NAIBU Rais wa Kenya, William Ruto amekubaliana na ombi la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini humo la kumpatanisha na Rais Uhuru Kenyatta. Anaripoti Patricia Kighono – TUDARCo … (endelea).
Kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la nchini humo, mazungumzo ya Ruto na viongozi hao wa kidini yalifanyika nyumbani kwake eneo la Karen jijini Nairobi.
Ruto amesema yuko tayari na ana utashi wa kukutana na Rais Kenyatta. Pia amesema uhasama baina yake na rais ulisababishwa na ‘watu kutoka nje’ ambao walitaka kunufaika na serikali ambayo hawakuiunda.
Amesema makubaliano ya Machi 2018 yanayofahamika kama ‘handshak’ baina ya kiongozi wa chama cha upinzani cha ODM, Raila Odinga na Rais Kenyatta yalikuwa chanzo.
“Kuna watu tu wanafki, walikuja na kusema huyu Naibu Rais tumuweke kando kwanza, lakini mimi niko tayari wakati wowote bila masharti kukutana na Rais Uhuru,” amenukuliwa Ruto.
Mzozo baridi umekuwa ukiendelea baina ya kambi ya Rais Uhuru Kenyatta na ile ya Naibu Rais William Ruto baada ya makubaliano baina ya Rais Kenyatta na kiongozi mkongwe wa upinzani yaliyoitwa ‘Handshake’.
Upande wa Rais Kenyatta unadai kuwa ‘handshake’ ilihusu makubaliano ya kurejesha umoja miongoni mwa Wakenya na hivyo kukomesha ghasia za kikabila zinazoibuka hususani kila baada ya uchaguzi.
Hata hivyo, Ruto anadai kuwa hakuhusishwa katika makubaliano hayo, na amekuwa akitengwa na Kenyatta katika masuala mbalimbali ya kitaifa baada ya ‘Handshake.’
Leave a comment