Saturday , 20 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Mkaa endelevu wafanya mapinduzi Morogoro
Habari Mchanganyiko

Mkaa endelevu wafanya mapinduzi Morogoro

Spread the love

 

WANANCHI wa vijiji vya Lulongwe kata ya Matuli na kijiji cha Mlilingwa kata ya Tununguo, Wilaya ya Morogoro mkoani humo, wamesema Mradi wa Mkaa Endelevu (TTCS) umeleta mapinduzi ya kiuchumi, kijamii na maendeleo katika vijiji vyao. Anaripoti Faki Sosi, Morogoro … (endelea).

Wananchi hao wameelezea mradi wa TTCS ulioratibiwa na Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu (MJUMITA), kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), wakati wakizungumza na waandishi wa habari waliotembelea vijiji hivyo jana.

Mkazi wa kijiji cha Mlilingwa Jiwanji Latilali amesema kabla ya mradi wa TTCS kufika alikuwa na hali ngumu ya maisha, ila kwa sasa amepata mafanikio makubwa hadi kujenga nyumba bora na anaisha na familia yake.

“Awali nilikuwa naishi kwa baba, lakini sasa nimejenga nyumba yangu nimeoa, nina mtoto mmoja na kwa kweli mradi huu umenipa maendeleo,” amesema Latilali.

Latilali amesema pamoja na maendeleo ambayo ameyapata, pia kupitia mradi uhifadhi wa misitu umeimarika na kuboreka na kuwataka wanakijiji wenzake kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kuhifadhi misitu.

Naye Nuru Tandawali amesema mradi huo umewezesha kumalizika kwa vitendo vya unyayasaji wa kijinsia kutokana na ushiriki wa jinsia zote kwenye utekelezaji, hali ambayo imeongeza uwezo wa kipato hasa kwa wanawake.

“Wanawake tumekuwa na vipato vya uhakika, unyanyasaji kwenye familia nyingi umekwisha kwa sababu kila mtu anashiriki kwenye uzalishaji mali kupitia mradi huu,” alisema Nuru.

Rogers Kibasindila Mwalimu wa Shule ya Msingi wa Lulongwe amesema mradi huo umeleta mwanga kwenye kijiji hicho hasa kwenye maendeleo ya elimu kwa kujenga nyumba za walimu pamoja na ukarabati wa madarasa .

“Walimu wameacha kupanga mtaani wananchi wametujengea nyumba hapo imetutia moyo wa kufundisha kwa nguvu zote,” amesema.

Shabani Luagwa Mjumbe wa Halmashauri ya kijiji cha Lulongwe amesema mradi wa mkaa endelevu umewawezesha kujenga zahanati ya kisasa, hivyo wataondokana na adha ya kufuata huduma zaidi ya kilomita saba.

“Tumejenga zahazati yetu wenyewe hapa kijijini Lulongwe kupitia mradi wa mkaa endelevu, mwanzoni hatukuwa na uwezo huo kwa sababu kijiji hakikuwa na njia mapato,” amesema Luagwa.

Amesema mradi huo umeondoa ukata kwa wananchi ambapo kwa sasa wananchi wana nafuu ya maisha na upande wa kilimo kimekuwa na tija.

Mwenyekiti wa kijiji cha Lulongwe Azizi Mohammed amesema kuwa mradi huo, umekusanya zaidi ya Sh.milioni 100 tangu uanzishwe mwaka 2017 hali ambayo imechangia miradi ya maendeleo kutekelezwa.

Amesema Sh. milioni 70 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ambapo Serikali imewaunga mkono kwa kumalizia ujenzi huo .

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Matuli,Lucas Lemomo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro amesema kijiji cha Lulongwe kimekusanya fedha zilizoweza kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Tumeweza kufanya ukarabati wa madarasa mawili kwenye Shule ya Msingi Lulongwe kwa Sh. milioni 5, nyumba za walimu Sh.milioni 50, zahanati Sh.milioni 150 ambapo Serikali kuu imechangia Sh.milioni 50,” amesema Lemomo.

Amesema pia wamepata fedha ya ukarabati wa visima vya kijiji hicho vilivyoharibika na kuweka bajeti ya ukarabati kila vikiharibika .

Lemomo amesema serikali imewajengea uwezo wa usimamizi wa pesa wananchi ili kudhibiti ubadhilifu na matumizi yasiyoidhinishwa na kijiji ambapo hakuna pesa inayokaa bila kupitishwa kwenye kikao cha halmashauri ya kijiji.

Mtendaji wa kata ya Mlilingwa, Vicent Clement amesema mradi huo umeharakisha maendeleo kwenye kata hiyo kutokana na mapato yatokanayo na uvunaji wa mkaa endelevu.

Amesema wanakijiji wamefanikisha ujenzi wa shule, mradi wa kuku wa kienyeji, ukarabati wa zahanati na ofisi ya Serikali ya kijiji.

Aidha, amesema mradi huo umewezesha kuwalipia zaidi ya wananchi 100 bima ya afya hali ambayo imeongeza amani kwa wanakijiji.

Mshauri wa Maliasi Mkoa wa Morogoro, Jeseph Chuwa amesema mfumo huo umesaidia kutunza mazingira pamoja na kuingiza mapato mengi zaidi vijijini.

Chuwa amesema mapato yatokanayo na msitu kwenye mko huo ni Sh.bilioni 2.4 ambapo vijiji 35 pekee vinavyotekeleza mradi huo vimechangia zaidi ya Sh.bilioni 1.6 kwenye mapato hayo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Gardner Habash wa Clouds Fm afariki dunia

Spread the loveALIYEKUWA mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wauguzi, madaktari 1000 kugawiwa mitungi ya Oryx Gas

Spread the loveKAMPUNI ya Oryx Gas na Taasisi ya Doris Mollel Foundation...

Habari Mchanganyiko

Tanzania yachaguliwa Makamu wa Rais Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani

Spread the love  TANZANIA kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)...

Habari Mchanganyiko

NEMC yaonya wanaojenga bila tathmini ya mazingira

Spread the loveBARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),...

error: Content is protected !!