Thursday , 2 May 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Mbowe ataja kiapo chake na Rais Samia
Habari za SiasaTangulizi

Mbowe ataja kiapo chake na Rais Samia

Spread the love

MWENYEKITI wa Chama cha Demokraria na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema kusimama katika misingi ya haki na ukweli ndilo agano aliloweka kati yake na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan pindi alipotoka gerezani na kuelekea Ikulu kuonana na Mkuu huyo wa nchi. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Mbowe na wenzake watatu ambao tarehe 4 Machi, 2022 walifutiwa kesi yenye mashtaka ya ugaidi, amesema Rais Samia alikubaliana naye kuendesha serikali kwa misingi ya haki.

“Sisi Chadema – chama kikuu cha upinzani tutaendelea kuhubiri demokrasia na misingi yake yote hadi siku ambayo Mungu atatupa kibali na sisi pengine tuiongoze serikali,” amesema.

Akizungumza katika ibada ya shukrani iliyofanyika leo tarehe 20 Machi, 2022 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Nshara – Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Mbowe amesema amewaomba viongozi wa dini wazungumzie haki bila hofu wakati wowote.

Amesema katika kikao chake cha kwanza baada ya kutoka gerezani alipoenda Ikulu kuonana na Rais Samia alimweleza kuwa watu wengi mioyo yao inavuja damu.

“Pia nikamuambia hofu inayojengwa na wasaidizi wa watawala kwamba wana-Chadema wana vurugu, hawapendi amani ya nchi hii ni maneno ya uongo.

“Chama hiki ninachokiongoza, hakijawahi hata siku moja kuomba serikali ya chama chochote kilichopo madarakani, (serikali ya CCM), hayajawahi kuwa matamanio au maombi yetu washindwe kutekeleza vizuri majukumu yao.

“Tunawaombea wafanye kazi yao kwa uadilifu kwa haki nchi yetu ipate ustawi, ustawi wa Taifa hili ukipatikana wawe Chadema, wasio na chama utaona maisha bora kwa kila mtanzania na hili ndio jambo tunalihubiri,” amesema Mbowe.

Amesema viongozi wa dini wanahubiri amani kila mara kwa sababu wanajua kwamba uchaguzi mkuu haukuwa huru na haki, kuna watu wanatekwa, watu wamefungwa kimakosa.

Amesema kwa kuwa wamekubaliana kukutana kwenye haki, sasa viongozi wa serikali na dini wabadilishe mazoea na kuzungumzia haki.

“Wanachama wa vyama vyote, taifa na raia wote watangulize haki na kila haki ina wajibu wake lakini ni dhahiri kwamba tukikubaliana tutakutana kwenye haki wala hatutagombana.

“Nilimuambia Rais tunakubaliana kwenye hilo, akaniambia tunakubaliana… basi nikamuambia ni jambo jema, ndio hili nalozungumza chini ya paa la Bwana,” amesema.

Amesema baada ya maagano hayo alimuomba Rais Samia watoke mbele ya umma na kutoa kauli pamoja.

“Nikamuambia tukatoe kauli yetu mbele ya dunia, nizungumze na wewe uzungumze, kwamba wewe kama Rais wa chama kinachoongoza Serikali na mimi kama kiongozi wa chama kikuu cha upinzani tukazungumze na dunia na tuweke kauli na kila mmoja asimame kwenye kauli hii na dunia ione,

“Kama sisi tutakuwa wa kwanza kuvunja agano hilo dunia itasema, kama wao watakuwa wa kwanza kuvunja agano hilo, dunia itasema vilevile. Huo ndio msingi,” amesema.

Aidha, amesema anaweza kuwa ametoka Ikulu na mtazamo wake kuhuau haki na Rais akawa na mtazamo wake kuhusu haki.

“Lakini tukikubaliana kama Taifa nini haki za wakulima, wafanyabiashara, watoto wetu, kwa makundi yote hata katika kuwapata viongozi wa kuongoza Taifa letu, hakutakuwa na ugomvi ndani ya taifa,” amesema.

Amesema hata katika chaguzi ili viongozi wapatikane kwa matakwa na mapenzi ya wanaowaongoza ni dhahiri kunahitajika Tume huru ya uchaguzi.

“Hii Tume huru ya uchaguzi, tukubaliane, tunatofatiana wapi, ndio amesema Baba mchungaji Kessy kwamba unajua kuna tatizo hutaki kukiri kuna tatizo.

“Hata katika masuala ya sheria, saa nyingine najiuliza hivi neno Katiba… tunagombania wapi na kwanini tugombane!

“Hawa wanasema wanataka katiba na hawa wanasema wanataka shule, kwani aliyesema anataka shule hataki katiba bora ni nani?, tukae tuzungumze tofauti zetu ziko wapi na hayo tutaendelea kuyafanyia kazi,” amesema.

Aidha, amesema jela ndiko ambapo Mungu hutajwa mara nyingi zaidi.

“Jela wanaamka saa 10 alfajiri wanaimba na kuabudu, na wengine wanajutia kwa makosa waliyoyafanya lakini kwa tukio hili kubwa nilililopitia sijutii kwa kwa niliyopitia najua wazi yalikuwa ni makusudi ya Mungu” amesema.

Pamoja na mambo mengine amewaahidi waumini wa Kanisa hilo ambalo lipo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi kuwa atakwenda kutafuta Sh milioni 100 ili achangie katika ujenzi wa kanisa hilo.

Amesema atafanya hivyo ili iwe kumbukumbu yake ya kukaa gerezani miezi nane Ukonga na kisha kutoka.

“Tukilijenga vizuri hekalu hili la BWANA (Kanisa la KKKT Usharika wa Nshara-Machame), litatoa huduma kwa watu wengi hata wasio na haki, kupitia hekalu la Mungu watasikia neno la Mungu nao hatimaye wataijua haki,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Chadema waendelea kulilia katiba mpya

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeendelea kudai upatikanaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema kumshtaki Rais Samia

Spread the loveCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetishia kumfungulia kesi ya...

Habari za Siasa

Tume huru ya uchaguzi yatangaza uchaguzi mdogo Jimbo la Kwahani

Spread the love  TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi, imetangaza uchaguzi mdogo...

AfyaHabari za Siasa

Dk. Biteko aagiza utoaji huduma saratani usiwe wa kibaguzi

Spread the loveNaibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko...

error: Content is protected !!