WAKATI kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini Kenya zikiendelea kupamba moto, mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi huo, Raila Odinga kutoka Chama cha ODM, ameachia kibao kinachokwenda kwa jina ‘Fire’, yaani moto. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Odinga ambaye ameshirikishwa na msanii Kelvin Kionko maarufu nchini humo kwa jina la Bahati, ameonekana akiitikia kwenye kiitikio (chorus) ya video hiyo ambayo tangu iachiwe mapema leo tarehe 7 Machi, 2022 tayari ina watazamaji, 52,000.
Katika kibao hicho, mbali na Odinga na Bahati pia kimewashirikisha wabunge na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Kenya wakiwemo gavana wa kaunti ya Mombasa, Hassan Joho; Junet Mohammed, Alfred Mutua, Babu Owino na wengine.
Kwenye kibao hicho Bahati anaonekana akimsifia Odinga, akisema yeye ndiye kiongozi ambaye anaweza kuleta maendeleo katika taifa hilo na kubadilisha maisha ya vijana wengi ambao wamehangaika kwa muda mrefu bila kazi.
Kibao hicho kinalenga kumpigia kampeni na kuuza sera za kiongozi huyo wa muungano wa Azimio kuelekea Uchaguzi Mkuu wan chi hiyo unaotarajiwa kufanyika Agosti mwaka huu.
Katika kibao hicho pia Bahatia anasema kwamba Odinga ndiye anaweza kumaliza ufisadi nchini humo ambao umedumu kwa muda mrefu.
Ifahamike kwamba hiki ni kibao cha pili kwa Raila Odinga mwaka huu, kibao cha kwanza kilikuwa ni Leo ni leo akiwa amemshirikisha msanii Emanuel Musindi.
Mbali na Bahati, pia Msanii Willy Paul alikuwa ametangaza kuachia kibao na Raila ila bado hakijapakuliwa mitandaoni, huku mashabiki wakijiuliza iwapo anafanya kiki au lah!
Grazie bahati wakati mali