VYAMA vya siasa vya upinzani nchini Sri Lanka vimekutana jana tarehe 10 Julai, 2022 kukubaliana kuhusu serikali mpya siku moja baada ya rais wa nchi hiyo na Waziri mkuu kutangaza kuachia madaraka. Inaripoti Mitandao ya kimataifa … (endelea).
Mbunge wa upinzani Mathiaparanan Sumathiran amesema vyama vyote vya upinzani kwa pamoja vinaweza kupata kwa urahisi wanachama 113 wanaohitajika kuonyesha wingi wa viti bungeni, ambapo watamuomba Rais wa nchi hiyo, Gotabaya Rajapaksa kutangaza serikali mpya kisha ajiuzulu.
Waziri Mkuu, Ranil Wickremesinghe amesema ataondoka madarakani baada ya serikali mpya kutangazwa jambo ambalo pia lilithibitishwa na Spika wa Bunge ambaye alisema Rajapaksa atajiuzulu Jumatano.
Shinikizo dhidi ya viongozi hao wawili lilikuwa limeongezeka baada ya mdororo wa uchumi uliosababisha uhaba mkubwa wa bidhaa muhimu, na kuwaacha watu wakitatizika kupata chakula, mafuta na mahitaji mengine.
Baada ya rais na Waziri mkuu kujiuzulu, Spika Mahinda Yapa Abeywardena atachukua usukani kama rais wa muda, kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo.
Hayo yanajiri wakati waandamanaji wameendelea kubaki nyumbani kwa Rais Rajapaksa, na kwenye ofisi yake pamoja na makaazi ya Waziri mkuu, wakisema wataendelea kubaki hapo hadi pale viongozi hao watakapojiondoa rasmi madarakani.
Leave a comment