UMOJA wa Vijana wa CCM (UVCCM) tawi la Mlowo, jana Jumapili wameadhimisha miaka 62 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kuendesha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kuruka kamba na kukimbiza kuku huku washindi wakipata zawadi mbalimbali. Anaripoti Ibrahim Yassin, Songwe.
Mwenyekiti wa UVCCM kata ya Mlowo, Bernad Nkwira amesema maadhimisho hayo yaliyonogeshwa na michezo hiyo ambapo waliokimbiza kuku walifanikiwa kuondoka nazo na mchezo wa mpira wa miguu mshindi alipata mbuzi.
Amesema lengo la kuendesha michezo ni kutoa hamasa kwa vijana ili wapende michezo ambapo mshindi kati ya timu ya Mji na Forest timu ya Maji ilishinda goli 3 -0 dhidi ya Forest na kupewa zawadi ya mbuzi na timu ya Forest ikipata zawadi ya Sh 30,000.
Katibu mjumbe wa mkutano mkuu CCM mkoani Songwe, Imani Banda ameupongeza umoja huo kwa kuendesha tukio hilo kwani mbali na kuendesha michezo, wamepanda miti 3,000, kufanya harambee na kukusanya Sh milioni 1.3 za kujenga ofisi.
Ametoa rai yake kwa vijana hao kuwa ili umoja wao usonge mbele waache makundi ili wafike mbali kimaendeleo.
Diwani wa kata hiyo, Jackson Mwanda amesema tukio walilofanya vijana hao kwa kuadhimisha miaka 62 ya uhuru kwa kupanda miti, ni jambo muhimu na anajivunia kuwa na vijana wenye upeo kama huo.
Leave a comment