Friday , 17 May 2024
Home Kitengo Biashara Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani
BiasharaHabari Mchanganyiko

Equity Bank yaendelea kusotea mabilioni ya fedha mahakama rufani

Spread the love

BENKI za Equity ya Tanzania na Kenya, zimeendelea kupambana mahakamani kwa ajili ya kudai haki yake ya kulipwa mabilioni ya fedha, inazodai kuwa kampuni mbili za nchini zimegoma kulipa. Anaripoti mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).

Ni baada ya rufaa iliyokata kwenye Mahakama ya Rufaa dhidi ya kampuni mbili za nchini, kukwama kusikilizwa kutokana na hukumu wanayoipinga kuwa na kasoro. Katika rufaa hiyo benki hizo zinabishania malipo ya malipo ya mkopo wa Dola za Marekani 16,275,000.

Rufaa hiyo iliyofunguliwa na benki hizo, dhidi ya kampuni za Nas Hauliers Limited, Everest Freight Limited na Tanga Petroleum, ilipangwa kusikilizwa Jumanne iliyopita, lakini mahakama iliahirisha hadi tarehe nyingine itakayopangwa, kwa ajili ya majaji wanaoisikiliza kutoa uamuzi kuhusu kasoro hizo.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, linaloongoza na Jaji Rehema Mkuye, akishirikiana na Jaji Abraham Mwampashi na Jaji Zainabu Muruke, linatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya rufaa hiyo kama iendelee au itupiliwe mbali, baada ya kutoa uamuzi dhidi ya hoja zilizotolewa na mawakili wa pande zote mbili kuhusu kasoro hizo.

Kasoro zilizobainika mahakamani hapo ni uwepo wa tofauti kati ya wadaawa wanaotajwa kwenye hukumu inayokatiwa rufaa, notisi ya rufaa na hati ya sababu za rufaa, ambazo ziliwasilishwa mahakamani hapo.

Mahakama ilibainisha kuwa, waliokuwa notisi ya rufaa na ile ya sababu za rufaa zinaonesha kuwa wakata rufaa ni wawili, yaani benki za Equity na wajibu rufaa ni 11, wakati katika hukumu inayokatiwa hukumu inaonesha wadai ambao ni wajibu rufaa walikuwa watatu.

Kufuatia dosari hizo, mahakama ilisema  kwenye notisi ya rufaa na ile ya sababu za rufaa kuna wadaawa wameongezeka ambao kwenye hukumu inayokatiwa rufaa hawapo na ikawahoji mawakili wa pande zote kama notisi hiyo ya rufaa na ya sababu za rufaa ziko sawa kuwepo mahakamani.

Wadaawa hao wanaoonekana kuongezeka kwenye rufaa, ni baadhi ya wakurugenzi wa kampuni hizo, ambao waliingizwa kwenye kesi na kujumuishwa kama wadaiwa kwenye madai kinzani ya benki hizo.

Mawakili wanaozitetea benki za Equity, ambao ni Mpaya Kamara na Timon Vitalis, walikiri kuwapo kwa tofauti hiyo lakini wakasema kuwa wadaawa hao wametajwa ndani ya hukumu hiyo kuanzia ukurasa wa 45 na 59 wa hukumu.

Hivyo Kamara alidai notisi hiyo ya rufaa na hati ya sababu za rufaa hazina kasoro, ila kama ni kasoro basi itakuwa kwenye hukumu kwa kutokuwajata juu kabisa wadaawa hao walioongezeka, lakini akadai kuwa hiyo kasoro ndogo ambayo haiathiri haki za upande wowote kwani haliendi kwenye mzizi wa kesi

Wakili anayezitetea kampuni hizo, ambazo ndio wajibu rufaa pamoja na wakurugenzi wake, Frank Mwalongo naye alidai kuwa kwa kuwa wadaawa hao (wakurugenzi), wametajwa ndani ya hukumu hiyo, hivyo naye haoni kama kuna shida.

Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa tarehe 22 Mei 2019, kampuni hizo ziliingia makubaliano na Equity Bank ya Kenya,  ili kuzitolea hati ya udhamini wa mkopo wa Dola  16,275,000, kutoka kampuni ya Lamar Commodity Trading DMCC, ya Dubai kupitia kampuni ya  Numora Trading PTE Limited.

Kampuni hizo pia zilitoa hati za mali zake mbalimbali kama dhamana ya kudhaminiwa kupata mkopo huo, ambazo zilitunzwa na Equity Tanzania kama wakala wa Equity Kenya. Kampuni hizo zilishindwa kulipa mkopo huo, badala yake Equity Kenya kama mdhamini ikalazimika kuulipa kisha ikazidai kampuni hizo zilipe deni hilo.

Hata hivyo, baadaye kampuni hizo zilizifungulia kesi dhidi ya benki za Equity Tanzania na Equity Kenya zikidai zirejeshewe hati za mali zake zilizoziweka kama dhamana ya kudhaminiwa na kupata mkopo huo.

Kampuni hizo pamoja na mambo mengine zilidai kuwa mkopo huo wa Dola 16.27 milioni, kutoka Lamar/Numora haukuwa na udhamini wa Equity Kenya, kwa madai kuwa hati yake ya udhamini ilikuwa na kasoro. Pia zilidai kuwa zilishalipa mkopo huo na hivyo benki hizo hazina haki ya kuzidai deni lolote

Kufuatia kesi hiyo, benki hizo nazo zilifungua madai kinzani dhidi ya kampuni hizo na wakurugenzi wake, zikidai kulipwa pesa hizo ambazo Equity Kenya ilizilipia deni la mkopo baada ya kushindwa kulipa.

Katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Deo Nangela Aprili 19, 2023, ilitupilia mbali madai kinzani ya benki hizo akieleza kuwa zimeshindwa kuthibitisha madai yake na akazipa ushindi kampuni hizo akieleza kuwa zimeweza kuthibitisha madai yake kuwa zilishalipa mkopo huo na benki hazina haki kuzidai.

Jaji Nangela aliaamuru kampuni hizo zirejeshewe hati zake zote za mali zilizokuwa zinashikiliwa na Equity Tanzania dhamana ya mkopo, ndipo benki hizo zikakata rufaa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Udhibiti wa serikali wakera asasi za kiraia

Spread the loveBaadhi ya wadau wa demokrasia na viongozi wa asasi za...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Nape aomba bajeti ‘kiduchu’ kwa mwaka 2024/25

Spread the loveWaziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Seneta: Wanasiasa hawasaidii mchakato wa Katiba mpya

Spread the loveSeneta wa jimbo la Busia, nchini Kenya, Okiya Okoiti Andrew...

Habari Mchanganyiko

Wananchi washauriwa kuongeza uelewa wa kujikinga na majanga

Spread the love WITO umetolewa kwa wananchi kuongeza uelewa na utayari kabla...

error: Content is protected !!