dhidi ya dhana potofu

Spread the loveMKOA wa Geita ni mmoja wa mikoa ya Kanda ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

error: Content is protected !!