Mkuu wa mkoa wa Singida, Peter Serukamba amewaagiza viongozi na watendaji mkoani humo kuhakikisha kaya zote zinakuwa na vyoo bora na kuchukua hatua kali kwa mujibu wa sheria dhidi ya kaya ambazo hazina vyoo ili kukabiliana na ugonjwa wa mlipuko wa kuhara na kipindupindu. Anaripoti Danson Kaijage, Singida… (endelea).
Akizungumza jana Jumanne katika kikao cha Kamati ya Afya ya Msingi cha mkoa, Serukamba amesema maradhi hayo husababishwa na mazingira ya uchafu.
Amesema jamii inapaswa kuhakikisha mazingira yote yanayowazunguka yanakuwa safi kwa lengo la kudhibiti magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu ili kisiwepo kabisa Mkoani Singida.
Aidha, Serukamba amewasisitiza wakuu wa wilaya wote mkoani humo kuhakikisha maeneo yote ya kaya, taasisi za umma, mashirika ya dini, masoko, stendi za mabasi, mashuleni, kwenye nyumba za ibada na mikusanyiko rasmi na isiyo rasmi, kutumia vifaa vya kunawia mikono, maji safi na sabuni ili kujikinga na maradhi hayo.
Amewasisitiza Wakuu hao wa Wilaya kwa kushirikiana na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha maeneo yote ya kupikia na kuuzia vyakula yanakaguliwa na wataalamu wa Afya ili kuwa safi muda wote.

Hata hivyo, Serukamba amewaagiza Wakurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (SUWASA), Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Mkoa Singida (RUWASA) pamoja na Mkurugenzi wa Bodi Bonde la Kati kuhakikisha wanachukuwa sampuli za maji na kutibu visima vifupi, virefu na kusambaza maji safi na salama kwa watumiaji maji hayo ili kujikinga na ugonjwa huo wa kuharisha na kutapika.
Katika hatua nyingine, amewahimiza Wakurugenzi wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha maeneo yote ya minada na masoko yanakuwa na vyoo bora ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo wa mlipuko wa kuharisha na kutapika hasa katika Mkoa wa Singida.
Leave a comment