November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Selasini, wenzie wakaidi amri ya Mahakama, wafanya mkutano

Spread the love

 

LICHA ya Mahakama Kuu Masjala ya Dar es Salaam kuweka amri ya zuio la muda la kutofanyika kwa mikutano ya Chama cha NCCR-Mageuzi, wanachama wa chama hicho upande wa unaomuunga mkono, aliyekuwa katibu mkuu, Martha Chiomba leo tarehe 24 2022 unafanya Mkutano jijini Dodoma. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Mkutano huo uliotajwa kuwa wa dharura, unafanyika kwenye ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma kwa lengo la kujadili masuala ya mgogoro ndani ya chama hicho.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Joseph Selasini amewaeleza waandishi wa habari kwamba katiba ya chama hicho inasema kutakuwa na mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano.

Amedai panapotokea dharura katiba hiyo inaruhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura.

“Pamoja na mambo mengine, mkutano mkuu utakuja kujadili na kuamua kuhusu kauli kuwa chama kina makundi mawili,” amesema.

Hayo yanajiri wakati tarehe 7 Septemba, 2022 Jaji Edwin Kakolaki alitoa amri ya zuio la mikutano wowote ndani ya chama utakaoratibiwa au kuitishwa na Chiomba na Joseph Selasini mpaka pale shauri la msingi litakaposikilizwa.

Joseph Selasini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi

Shauri la msingi ni maombi namba 150 ya mwaka 2022 yaliyofunguliwa na Angelina Mutahiwa Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bara, na Hemedi Kanoni mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Maombi yaliyofunguliwa tarehe 6 Septemba 2022 yaliomba mahakama iwazuie Selasani, Chiomba na wenzao sita kutojihusisha na kuratibu shughuli zote za chama hicho.

Wengine waliozuiliwa na amri hiyo ni Haji Ambar Khamis, Ameir Mshindani Ali, Susanne Masele, Beati Mpitabakana, Martin Mng’ong’o, Ramadhan Manyeko, na Hassan Ruhwanya.

Licha ya Jaji Kakolaki kuamua kusimamisha shauri hilo kwa ajili ya kusubiri kuthibitishwa kwa wajumbe wa Bodi ya wadhamini tarehe 15 Septemba mpaka tarehe 3 Oktoba hakuna pahala popote kwenye uamuzi wake alipoeleza kutengua amri ya zuio la mikutano.

Mkutano huo unaofanyika leo Dodoma, ulitanguliwa na Vikao vya Halmashauri Kuu vilivyofanyika tangu tarehe 22 Septemba 2022 na kwamba miongoni mwa ajenda ni kumjadili Mwenyekiti James Mbatia.

error: Content is protected !!