MKE wa Mwenyekiti wa Chadema, Freema Mbowe, Dk. Lilian Mtei amesema Baba mkwe wake Aikael Mbowe ndiye aliyekuwa kiongozi wa ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Nshara ambalo lilitumika kufunga ndoa kati yake na mumewe miaka 30 iliyopita.
Amesema katika kanisa hilo lililopo Machame wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, alitambua kuwa limebeba historia kubwa ya familia ya Mbowe baada ya kufunga ndoa Agosti mwaka 1991. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).
Akizungumza katika ibada ya shukrani iliyoendeshwa na Mchungaji Kelvin Kessy, Dk. Lilian amesema baada ya kujiunga na familia ya Mbowe miaka 30 iliyopita ndipo alipopata historia ya kanisa hilo na ukaribu wa familia hiyo.
Amesema kanisa hilo ambalo limevunjwa na sasa linajengwa lingine kubwa, ndilo lililotumika kuwabatiza na kuwabariki watoto wao.
Aidha, akiomba waumini kuunga mkono familia hiyo ya Mbowe katika mchango Sh milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo, Dk. Lilian amesema kanisa hilo limebeba historia ya kipekee ya familia ya Mbowe.
“Ni kanisa ambalo lipo sana kwenye roho zetu ningeomba mtuunge mkono tuweze kulimazia hili kanisa na kutoa mfano kwa vizazi vijavyo.
“Sasa sijui uzao wetu nao watalivunja na wajenge lingine, itategemea watu watakuwa wameongezeka kiasi gani, licha ya kwamba halijakamilika lakini tumekaa ndani watu wengi… mtuunge mkono kuweka alama kwenye kanisa hili,” amesema.
Mbowe na msafara wake wameelekea Hai mkoani Kilimanjaro kwa mara ya kwanza baada ya kutoka gerezani walikodumu kwa zaidi ya miezi nane kabla ya kufutiwa kesi na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP). Mbowe na wenzake watatu walifutiwa kesi hiyo tarehe 4 Machi mwaka huu.
Leave a comment