Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Ndumbaro ataja mambo nane yakufanywa na asasi za kiraia
Habari za SiasaTangulizi

Ndumbaro ataja mambo nane yakufanywa na asasi za kiraia

Spread the love

 

JUKWAA la Asasi za Kiraia (RCSF) za Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu Afrika (ICGLR) limetakiwa kusimamia mambo nane ambayo yatagusa jamii ya wananchi wa nchi 12 za jukwaa hilo. Anaripoti Selemani Msuya, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesemwa na  Waziri wa Sheria na Katiba Dk Damas Ndumbaro wakati akifungua mkutano mkuu wa tatu wa ICGRL unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili kuanzia leo.

Mkutano huo mkuu wa ICGLR unatarajia kuchagua viongozi wapya ambapo kwa sasa Mwenyekiti wake ni Joseph Butiku.

Waziri Ndumbaro amesema jambo la kwanza kwa RCSF katika Ukanda wa Maziwa Makuu ni kusimamia amani na usalama ili kuhakikisha jamii zilizopo zinafanya shughuli za maendeleo bila usumbufu.

“Amani na usalama ni nguzo ya muhimu kwa jamii yoyote, sisi Tanzania tunajivunia amani kuwepo na tutaendelea kusaidia nchi wanachama wa ICGLR ziendelee kuwa na amani,”amesema.

Amesema jambo la pili ambalo anazitaka asasi za kiraia kusimamia ni utawala bora, sheria na demokrasia.

Dk Ndumbaro amesema utawala bora, sheria na demokrasia sio vitu ambavyo vinashuka kutoka angani, bali vinatengenezwa na jamii husika ambapo asasi za kiraia ni moja wadau muhimu.

“Tatizo la nchi za Kiafrika ni kufikiria kuwa utawala bora, sheria na demokrasia vinapatikana kwa wazungu, hii sio kweli, lazima tutengeneze mifumo yetu na sio kukopi, kwa mfano Chancellor wa Ujerumani anaongoza hata miaka 17, ila sisi wananchi wakisema 10 huo ndio utaratibu wetu, hivyo asasi zina wajibu wa kusimamia hilo,” amesema.

Waziri Ndumbaro amesema asasi za kiraia zinapaswa kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi na kwamba mifumo ya kufikia huko haiwezi kuwa sawa kwa nchi zote na kusisitiza kila nchi kutumia mifumo yake.

Waziri huyo wa Katiba na Sheria amesema jambo la nne ni asasi hizo kupigania utengemano wa kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashari (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nyingine ambazo ni muhimu katika kuchochea maendeleo.

“Jambo la tano naomba mjadili uwepo wa vita na mambo yote yanayoweza kusababisha vita na sita mjadili masuala ya kijamii katika nchi wanachama wa ICGLR na zingine,” amesema.

Dk Ngumbaro amesema jambo la saba asasi zinapaswa kujadili mazingira ambapo amesema Tanzania imefanikiwa katika eneo hilo kwa kuwa thelusi moja ya nchi imetunzwa.

Amesema jambo la nane ambalo anatamani kuona asasi za kiraia zinasimamia ni masuala mtambuka ambayo yatahusisha makundi yote kama wanawake, vijana, watoto na wazee ambao wanashiriki katika yote ambayo ameyataja awali.

Waziri Ndumbaro amesema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itatoa ushirikiano chanya kuhakikisha hoja za asasi za kiraia zinafanyiwa kazi.

Amesema pamoja na Serikali kushiriki kufanikisha hilo pia vyombo vya habari vinapaswa kupewa kipaumbele kwa kila hatua.

Joseph Butiku

Mwenyekiti wa RCSF katika ICGLR Joseph Butiku amesema kwa miaka takribani 18 wamekuwa wakijadili mambo ya amani, usalama, demokrasia, utawala bora, maendeleo ya uchumi, mshikamano wa nchi wanachama, vurugu zilizozalisha wakimbizi, mazingira na jinsia kwa ufanisi mkubwa.

Butiku amesema wanazipongeza nchi wanachama wa ICGLR zimekuwa zikitoa ushirikiano kwao jambo ambalo limerahisisha utekelezaji wa ajenda zao.

Mwenyekiti huyo amesema wamekuwa wakisimamia Serikali za nchi wanachama kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa kufuata utawala wa sheria.

“Leo asasi za kiraia za nchi wanachama ICGLR tumekutana hapa Dar es Salaam kujadili mambo mbalimbali ambapo pia tunarajia kesho kufanya uchaguzi kupata viongozi wapya,” amesema.

Butiku amesema ICGLR inahusisha nchi za Afrika ya Kati, DR Congo, Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Zambia, Sudan Kusini, Burundi, Rwanda na Congo Brazzaville ambapo kwa kiasi fulani wameweza kujenga mshikamano.

Amesema jitihada zao ni kuhakikisha mfumo wa sheria unachukua nafasi patika kuendesha nchi zote wanachama.

Naibu Katibu Mkuu wa wa ICGLR Balozi Mohamed Yassir amesema mikakati yao ni kuendeleza mazuri yote ambayo wamekubaliana, ili kuhakikisha nchi wanachama zinapata maendeleo kwa kasi.

“Sisi tumekuwa tukisimamia mipango yetu, pamoja na changamoto ambazo zinatokea, tunaamini tutafanikiwa iwapo mshikamano wa Wadau wote utapewa kipaumbele,” amesema.

Balozi Yassir amesema katika kipindi cha janga la Uviko-19 walipitia wakati mgumu, ila wanaendelea kuimarika siku hadi siku.

Naye Hodan Addou kutoka UN Women akiwamwakilisha Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Ukanda wa Maziwa Makuu amesema wataendelea kushirikiana na ICGLR ili kuhakikisha amani na usalama unaongezeka katika ukanda huo.

Amesema UN Women itashirikiana na ICGLR kuhakikisha kundi la wanawake linapewa msukumo ili liweze kushiri kikamilifu katika kupigania amani na usalama.

Kwa upande wake Dk Majaliwa Marwa kutoka UNFPA amesema watatoa ushirikiano kwa asasi za kiraia ambazo zitakuwa zinapigania haki za raia wake kwa kufuata misingi ya kisheria na utawala bora.

Dk Marwa amesema UNFPA inaamini katika majadiliano ili kuweza kujenga jamii yenye maelewano na maendeleo, hivyo wanazitaka asasi za kiraia kusimamia eneo hilo kama inavyofanya RCSF kupitia ICGLR.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Asasi za Kiraia nchini Kenya Peter Ole amesema asasi za kiraia ndio zimefanya Kenya kuwa nchi ya mfano kwa nchi nyingine hasa mfumo wake wa uchaguzi.

Naye Makamu Mwenyekiti wa CSO Sudan Kusini Akuoch Ajang amesema nchi yao imepitia wakati mgumu ila kupitia ujio wa asasi za kiraia jamii inaanza kubadilika na kutambua haki zao za msingi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Serikali yaanza msako wanaotoa mikopo kausha damu

Spread the loveSERIKALI imeanza kufuatilia watu, vikundi na taasisi zinazotoa kinyume cha...

Habari za Siasa

Spika Tulia aibana Serikali mafao ya wastaafu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Spread the loveSPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameitaka Serikali kufanya tathimini...

Habari za Siasa

Serikali yawapa maagizo Ma-RC udhibiti magonjwa yasiyoambukiza

Spread the loveWAKUU wa mikoa nchini wametakiwa kuandaa utaratibu wa kuwawezesha wananchi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

error: Content is protected !!