ASKARI wawili wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wanashikiliwa kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga risasi aliyekuwa mlinzi wa baa moja iliyoko maeneo ya Sinza, jijini humo, inayofahamika kwa jina la Board Room. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana tarehe 29 Novemba 2023 na Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, ACP G.J Puppa, askari hao wanadaiwa kutekeleza tukio hilo usiku wa kuamkia jana, baada ya mkujeruhi mlinzi huyo, Razaki Azan, kwa risasi.
Taarifa hiyo imesema kuwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi.
“Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kuwa, askari wawili majira ya Saa sita usiku walimjeruhi mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Razaki Azan mwenye umri wa miaka 29, mlinzi binafsi wa baa ya Board Room, ambaye baadae alipoteza maisha,” imesema taarifa hiyo na kuongeza:
“Jeshi la Polisi tayari limewakamata askari hao na mambo ya kisheria yanakamilishwa na watachukuliwa hatua za kisheria haraka kadri iwezekanavyo kwa kufuata mifumo ya kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani.”
Leave a comment