November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mahakama yaamuru Zuma arejeshwe gerezani

Jocob Zuma, Rais mstaafu wa Afrika Kusini

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu ya Rufaa nchini Afrika Kusini jana tarehe 21 Novemba, 2022 imesema Rais wa zamani wa taifa hilo, Jacob Zuma, alipewa msamaha wa matibabu na kutoka kwenye kifungo cha gereza alichokuwa akitumikia mwaka 2021 kinyume cha sheria.

Kutokana na msamaha huo, mahakama hiyo imeagiza kiongozi huyo anatakiwa kurejea gerezani kukamilisha kifungo chake. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).

Zuma (80), alihukumiwa kifungo cha miezi 15 gerezani Juni 2021 kwa kutofika mahakamani, hali iliyozua maandamano makali nchini humo.

Hata hivyo, kiongozi huyo alidumu kwa miezi miwili pekee gerezani, ambapo baadaye alipewa msamaha wa matibabu katika hali tatanishi.

Msamaha huo ulitolewa na Mkuu wa Idara ya Magereza nchini humo, licha ya ushauri wa kamati ya matibabu ya idara hiyo kusisitiza kwamba Zuma hakuwa ametimiza masharti ya kupewa msamaha huo.

“Mahakama hii imetoa uamuzi kuwa Zuma alipewa msamaha wa matibabu kinyume cha sheria.

“Kisheria, Zuma hajamaliza kutumikia kifungo chake. Lazima arejee katika Kituo cha Kurekebishia Tabia cha Estcourt ili kukimaliza,” ilieleza taarifa ya mahakama hiyo.

Kulingana na tathmini za kimatibabu zilizorejewa kwenye uamuzi wa mahakama, Zuma ana matatizo ya kiafya yanayohusishwa na mapigo ya juu ya damu, kiwango cha juu cha sukari katika damu yake na matatizo ya utumbo wake.

Zuma, ambaye alikuwa miongoni mwa watu walioukabili utawala wa ubaguzi wa rangi, alichaguliwa kama rais mnamo 2009.

Hata hivyo, alilazimika kujiuzuli mwka 2018 kufuatia madai ya kushiriki katika sakata za ufisadi.

Licha ya tuhuma hizo, bado ana umaarufu mkubwa miongoni mwa wafuasi wa chama tawala cha African National Congress (ANC), wengi wakimuona kama mtetezi wa watu maskini na wanaonyanyaswa.

Wakati kifungo chake cha gerezani kilipotangazwa, maandamano makali yalizuka katika maeneo tofauti nchini humo, hali iliyosababisha vifo vya watu 350. Maduka kadhaa pia yaliporwa.

Huenda agizo hilo la Mahakama Kuu ya Rufaa likapata upinzani kwani Zuma, bado ana nafasi ya kwenda katika Mahakama ya Kikatiba, kwani ndiyo ya juu zaidi nchini humo.

Oktoba mwaka huu wasimamizi wakuu wa magereza walitangaza kuwa kifungo cha miezi 15 alichohukumiwa Zuma kimekamilika.

Tangu wakati huo, amehudhuria mikutano kadhaa ya umma, huku akiimba na kucheza densi mbele ya wafuasi wake.

Pia, amekuwa akimkosoa vikali mrithi wake, Cyril Ramaphosa, kwa madai ya ufisadi na uhaini.

Ramaphosa atashiriki kwenye kongamano muhimu la ANC mwezi ujao Desemba ambapo anatafuta uungwaji mkono wa chama kumuidhinisha kuwania urais kwa muhula wa pili.

Hili linajiri huku akiandamwa pia na tuhuma za ufisadi, kwani anadaiwa kuficha mamilioni ya pesa nyumbani kwake.

error: Content is protected !!