August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali kuajiri walimu 10,000 upungufu ukiwa 175,701

Moja ya shule za kata nchini

Spread the love

 

WAKATI upungufu wa walimu wa msingi na sekondari nchini ukiwa ni 175,701, Serikali imeomba kibali cha kuajiri walimu 10,000 pekee, 5,000 kati yao wakiwa wa sekondari na 5,000 wa shule za msingi na awali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Hotuba ya Wizara ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI iliyowasilishwa leo Alhamisi tarehe 14 Aprili, 2022, na Waziri Innocent Bashungwa imebainisha kuwa Shule za Msingi zina upungufu wa walimu 100,958 huku Sekondari zikiwa na upungufu wa walimu 74,743.

Bashungwa amesema takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kuna jumla ya Shule za Msingi 17,034 zenye jumla ya wanafunzi 12,033,594 wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 60,825.

“Hadi Machi, 2022 mahitaji ya walimu katika Shule za Msingi ni 274,549 kwa kutumia uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 60, walimu waliopo ni 173,591, upungufu ni walimu 100,958 sawa na asimilia 36.77 ya mahitaji,” ameeleza Bashungwa katika hotuba hiyo.

Aidha, amesema mahitaji ya walimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa Shule za Msingi ni ni walimu 3,631, waliopo ni 1,517 na upungufu ni walimu 2,143 sawa na asilimia 59.02 ya mahitaji.

Waziri wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa

Kwa upande wa Shule za Sekondari amesema mahitaji ya walimu ni 159,443 waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 74,743 sawa na asilimia 46.87.

Hali hiyo ni kutokana na uwepo wa shule za Sekondari 4,175 zenye jumla ya wanafunzi 2,607,142 wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum 11,106.

Ili kukabiliana na upungufu huo amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeomba kibali cha kuajiri walimu 10,000 wa Shule za Msingi na Sekondari.

“Kati ya hao, walimu 5,000 ni kwa ajili ya shule za Awali na Msingi na 5,000 kwa ajili ya Shule za Sekondari,” amesema Bashungwa.

error: Content is protected !!