Thursday , 2 May 2024
Home Habari Mchanganyiko NMB yampongeza Rais Samia kuimarisha sekta ya benki, kuifungua nchi
Habari Mchanganyiko

NMB yampongeza Rais Samia kuimarisha sekta ya benki, kuifungua nchi

Spread the love

 

UTAWALA wa mwaka mmoja wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan umeelezwa kuchangia kuimarika kwa sekta za kibenki kwani imekuwa imara, salama, tulivu na yenye faida kwa iliyosababisha mazingira wezeshi kwa wananchi.

Hayo yamesemwa jana Jumamosi, tarehe 19 Machi 2022 na Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia madarakani.

Rais Samia aliingia madarakani tarehe 19 Machi 2021, baada ya aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli kufariki dunia siku mbili kabla katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo, lilishirukisha watu wa kanda mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania na kufanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na mgeni rasmi alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Kimori alisema sekta ya benki ilishuhudia kukua kwa mizania kwa asilimia 24 hadi kufikia jumla ya mali ya Sh.38.7 trilioni kiasi ambacho ni rekodi kwenye sekta hii.

Alisema sekta ya benki nchini kwa ujumla iliendelea kuwa imara na yenye mtaji wa kutosha huku kwa upande wa faida, kutokana na kasi madhubuti ya mapato, pamoja na kuimarika kwa ubora wa mikopo, benki zote nchini kwa ujumla zilipata faida kabla ya kodi ya mapato ya Sh.1.04 trilioni.

“Hii ni faida ya juu zaidi katika historia ya sekta ya kibenki kwa hapa nchini. Haya yote ni matokeo ya utendaji wako wa kipekee na wa kizalendo pamoja na serikali yako ndani ya mwaka mmoja tu wa Uraisi wako,” alisema Kimori.

Kwa upande wake, Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson alisema nchi imefunguka kiuchumi na mzunguko wa fedha umeimarika hasa baada ya serikali kuhakikisha fedha za bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 zilizopitishwa na Bunge zinafika kwa wingi kuhudumia jamii.

Dk. Tulia alisema kumekuwepo na mazingira wezeshi na rahisi kwa wananchi kujiinua kipato kutokana na shughuli mbalimbali zinazofanyika za kiuchumi, lakini pia huduma muhimu za kijamii ikiwemo afya, maji, umeme na miundombinu kupatikana kirahisi na uhakika.

“Tunapiga hesabu kwa maana ya yale yaliyofanyika kwa mwaka mmoja, kwenye eneo la afya asilimia 62.32 ya fedha zilizotengwa na Bunge katika bajeti zimeshafika maeneo husika, unaweza kuona ni nusu mwaka lakini ameshavuka nusu ya lengo.”

“Upande wa maji asilimia 76.51 ya fedha zilizotengwa zimeshafika kwenye maeneo husika, hizi takwimu nazitaja mpate picha ili ikifika mwezi Juni mwaka huu mjue itafika wapi kwa sababu kazi inaendelea na kuzidi,” alisema Dk. Tulia.

Kwa upande wa Maliasili, asilimia 58.08 ya fedha zimeshafika, sekta ya ujenzi ni asilimia 60.69, sekta ya uchukuzi ni asilimia 23.32, sekta ya elimu ni asilimia 69.31.

Aidha, kwa upande wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo imegusa maeneo mengi ni asilimia 39.46, kwa upande wa mikoa yote asilimia 56.03.

“Kwa ujumla ukifanya tathmini na sekta nyingine unapata wastani wa asilimia 60.5 kutoka Julai 2021 hadi Januari 2022, kwa hivyo Rais Samia anaifanya kazi inaendelea ameweza na kuzidi,” alisema Dk. Tulia

Alisema, “mtakumbuka Rais Samia alipoingia madarakani mwaka 2021 nchi haikuwa imejitayarisha kuwa na mabadiliko, changamoto aliyoikuta ni janga la UVIKO-19, alipoingia alifanya mambo mengi, mfano fedha ambazo alizitafuta kwa kupigana na changamoto hiyo, maarufu Sh.1.3 trilionikutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).

“Hizi fedha katika eneo la afya zimenunua magari ya wagonjwa ya kisasa 20, ya kawaida 365 kama siku zake tunazosherehekea leo (jana), zimejenga vituo vya afya vya dharura nchi nzima, zimeimarisha mfumo wa usambazai na ununuzi mitungi ya gesi nchi nzima, mashine za X-Ray 25, MRI hospitali za taifa, mikoa na kanda, kumejengwa vyumba vya ICU 72 nchi nzima.”

Dk. Tulia aliweka wazi wananchi wanapowasikia wanawake wanampongeza zaidi Rais Samia si kwa kuwa ni mwanamke mwenzao, bali maeneo waliyopunguziwa mzigo ni mengi, kwa kuwa huduma za afya zikipatikana mbali wanaopata tabu zaidi ni wanawake, wanawake ndio wauguza wagonjwa, kama mgonjwa atakuwa mbali atalazimika kulala huko.

Katika maelezo yake, Afisa Mkuu wa Fedha Benki ya NMB, Juma Kimori awali alieleza kuwa katika mwaka mmoja wananchi wameshuhudia mipaka ya nchi ikifunguka na sasa biashara za kimataifa zimezidi kuongezeka.

Watanzania wengi wamepata fursa za kufanya biashara nje ya nchi na kukuza uchumi.

“Ziara zako (Rais Samia) katika nchi mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika zimezaa matunda kwa kipindi kifupi. Zinapopatikana fursa nyingi kwa Watanzania kufanya biashara ndipo na sisi sekta ya kibenki tunapata fursa nyingi zaidi za kufanya biashara hivyo kukua zaidi, na kukua kwetu ndiko kukua kwa uchumi wa nchi yetu,” alibainisha Kimori.

Kuhusu janga la Uviko-19, Kimori alisema Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilichukua hatua kadhaa za kisera kuiimarisha sekta ya benki kwa kuboresha mazingira ya biashara na ufanisi katika utoaji huduma za fedha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

NEMC yatoa elimu matumizi sahihi ya zebaki kwa wachimbaji

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC)...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Oryx gesi yagawa mitungi, majiko 100 kwa waandishi wa habari Dar

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gesi Tanzania imegawa mitungi 100 ya gesi...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mavunde ataja malengo “Vision 2030”

Spread the loveWAZIRI wa Madini amesema dhana ya “Vision 2030” inakusudia kuiendeleza...

Habari MchanganyikoMichezo

Wanamichezo Mei Mosi wachangia wahitaji vitu vya mil. 11.5

Spread the loveWanamichezo wanaoshiriki Michezo ya Mei Mosi Taifa 2024 jijini Arusha...

error: Content is protected !!