Taarifa kutoka makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, mkoani Dar es Salaam zinasema, Mdee amepanga kujimilikisha Bawacha, kupitia uchaguzi wake, unaotarajiwa kufanyika 7 Machi mwaka huu.
Uchaguzi mkuu wa Bawacha, unalenga kujaza nafasi zilizoachwa wazi na Mdee na wenzake, ambao walifukuzwa uanachama wa Chadema, Novemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa vyanzo vya taarifa, Mdee ambaye alibebwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, mithili ya “mtoto wa mwisho,” anapanga mkakati kuhakikisha kuwa viongozi wote watakaochaguliwa, ni “wafuasi wake.”
Kamati Kuu (CC) ya Chadema, iliyokutana Novemba mwaka jana, iliwafukuza uanachama Mdee na wenzake 18, kufuatia kupatikana na hatia ya usaliti, kuhujumu chama na kwenda bungeni kujiapisha kuwa wabunge.

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni pamoja na waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega na aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha), Nusrat Hanje.
Wengine, ni aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha (Bara), Hawa Mwaifunga; aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha (Bara), Jesca Kishoa; aliyekuwa katibu mwenezi wa baraza hilo, Agnesta Lambat na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.
Katika orodha hiyo, wamo pia aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Asia Mwadin Mohamed; Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.
Genge hilo lililopachikwa jina la Covid 19, limewasilisha rufaa Baraza Kuu (BKT), kupinga maamuzi hayo.
Hata hivyo, pamoja na Mdee na wenzake, kufutwa uanachama na wenyewe kupokea adhabu hiyo kwa kukata rufaa, bado wameruhusiwa kuendelea kuwa wabunge, kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Vyanzo vya taarifa vinasema, miongoni mwa mikakati aliojiwekea Mdee na genge lake, ni kuhakikisha Bawacha ambayo inaushawishi mkubwa kwa wanawake, inashindwa kutekeleza majukumu yake ya uhamasishaji kwa chama.
Amesema, kuna taarifa za kina kuwa Mdee na wenzake, wameweka wagombea wao na kwamba wanalenga kugharamia baadhi ya gharama za uchaguzi.
Miongoni mwa wanaotajwa kumrithi Mdee, ni mfuasi wake mmoja, aliyewahi kumleta makao makuu ya Bawacha na kumfanya msaidizi wake.
Mfuasi huyo wa Mdee, amechukua fomu ya kuwania nafasi ya katibu mkuu. Alikuwa mmoja wa wafuasi wa Mdee, waliohudhuria msiba wa bibi yake, miezi miwili iliyopita.
Leave a comment